1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jopo la marais wahitimisha kikao chao Cote d'Ivoire

23 Februari 2011

Jopo la marais wa Kiafrika linaloushughulikia mzozo kisiasa nchini Cote d`Ivoire limekamilisha ziara yao ya siku mbili ya Abidjan bila ya kupata suluhu ya moja kwa moja

https://p.dw.com/p/10NFq
Alassane Ouatarra na mpinzani wake Laurent GbagboPicha: AP/DW

Wakati huohuo,mapigano yanaripotiwa kuendelea kati ya wanajeshi na wafuasi wa mgombea wa urais Alassane Ouatarra.Mzozo huo wa kisiasa unasababishwa na duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliozua utata.Mpaka sasa mshindi wa moja kwa moja hajapatikana.

Serikali ya umoja wa kitaifa

Katika taarifa yao iliyochapishwa hapo jana,Umoja wa Afrika ulieleza kuwa ujumbe wa jopo hilo la marais wanne wa Afrika Kusini,Chad,Mauritania na Tanzania walifanya vikao vya ngazi ya juu na washirika wote wakuu.Marais hao wanatazamiwa kukutana tena katika kipindi cha siku kadhaa zijazo ili kuijadili hatua itakayofuatia.Kwa mujibu wa Rais wa Afrika Kusini,Jacob Zuma,harakati zao zilijikita katika suala la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa mpaka pale uchaguzi mpya utakapofanyika.

Kwenye kikao hicho,Ouatarra aliwalaumu wafuasi wa mpinzani wake wa kisiasa Laurent Gabgbo wanaodaiwa kuwazuwia kwa nguvu wafuasi wake mwanzoni mwa wiki hii.Ouatarra amekuwa akisiistiza kuwa hasimu wake anatumia mamluki katika operesheni za mauaji,''Mamluki wanakuja hapa na kuifanya shughuli hiyo kwa pesa….sio kuuawa.Kumuondoa Gbagbo haraka iwezekanavyo ni jambo litakalokuwa na manufaa kwetu sote."

Elfenbeinküste Wahl und Unruhen Flash-Galerie
Wafuasi wa wanasiasa wanaoshinda kuwa rais wa nchi:Kuzuka fujo ndio wasiwasi uliopoPicha: picture alliance/dpa


Amani ndilo la msingi

Kulingana na mwandishi wa habari wa shirika la AFP,kiasi ya watu 12 waliuawa katika purukushani hizo.Akizungumza kwenye kikao hicho,kiongozi wa jopo hilo,Rais wa Mauritania Mohamed Ould Abdel Aziz alisema kuwa ana imani matokeo ya harakati zao yataipa kipa umbele amani ya kudumu kote barani Afrika.Kauli hizo zinaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika,Jean Ping aliyeyasema hayo pindi jopo hilo lilipoteuliwa aliposisitiza kuwa,"Tutatumia mbinu zote ili tufikie matokeo tunayoyataka….ambayo ni kuidumisha demokrasia.Naamini kuwa tukifanya hivyo tutafanikiwa bila ya kutumia nguvu.

Jopo hilo lililoteuliwa na Umoja wa Afrika ni sehemu ya juhudi za kuutanzua mzozo wa kisiasa wa Cote d'Ivoire uliosababisha mauaji ya kiasi ya watu 300 tangu ifanyike mwezi Novemba mwaka uliopita duru ya pili ya uchaguzi wa rais.Laurent Gbagbo na mpinzani wake mkuu wa kisiasa,Alassane Ouatarra wote wanadai kuwa washindi wa kinyang'anyiro hicho.

Elfenbeinküste Thabo Mbeki Besuch
Rais wa Afrika Kusini wa zamani Thabo Mbeki na Alassane OuatarraPicha: AP

Vijana waliojawa ghadhabu

Wakati wa ziara yao hiyo ya kilele,Rais wa Afrika Kusini,Jacob Zuma,alizingirwa na vijana waliojawa na ghadhabu wanaomuunga mkono Laurent Gbagbo.Mwenzake wa Burkina Faso,Blaise Compaore alijiondoa kwa kuhofia hali kama hiyo.Vijana hao wa kundi la Young Patriots,walitishia kuuvamia uwanja wa ndege ulioko mjini Abidjan,kwa minajili ya kumzuwia kuingia nchini humo, Rais Compaore anayeaminika kuwa anamuunga mkono Alassane Ouatarra.Vitisho hiyvo ndivyo vilivyowafanya

wajumbe wa Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya magharibi,ECOWAS,wajiondoe hapo jana Jumanne kwenye jopo hilo lililoteuliwa kuushughulikia mzozo wa Cote d'Ivoire.Kwenye taarifa yao,wawakilishi wa Jumuiya ya ECOWAS waliulaumu Umoja wa Afrika kwa kuendelea na hatua hiyo bila ya rais Compaore.Hata hivyo bado wanaendelea kuziunga mkono harakati hizo za usuluhishi.

Kwa upande mwengine,ghasia ziliendelea Cote d'Ivoire ijapokuwa juhudi za upatanishi nazo zilikuwa zimeshika kasi.Kiasi ya watu watatu wanaripotiwa kuuawa katika mtaa mmoja ulio ngome ya wafuasi wa Ouatarra.Itakumbukwa kuwa siku ya Jumamosi wiki iliyopita,wafuasi wa Ouatarra walitishia kuwa wanaandaa maandamano ya ghasia ya kudai demokrasia kama yale yaliyotokea Misri hivi karibuni.

Elfenbeinküste Landwirtschaft Kakaobohnen Flash-Galerie
Zao la Kakao:Cote d'Ivoire ndiyo mzalishaji mkubwa wa Kakao ulimwenguniPicha: DW

Kakao kutouzwa nje

Hapo jana,Ouatarra aliamuru muda wa marufuku ya kuuza kakao nje uongezwe hadi ifikapo katikati ya mwezi ujao wa Machi ili kulibana pato la zao hilo,fedha anazozitumia Laurent Gbagbo kufadhili harakati zake.

Wajibu wa jopo hilo la marais ni kutafuta suluhu ya kudumu ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Februari.

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman