1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je,Yemen itaunda makubaliano mapya?

1 Oktoba 2022

Wakati tarehe ya mwisho ya kusitisha mapigano nchini Yemen ikikaribia, raia wanamatumaini kwamba mapatano hayo yatarefushwa wakihofia mapigano yoyote mapya.

https://p.dw.com/p/4HcJq
Jemen Konfliktparteien vereinbaren Gefangenenaustausch
Picha: Fabrice Coffrini/AFP

Vita vya Yemen kati ya waasi wa Huthi wanaoungwa mkono na Iran na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia vimesababisha vifo vya mamia kwa maelfu na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

soma Mjumbe Maalum wa Yemen ataka usitishwaji mapigano urefushwe

Kwa mujibu wa zaidi ya makundi 40 ya misaada ya kibinadamu nchini yemen, Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa, ambayo yalianza mwezi Aprili na kurefushwa mara mbili, yamepunguza majeruhi kwa asilimia 60 na kuongeza mara nne uagizaji wa mafuta katika bandari inayoshikiliwa na waasi ya Hodeida.

Makubaliano hayo yamedumu kwa kiasi kikubwa, ingawa pande zinazozozana zimelaumiana kwa ukiukaji. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito kwa kila upande kurefusha muda wa kusitisha mapigano.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa katibu huyo, Guterres amesihi vyama vya Yemen sio tu kuunda upya bali pia kupanua masharti na muda wa makubaliano hayo.

Matumaini ya raia

Jemen Sanaa | Arbeiter auf einem Dach
Picha: Mohammed Mohammed/Xinhua/picture alliance

Katika mji mkuu wa Sanaa unaoshikiliwa na waasi, Loujain al-Ouazir amekuwa akifanya kazi ya kufuga mbuzi na kuku kwa miaka mitatu kwenye shamba lililo juu ya nyumba ya matofali ya udongo katika jiji hilo la kale.

Ouazir alifanikiwa kulima katika shamba hilo katika miezi ya hivi karibuni kwani mapatano katika eneo hilo yaliruhusu usafirishaji huru wa bidhaa na kupunguza bei ya bidhaa.

soma Pande hasimu zalaumiana juu ya kukiukwa makubaliano, Yemen

Aidha Ouazir amesema amani iliyodumu kwa kiasi cha haja hasa kukomesha mashambulizi ya anga mjini Sanaa kumeunda mazingira salama kwa biashara yake ya kuuza maziwa na mayai.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kumalizika Jumapili, huku Umoja wa Mataifa ukifanya kazi kuhakikisha kila upande unakubali kurefushwa kwa mara nyingine tena.

Chini ya makubaliano hayo, safari za ndege za kibiashara zimeanza tena kutoka mji mkuu unaoshikiliwa na waasi Sanaa hadi Jordan na Misri, wakati meli za mafuta zimeweza kutia nanga Hodeida.

Mafanikio yaliyopatika

Jemen Feuerpause, Ramadan
Picha: Mohammed Huwais/AFP

Mapigano hayo yaliyofuatana yameleta ahueni kwa watu waliochoshwa na miaka minane ya vita, katika nchi ambayo takriban watu milioni 23.4 kati ya milioni 30 wanategemea misaada ya kibinadamu.

soma Je makubaliano ya kusitisha mapigano Yemen yatafanikiwa?

Lakini kumekuwa na maendeleo madogo ya msingi kuelekea kupatikana kwa amani. Mzingiro umesalia katika eneo la Taez, mji wa tatu kwa ukubwa nchini Yemen, ambao unadhibitiwa na serikali lakini umezingirwa na vikosi vya Kihuthi.

Licha ya kusitishwa kwa mapigano, barabara kuu za kuingia na kutoka katika mji wa mlimani bado zimefungwa.

Diego Zorrilla, naibu mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, alisema mapatano hayo yameboresha hali "katika mambo mengi" lakini "maisha yanasalia kuwa magumu" kwa walio wengi.

"Kwa mtazamo wa kibinadamu, kuundwa upya kwa mapatano mnamo Oktoba 2 ni jambo la lazima," Zorrilla alisema.

"Ni utatuzi pekee wa mzozo unaoweza kuruhusu uchumi kuimarika, kuwaondoa watu kutoka kwenye umaskini na kupunguza mahitaji ya kibinadamu."

Mazungumzo ya kufikia makubaliano ya amani ya kudumu bado yamekwama. Mwezi Mei, mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Hans Grundberg, alisema mapatano hayo "yalitoa fursa ya kuondokana na ghasia na mateso ya siku za nyuma".

Upi mwelekeo wa Yemen?

Jemen | Abholzung der Wälder
Picha: Khaled Abdullah/REUTERS

Mchambuzi Thomas Juneau, kutoka Chuo Kikuu cha Ottawa, alisema mapatano hayo "hayajabadilisha chochote" katika suala la kuendeleza mazungumzo ya amani na yalikuwa yakithibitisha "kufeli katika mambo fulani". soma Vita vya Yemen vyasababisha zaidi vifo vya watoto-UNICEF

"Kwa upande wa Huthi, hakuna nia ya dhati ya kujadiliana na kufanya maafikiano na serikali," Juneau alisema.

Kwa upande wa serikali, tofauti kati ya vikundi vingi vya kupinga waasi zimeongezeka.

Kwa Juneau, kuna "ni upuuzi kuunda upya makubaliano ambayo hayafanyi kazi", na ambayo "yanachelewesha kurudi" kwa vurugu.Lakini, aliongeza kusema kwamba "Sioni mbadala mwingine wowote."

//AFP