1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi lamuunga mkono Zida kuiongoza Burkina Faso

1 Novemba 2014

Jeshi la Burkina Faso lamuunga mkono Luteni Kanali Isaac Zida kuongoza kipindi cha mpito baada ya Rais Blaise Compaore aliyetawala kwa miaka 27 kujiuzulu kutokana na shinikizo la waandamanaji.

https://p.dw.com/p/1DfVl
Luteni Kanali Isaac Zida anayeungwa mkono na jeshi kuongoza kipindi cha mpito Burkina Faso.
Luteni Kanali Isaac Zida anayeungwa mkono na jeshi kuongoza kipindi cha mpito Burkina Faso.Picha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Taarifa iliochapishwa Jumamosi (01.11.2014) baada ya mkutano wa wakuu wa majeshi na kusainiwa na mkuu wa majeshi Generali Navere Honore Traore ambaye awali alisema yenye ndie mwenye kuchukuwa madaraka ya kuongoza nchi imesema "Luteni Kanali Isaac Zida amechaguliwa kwa kauli moja kuongoza kipindi cha mpito kufuatia kujiuzulu kwa rais Compaore."

Kiongozi wa kundi la maafisa vijana wa kijeshi Luteni Kanali Isaac Zida amejitangaza kuwa ndio mkuu wa nchi hiyo na kulipuuzilia mbali tangazo lililotolewa awali na mkuu wa majeshi na mshirika wa karibu wa rais aliyen'golewa madarakani kuwa kusema kuwa "halifai".

Baada ya siku kadhaa za maandamano yaliyowateremsha maelfu ya watu katika mitaa ya mji mkuu wa Ouagadougou, hali ya utulivu imerudi tena Jumamosi (01.11.2014) kwa kufunguliwa kwa maduka na mashirika yaliohusika na maandamano hayo kutowa wito kwa wafuasi wao kusafisha vifusi vilivyoachwa na maadamano hayo.

Zida ajitangaza kuongoza nchi

Akizungumza kwa kupitia televisheni mapema Jumamosi , Zida ambaye anashika nafasi ya pili ya uongozi katika kikosi cha ulinzi cha rais amesema amechukuwa majukumu ya kuwa mkuu wa kipindi cha mpito na mkuu wa nchi kuhakikisha demokrasia inaingizwa kwa utulivu.

Luteni Kanali Isaac Zida.
Luteni Kanali Isaac Zida.Picha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Amesema "matakwa ya kuwa na mabadiliko ya demokrasia ya vijana wa Burkina katu hayatotelekezwa au kukatishwa tamaa."Amesema tangazo lililotolewa awali na mkuu wa majeshi Navere Honore Traore "halifai".

Pia amesema kwamba rais wa zamani Compaore ambaye inasemekana kwamba ameukimbia mji mkuu wa Ougadougou "yuko mahala salama " na " anahakikishiwa usalama wake na afya yake."

Mahala alipo Compaore

Mtawala wa muda mrefu wa Burkina Faso Blaise Compaore ambaye amejiuzulu Ijumaa kutokana na maandamano makubwa dhidi ya utawala wake wa miaka 27 amewasili katika nchi jirani ya Cote d' Ivoire.

Rais aliyetimuliwa madarakani Blaise Compaore.
Rais aliyetimuliwa madarakani Blaise Compaore.Picha: picture alliance/AP Photo/R. Blackwell

Duru za kijeshi za nchi hiyo zilizokataa kutajwa jina zimesema hapo Jumamosi kwamba Compaore alikuwako katika mji wa kitalii wa mwambao wa assinie ulioko mashariki mwa mji mkuu wa kibisahara nchini humo wa Abidjan.

Inaelezwa kuwa amekuwepo katika mji huo tokea asubuhi na hakuwa peke yake kwamba baadhi ya ndughu wa familia walikuwa wameandamana naye.

Awali duru za kidiplomasia za Ufaransa zimeliambia shirika la habari la AFP kwamba Compaore alikuwa amesafiri kuelekea kusini katika mji wa Po karibu na mpaka na Ghana na kwamba alikuwa hakuomba hifadhi nchini Ufaransa mkoloni wa zamani wa nchi hiyo.

Uasi nchini Burkina Faso ambao unalingana na Vuguvugu la Majira ya Machipuko ya Nchi za Kiarabu ulichochewa na mipango ya kubadili katiba kumuwezesha Compaore kusimama tena kugombania uchaguzi mwakani.

Compaore ni miongoni mwa viongozi kadhaa wa kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika ambao wamesalia madarakani kwa miongo kadhaa na takriban wakuu wengine wanne wa nchi barani Afrika wanashinikiza mabadiliko ya katiba kuwawezesha kun'gan'gania madaraka.

Kibaraka wa Compaore

Mkuu wa majeshi Traore alisema hapo Ijumaa kwamba alikuwa anachukuwa madaraka ya kuwa mkuu wa nchi ikiwa ni siku moja baada ya kuamuru kuvunjwa kwa serikali na kutotoka nje kuanzia magharibi hadi alfajiri.

Mkuu wa majeshi General Honore Traore (katikati) akitangaza kuchukuwa majukumu ya kuongoza nchi. (31.10.2014)
Mkuu wa majeshi General Honore Traore (katikati) akitangaza kuchukuwa majukumu ya kuongoza nchi. (31.10.2014)Picha: Reuters/J. Penney

Lakini waandamanaji wengi wanapinga asishike madaraka kwa kuona kwamba ni mshirika wa karibu wa Compaore.

Mwanaharakati wa chama cha Vuguvugu la Wananchi kwa Maendeleo Monou Tapsoaba amekaririwa akisema "Hatumtaki Generali Traore madarakani. Tunahitaji mtu wa kuaminika. Traore ni kibaraka wa Blaise."

Chimbuko la maandamano

Tangazo la kujiuzulu kwa Compaore liliamsha furaha miongoni mwa waandamanaji lakini wengi hawataki Traore awe rais na badala yake wangelipendelea Kouame Lougue waziri wa zamani wa ulinzi na mkuu wa majeshi aliyehitilafiana na Compaore. Lakini kunyamaza kimya kwa Lougue kumetafsiriwa kumaanisha kuwa hana utashi na wadhifa huo.

Vikosi vya usalama wakati wa makabiliano na waandamanaji Ouagadougou. (30.10.2014)
Vikosi vya usalama wakati wa makabiliano na waandamanaji Ouagadougou. (30.10.2014)Picha: Getty Images/I. Sanogo

Nchi hiyo ya Afrika magharibi ilikumbwa na maandamano kwa maelfu ya watu kumiminika katika mji mkuu wa Ouagadougou ambapo takriban watu watatu wameuwawa katika mapambano na vikosi vya usalama.Waandamanaji waliliunguza moto jengo la bunge la nchi hiyo na majengo mengine ya serikali.

Walikuwa wakiandamana kupinga mipango ya Compaore kufanya mabadiliko ya katiba ambayo yangelimruhusu kugombania kipindi cha tano cha urais.Compaore mwenye umri wa miaka 63 ameitawala Burkina Faso tokea alipoingia madarakani kwa njia ya mapinduzi hapo mwaka 1987.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri : Amina Abubakar