1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je,Ugiriki iachiliwe kufilisika?

Prema Martin26 Februari 2010

Waziri Mkuu wa Ugiriki Georgios Papandreou ametoa mwito kwa wabunge kuchukua hatua kali kutenzua mzozo wa fedha nchini humo.Wachambuzi nao wanaonya kuwa Ugiriki ipo katika hatari ya kushindwa kulipa madeni yake.

https://p.dw.com/p/MDL3
Greece's Socialist Prime Minister George Papandreou attends a swearing in ceremony for his new government, at the presidential mansion in Athens, Wednesday, Oct. 7 2009. The Socialist government was formally sworn in, after a crushing weekend electoral victory that ousted the scandal-battered conservatives. Papandreou, 57, will be personally responsible for foreign policy in his new Cabinet _ a position he held in the last Socialist government five years ago. (AP Photo/ Petros Giannakouris)
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Georgios Papandreou.Picha: AP
"Huu ni wakati wa kuchukuliwa hatua." amesema Waziri Mkuu Papandreou akiwasihi wabunge wa upinzani kuunga mkono mipango ya kupunguza matumizi serikalini.  Amesema,"Suali ni, je tutaiachia nchi hii kufilisika au tutachukua hatua."  Matamshi hayo yamezidisha wasiwasi katika masoko ya fedha. Hapo awali, Papandreou alitamka kuwa serikali inaweza kugharimia matumizi yake mpaka katikati ya mwezi wa Machi. Vile vile ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuingilia kati kupunguza kiwango cha riba inayotozwa kwa mikopo ya Ugiriki.

Wachambuzi katika benki ya Goldman Sachs mjini New York, Marekani, wanaonya kuwa Ugiriki inakabiliwa na changamoto kali kujipatia mikopo na huenda ikashindwa kupata fedha za kugharimia matumizi yake. Kwa maoni ya wataalamu hao, itakuwa vigumu sana kwa serikali ya Ugiriki peke yake kujipatia fedha zinazohitajiwa. Hatimae itahitaji kusaidiwa kutoka nje, iwapo kwa msaada wa fedha au kwa mikopo inayodhaminiwa na mwanachama mmoja mmoja katika Umoja wa Ulaya.

Kwa upande mwingine, gazeti la Financial Times nchini Ujerumani limeripoti kuwa benki kubwa nyingi za Kijerumani zimeamua kutonunua hati za serikali ya Ugiriki kwa sababu ya kuhofia hali ya kifedha inayokutikana Ugiriki. Uamuzi wa benki hizo za Kijerumani unatazamwa kama ishara kuwa ni hatari kuwekeza katika hati za serikali ya Ugiriki. Wasiwasi huo uliongezeka baada ya serikali ya Ugiriki kuarifu kuwa tathmini ya nakisi ya bajeti yake ya mwaka 2009 ni asilimia 12.7 ya pato lake la ndani na sio asilimia 3.7 iliyokadiriwa hapo awali. Tarakimu hizo zimedhihirisha hali mbaya sana ya kifedha na uwekaji hesabu mbovu.

Serikali ya Ugiriki inashinikizwa na Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kali zaidi kupunguza matumizi yake katika sekta ya huduma za umma kwa hadi asilimia nne katika mwaka huu. Mapema juma hili, nchini Ugiriki watu waliaandamana kwa maelfu kupinga hatua kali zilizopangwa kuchukuliwa na serikali katika jitahada ya kupunguza nakisi ya bajeti yake.

Police clash with protesters in Athens on Wednesday Feb. 24, 2010. Police fired tear gas and clashed with demonstrators in central Athens on Wednesday as violence broke out after a large protest march against government austerity measures intended to fix the country's debt crisis. (AP Photo/Thanassia Stavrakis)
Polisi wakipambana na waandamanaji mjini Athens.Picha: AP

Nchi zinazotumia sarafu ya Euro katika Umoja wa Ulaya zinafuatilizia kwa makini hali ya uchumi nchini Ugiriki kwani mzozo huo wa fedha umeathiri thamani ya Euro. Waziri wa Fedha wa Luxembourg, Luc Frieden, katika mahojiano yaliyochapishwa leo katika gazeti la kibiashara la Ujerumani, Handelsblatt, amesema, ikihitajika nchi za kanda ya Euro hazina budi kuinusuru Ugiriki kwa maslahi ya mshikamano wa Ulaya. 

Mwandishi:P.Martin/AFPE

Mhariri:Othman,Miraji