1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Kerry ziarani Moscow

7 Mei 2013

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amewasili Moscow kwa mazungumzo pamoja na rais Vladimir Putin kuhusu mzozo wa Syria na jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya mahasimu hao wawili wa vita baridi.

https://p.dw.com/p/18TOk
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry akiterema ndani ya ndege ya serikali yakePicha: Reuters

Mara baada ya kutuwa katika uwanja wa ndege wa Moscow-Vnoukovo,John Kerry ameweka shada la mauwa mbele ya kaburi la mwanajeshi asiyejulikana karibu na ikulu ya rais-Kremlin kabla ya kukutana na rais Vladimir Putin.

Hii ni ziara yake ya kwanza rasmi na tete kama waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani nchini Urusi ,ziara inayofanyika katika wakati ambapo uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeharibika vibaya sana tangu mwaka mmoja uliopita.

Ziara hii inatokea wakati mmoja na maadhimisho ya kurejea Kremlin Vladimir Putin,May 7 mwaka 2012.

Syria ndio mada itakayohodhi mazungumzo kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na rais Vladimir Putin,pamoja pia na mzozo wa Korea.Afghanistan na mada nyenginezo zinazohusu nchi hizo mbili na pia za kimataifa.

"Ni nadra kupata fursa ya kuzungumza ana kwa ana na rais Putin" alisema mwanadiplomasia mmoja wa Marekani kabla ya waziri John Kerry kuondoka Washington na kuongeza "Moscow imesema wazi kabisa inataka kuzungumzia suala la Syria.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amepangiwa pia kukutana na waziri mwenzake Serguei Lavrov.

Mapigano yaendelea nchini Syria

Israelische Armee in Alarmbereitschaft
Jeshi la Israel limewekwa katika hali ya tahadhari katika milima ya GolanPicha: Reuters/Baz Ratner

Nchini Syria kwenyewe,waasi wamekanusha madai ya mjumbe wa tume ya uchunguzi ya Umoja wa mataifa aliyedai huenda waasi wametumia gesi ya sumu inayouwa neva za binaadamu-Sarin."Hatuna gesi ya sarin na hatudhamirii kuwa nayo" amesema Luai al Mekdad ambae ni msemaji wa jeshi huru la Syria,alipohojiwa na shirika la habari la Ujerumani dpa.

Wakati huo huo waasi wanadai kuiangusha helikopta ya jeshi la serikali katika mkoa wa mashariki wa Deir al Zaour na kuwauwa wanajeshi wanane.

Mapigano yanaendelea pia katika mkoa wa kakazini wa Idlib kati ya viklosi vya serikali na waasi wanaopigania kuudhibiti uwanja wa ndege wa kijeshi wa abu Al Dhuheir.

Na msemaji wa jeshi la Israel amesema kombora lililoripuliwa toka Syria limeangukia katika eneo linalokaliwa la milima ya Golan.Makombora mawili yaliangukia jana pia katika eneo hilo la milimani la Syria linalokaliwa na Israel.

Tukio hilo limejiri katika wakati ambapo hal ni tete kati ya Syria na Israel baada ya ndege za Israel kuihujumu mara mbili Syria Ijumaa na jumapili iliyopita.Afisa mmoja wa serikali amesema Syria itajibu "kwa wakati muwafaka" mashambulio hayo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman