John Kerry kuzuru mashariki ya kati na Afrika
18 Mei 2013Kerry anatarajiwa kuanza ziara yake mjini Muscat siku ya Jumanne (21.05.2013), ikifuatiwa na Jordan siku ya Jumatano, ambako atakutana na kile kinachoitwa "washirika muhimu wa kimataifa", kuangalia uwezekano wa kupatikana kwa suluhisho la kisiasa kupitia majadiliano nchini Syria , wizara ya mambo ya kigeni nchini Marekani imesema katika taarifa.
Mkutano huo unakuja kabla ya mkutano mkubwa wa kimataifa kuhusu Syria unaopangwa na Urusi na Marekani , na ambao unatarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Siku ya Alhamis na Ijumaa , Kerry anatarajiwa kuzuru Jerusalem na Ramallah kufuatilia mazungumzo juu ya kuleta pamoja Israel na Palestina katika meza ya majadiliano, kujadili amani, taarifa hiyo imesema.
Sherehe za Umoja wa Afrika
Pia siku ya Ijumaa , Kerry anatarajiwa kusafiri kwenda mjini Addis Ababa kushiriki katika sherehe za siku mbili za kuadhimisha miaka 50 tangu kuundwa kwa Umoja wa nchi za Afrika OAU, ambao hivi sasa unajulikana kama Umoja wa Afrika, AU. viongozi kutoka sehemu mbali mbali za Afrika watahudhuria sherehe hizo.
Hapo Mei 26 , waziri Kerry anapanga kurejea mjini Amman Jordan kushiriki katika jukwaa la kiuchumi la dunia.
Wakati huo huo baraza la usalama la umoja wa mataifa linatafakari ombi kutoka kwa maafisa wa ngazi ya juu wa shirika la misaada la umoja huo linalodai kufikishwa kwa misaada katika nchi iliyoharibiwa kwa vita ya syria, hatua ambayo inaweza kusababisha hali ya mivutano baina ya Urusi na mataifa ya magharibi kuhusiana na upelekaji wa misaada ya kiutu kupitia mipakani, wamesema wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa.
Wakimbizi wamiminika nchi jirani
Wakati nchi jirani za Jordan, Lebanon, Uturuki na Iraq zinasumbuka kuhimili wimbi la wakimbizi wanaoingia katika nchi zao , ambao shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, limesema siku ya Ijumaa, (17.05.2013), imevuka idadi ya watu milioni 1.5, maafisa wa umoja huo wameliambia baraza la usalama , kuwa kuna mamilioni ya watu wanaohitaji misaada ndani ya Syria.
Lakini mpambano wa aina hiyo kuhusiana na azimio jipya katika baraza hilo lenye wajumbe 15, ambalo kwa muda mrefu limeendelea kukwama kuhusiana na vipi wanaweza kuushughulikia mzozo wa Syria uliodumu miaka miwili sasa, huenda likaachwa hadi baada ya mkutano wa kimataifa kuhusu Syria utakaofanyika mjini geneva mwezi ujao, wameeleza wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa.
Urusi, mshirika wa karibu wa rais wa Syria Bashar al-Assad na China zimetumia kura ya turufu mata tatu kuzuwia baraza hilo kuchukua hatua dhidi ya Assad, hatua zilizoungwa mkono na mataifa mengine matatu yenye kura hiyo, Marekani, Ufaransa na Uingereza.
Viongozi wa mataifa ya magharibi wamechukua tahadhari kuhusu uwezekano wa mafanikio ya mkutano wa syria mjini Geneva kuwa unaweza kupata kufikia kuondoa mkwamo, na mapendekezo ya Urusi kuwa Iran ni lazima ihudhurie katika mazungumzo hayo yameanza kufanya mambo kuwa magumu.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / dpae
Mhariri: Caro Robi