1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

J&J yasitisha majaribio ya chanjo baada ya mtu kuugua

Sekione Kitojo
13 Oktoba 2020

Awamu ya mwisho ya utafiti wa chanjo ya COVID-19 uliokuwa ukifanywa na  kampuni ya Johnson and Johnson umesitishwa  kutokana na mmoja wa watu waliojitolea kufanyiwa uchunguzi kupata ugonjwa ambao haueleweki

https://p.dw.com/p/3jq4x
Österreich Grippeimfpung in Wien
Picha: Lisi Niesner/Reuters

Idadi ya  kesi zilizothibitishwa  za  maambukizi  ya  virusi vya  corona nchini Ujerumani  imeongezeka  kwa  watu 4,122  hadi  jumla  ya watu 329,453, data kutoka  katika  taasisi  ya  udhibiti  wa magonjwa  ya  kuambukiza  ya  Robert Koch, zimeonesha  hii leo. Idadi ya watu waliofariki  hadi  sasa  imepanda  kwa watu 13 hadi watu 9,634, data  hizo zimeonesha. Soma pia: Maambukizi ya Corona yaongezeka Ulaya na Amerika Kusini

Utafiti wa hatua ya juu uliokuwa ukifanywa  na  kampuni ya  Johnson & Johnson  wa  chanjo ya COVID-19 umesitishwa kwa muda wakati  kampuni hiyo  inachunguza  iwapo mmoja  wa watu waliojitolea  kushiriki  katika  chanjo hiyo, alipata ugonjwa  ambao haukuweza kupatiwa maelezo kwa haraka, kama unahusiana na chanjo hiyo.

Mataifa ya Ulaya leo yamekubaliana kuhusu mbinu za pamoja  za kuratibu vizuwizi vya usafiri kutokana  na  janga  la  virusi vya corona, katika  juhudi  za  kufikisha mwisho sheria za kitaifa za kuumba umba ambazo zimejitokeza  wakati huu  wa janga.

Berlin | Geschlossene Bar während Ausgangssperre
Kanuni kali zinachukuliwa katika baadhi ya miji UjerumaniPicha: Fabrizio Bensch/Reuters

Nchini Ufaransa  baraza  la  mawaziri  litakutana  leo kujadili hatua zaidi za kupambana  na  janga  la  virusi  vya  corona, amesema naibu waziri wa nyumba  na  makaazi Emmanuelle Wargon. Alipoulizwa  juu  ya  uwezekano wa  kuweka  marufuku  ya  kutoka nje wakati  wa  usiku  katika  miji kama  paris ambako  kesi  za maambukizi zinaongezeka, alirudia  matamshi ya  waziri mkuu Jean castex kuwa  hatuna  fursa itakayowekwa  kando. Soma pia: Trump arejea kwenye kampeni baada ya kupona COVID-19

Serikali  ya  Uingereza  nayo  huenda  ikaweka  vizuwizi vikali  zaidi kuliko  vya  hivi  sasa  iwapo wimbi la  pili la  maambukizi  litaendelea katika  maeneo yaliyoathirika  zaidi. Waziri mkuu Boris Johnson alitangaza mfumo  mpya wa vizuwizi  kwa  England jana  Jumatatu, ambapo Liverpool  na  eneo lake la Merseyside liliwekwa  katika kiwango cha juu cha  eneo  la hatari, na  vilabu  vya pombe vilifungwa kuzuwia ongezeko la  maambukizi ya COVID-19.

Serikali  ya  Italia  inaimarisha  hatua zake dhidi ya  kusambaa  kwa ugonjwa  huo  wa  COVID-19,  kwa kupiga marufuku  hafla za watu binafsi na marufuku ya watu kuendelea  kuwa  katika  mabaa na mikahawa nyakati za usiku.

Huko Urusi idadi ya  kesi  za  maambukizi  ya  virusi vya corona imepanda kwa watu 13,868 leo, ikiwa  ni rekodi  mpya ya  idadi kwa siku tangu kuanza  kwa  janga  hili mapema  mwaka  huu. India  nayo imeripoti maambukizi  mapya 55,342 leo , ikiwa  ni  ya  chini kwa siku tangu  katikati ya  mwezi Agosti.

dpae / rtre / ape