1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kupunguza joto la dunia zaendelea

1 Desemba 2015

Siku moja baada ya viongozi wa dunia kuonyesha dhamira ya kuungana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, wajumbe wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wanaendelea na mazungumzo muhimu.

https://p.dw.com/p/1HFCj
Frankreich Paris Klimagipfel COP 21 Obama mit Hollande​, Trudeau und Bill Gates
Viongozi Obama na Hollande​, Trudeau na mfanyabiashara Bill Gates mjini ParisPicha: DW/N. Pontes

Wakuu wa mataifa zaidi ya 150 wamekusanyika katika viunga vya jiji la Paris tangu Jumatatu katika jitihada ya kuchapua kasi ya kisiasa katika kile ambacho wengi wamekielezea kuwa fursa ya mwisho ya kuepusha madhira ya mabadiliko ya tabia nchi.

Wakati wa ufunguzi kiongozi mwenyeji wa mkutano huo Francois Hollande amenukuliwa akisema "Matumaini yote ya ubinaadamu yapo katika jitihada zetu".

Marekani na China zatoa ahadi

Marais Barack Obama na mwenziwe wa China Xi Jinping sambamba na viongozi wengine wengi waliapa, kwamba mataifa yao yatapambana kudhibiti hewa chafu, ambayo inasababisha ongezelo la joto duniani. Wameahidi kwamba matokeo ya mkutano huo wa mabadiliko ya tabia nchi yatakuwa kuwepo kwa mkataba wa 2020, ambao utausaidia ulimwengu na vizazi vijavyo.

Xi Jinping Präsident China
Rais wa China Xi JinpingPicha: Reuters/J: Ernst

Rais Obama ambaye leo hii(10-12-2015) anatarajiwa kukutana na viongozi wa visiwa ambavyo vipo hatarini kuzama kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari alisema "Hatma ni moja, ambayo tuna nguvu ya kuibadili, hapa hapa na sasa hivi". Katika mkutano huo Obama atawaelezea viongozi hao jukumu lake katika kusaidia vile visiwa vilivyo katika mazingira magumu sana.

Lakini ahadi kama hizo zilitolewa katika mkutano kama huo wa mazingira wa Umoja wa Mataifa zaidi ya miongo miwili iliyopita.

wasiwasi wa mafanikio

Mchakato wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia mabadiliko ya tabia nchi unakabiliwa na wasiwasi kuhusu matumizi ya nishati ya mafuta, kama tegemeo la dunia na kwamba kutokana na jambo hilo maslahi makubwa yatakuwa hatarini. Kwa miaka kadhaa katika mikutano mikubwa ya mabadiliko ya tabia nchi kumekuwa vitendo vya kunyoosheana vidole, hasa kati ya mataifa tajiri ya masikini juu ya nani hasa anapaswa kubeba mzigo wa uchafuzi wa mazingira.

Mvutano huo umeibuka wazi kabisa hata Jumatatu, siku ya kwanza ya mkutano wa kilele wa maadiliko ya tabia nchi pale ambapo mataifa yanayoendelea yalipoyashambulia mataifa yalioendelea yapohimiza kupunguzwa kwa matumizi ya nishati ya mafuta baada ya wao kupata mafaniko kwa kutumia nishati hiyo hiyo iliyosababisha kiwango kikubwa cha uchafuzi wa mazingira duniani.

Katika hatua nyingine rais wa Ufaransa, Francois Hollande anafanya mkutano na viongozi wa Afrika wenye lengo la kutaka kujua mataifa hayo yanahitaji nini hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchini na kupunguza ongezeko la joto duniani.

Mkutano huo wa leo, ni sehemu ya jitihada pana ya kidemokrasia yenye lengo la kufanikisha makubaliano ya muda mrefu yanayowezekana kufanyika kwa mtaifa yote ya Afrika, kudhibiti uzalishaji wa hewa chafu unaofanwa na mwanadamu. Wanasayansi wanasema hewa hizo zinasababisha mgamdo wa gesi ambayo inasababisha kuyeyuka kwa barafu na kiwango cha bahari kuongezeka na kuongeza hali ya ukame na majanga mengine.

Mwandishi: Sudi Mnette APE/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel