1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli kumrithi Kikwete kama rais wa Tanzania

Admin.WagnerD4 Novemba 2015

Tanzania kunashuhudiwa doria kubwa ya vikosi vya polisi vilivyowekwa ili kukabiliana na vuguvugu lolote la maandamano yaliyopangwa kufanywa na wafuasi wa Chadema wanaopinga ushindi wa John Magufuli

https://p.dw.com/p/1GzM5
Tansania Präsidentschaftswahl Nationalflagge
Picha: DW/M. Khelef

Vikosi vya polisi kuanzia vile vyenye magari makubwa ya kuwasha washa mpaka wale wenye silaha na mbwa vimekuwa vikiranda katika mitaa mbalimbali ya miji katika kile kinachotafsiriwa na wengi ni kuwa mkakati wa jeshi hilo kuwadhibiti wafuasi wa upinzani walioko kwenye mkakati wa chini kwa chini wa kuendesha maandamano ya amani.

Jaribio la wafuasi hao wa upinzani kuanzisha maandamano hayo yaliyotajwa kuwa yasiyo na ukomo kwa nchini nzima, limegonga mwamba huku jeshi hilo la polisi likionya kufanyika kwa maandamano yoyote hasa wakati huu kukiwa na hekaheka za maandalizi ya kumwapisha rais wa awamu tano anayetarajiwa kula kiapo chake tarehe (05.11.2015).

Hata hivyo wapinzani hao wameapa kuendesha maandamano hayo licha kwamba hadi dakika hii bado haijafahamika wazi yatafanyika lini na kwa mfumo wa aina gani. Kutokana na sokomoko hilo jeshi la polisi limemwaga maafisa wake mitaani, wanaranda randa huku wakichunga mwenendo wa kila raia.

Hisia za wakaazi

Hali hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na wakazi wengi wa maeneo ya mijini, huku wengine wakisema kuwa kitendo hicho siyo cha kawaida hasa kwa nchi kama Tanzania ambayo wakati wowote imekuwa ikihubiri amani na mshikamano.

Tansania Wahlen John Magufuli
Rais mteule wa Tanzania John Pombe MagufuliPicha: Reuters

"Kwa jumla ninavyoona askari ni wengi, wanapita na maji ya washa washa na kusimama barabarani, watu wanawacha kufanya kazi zao kwa hofu, sasa maendeleo nayo yanazidi kushuka " alisema raia mmoja wa Tanzania.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, kushuhudia vikosi vya serikali vikiendelea kuranda randa mitaani baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu. Baadhi wanaikosoa serikali, wakisema kuwa imekuwa ikitumia nguvu kupindua katika eneo lisilostahili.

Kumekuwa na ongezeko la malalamiko kutokana na uwingi huo wa askari mitaani huku baadhi wamesema kuwa hali hiyo inawatia woga na hata wakati mwingine wanashindwa kuendelea na shughuli zao za kawaida.

"Nadhani serikali ya chama cha CCM inaweka mkazo katika suala la kudhibiti watu, badala ya kulitumia jeshi kufanya kazi zake ambazo ni za kulinda raia," alisema raia mwengine wa Tanzania.

Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa pia chopa za jeshi hilo la polisi zikipiga doria katika maeneo kadhaa huku jeshi hilo likisisitiza kuwa hali hiyo ni moja ya sehemu yake ya kuimarisha hali ya usalama hasa pale kunapojitokeza kwa hali ya sintofahamu.

Ulinzi huo ukiimarishwa wakati ambapo maandalizi ya kumwapisha rais mteule yakiwa yamekamilika na taarifa zinasema kuwa jumla ya marais nane wanatarajiwa kuhudhuria sheria hizo.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri: Yusuf Saumu