1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jonathan kuwania muhula mwengine

14 Januari 2011

Chama tawala nchini Nigeria cha PDP kimemchagua kwa kura nyingi rais aliye madarakani Goodluck Jonathan kuwania tena wadhifa huo katika uchaguzi ujao.

https://p.dw.com/p/zxTc
Goodluck Jonathan,Rais wa NigeriaPicha: AP

Jonathan Goodluck ambaye ni Mkristo anayetokea jimbo lililo na utajiri mkubwa wa mafuta la Bayelsa, alipata kura nyingi si tu za eneo la kusini atokeako bali pia kaskazini kuliko na wakaazi wengi wa kiislamu.Ifahamike kuwa mpinzani wake mkuu,Makamu wa rais wa zamani Atiku Abubakar anatokea eneo hilo la kaskazini.Uchaguzi umepangwa kufanyika tarehe 9 mwezi wa Aprili.

Ushindi wa kishindo

Rais aliye madarakani Goodluck Jonathan alipata ushindi wa kishindo katika kongamano la chama chake tawala cha PDP lililofanyika katika eneo la Eagle lililo katikati mwa mji wa Abuja.Mgombea huyo alijinyakulia kura 2,736 naye mpinzani wake mkuu,makamu wa rais wa zamani Atiku Abubakar alipata kura 805 kama ilivyotangazwa baada ya zoezi hilo muhimu.

Nigeria Korruption
Mabango ya wagombea wa Urais:Uchaguzi umepangiwa Aprili 9Picha: DW/Katrin Gänsler

Mgombea wa kaskazini?

Goodluck Jonathan amekuwa rais wa Nigeria kwa kipindi cha miezi minane iliyopita tangu afariki Umaru Yar'Adua aliyetokea eneo la kaskazini.Kwa mantiki hiyo, mgombea wa urais anatakiwa kutokea eneo hilohilo la kaskazini kama wanavyohisi baadhi ya wakaazi walioupinga ushindi huo.Kulingana na makubaliano yaliyopo ya PDP,uteuzi wa mgombea wa rais unapaswa kuwa wa kupokezana kati ya eneo la kusini na kaskazini kila baada ya miaka minane.Chama cha PDP kimekuwa uongozini kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita na Jonathan Goodluck huenda akawa chaguo la wengi katika uchaguzi ujao wa Aprili ijapokuwa kuna mivutano ya ndani chamani.Endapo atashinda katika kinyang'anyiro hicho, Goodluck Jonathan atakuwa rais wa kwanza anayetokea eneo la Bonde la Niger kuliko na mafuta mengi kadhalika mwakilishi wa kabila dogo zaidi ikilinganishwa na yale ya Yoruba,Hausa,Fulani na Igbo.Uteuzi huo umezua mitazamo tofauti.Hata hivyo mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi ya Nigeria,INEC,Attahiru Jega anasisitiza kuwa,"Sidhani tukio hili limeitia doa hadhi ya tume huru ya uchaguzi.Aghalabu, tunasisitiza kuwa,tutakuwa wazi na huru mahsusi kwa raia wa Nigeria", na shabaha yao ni kuwatendea raia wote haki.

Hotuba ya maneno makali

Vize Präsident Atiku Abubakar, Nigeria
Makamu wa rais wa zamani wa Nigeria,Atiku AbubakarPicha: AP Photo

Kwa upande mwengine,mpizani mkuu,Atiku Abubakar,mfanyabiashara anayetokea eneo la kaskazini na kabila la Hausa alitaraji kuungwa mkono na wafuasi wa eneo lake.Alijinyakulia kura katika majimbo ya kaskazini ya Kano,Sokoto na Zamfara.Kwa mujibu wa meneja wake wa Kampeni,Ben Obi,hila ilitokea na baadhi ya orodha za wajumbe zilikuwa na dosari.Kwa upande wake Atiku Abubakar alitoa hotuba iliyokuwa na maneno makali katika kongamano hilo iliyomlaumu Jonathan kwa kuzikiuka sheria za uchaguzi huo.

Jonathan wa kabila la Ijaw aliingia madarakani baada ya Umaru Yar'Adua kufariki dunia mwezi wa Mei mwaka uliopita.Hata hivyo mtazamo mwengine unaashiria kuwa Nigeria imekomaa kisiasa na inajisogeza mbali na siasa zinazojikita katika misingi ya kikabila.

Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-RTRE/AFPE
Mhariri: Miraji, Othman