1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jopo maalum la wapiga kura kuamua Marekani

Admin.WagnerD19 Desemba 2016

Jopo maalum la wapiga kura katika majimbo yote ya nchi hiyo watapiga kura ya kuamua juu ya kumuidhinisha rasmi Donald Trump kama rais wa Marekani,

https://p.dw.com/p/2UY0o
USA Proteste gegen Donald Trump in Los Angeles
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/M. Nelson

 Ikiwa ulidhania Wamarekani walishamaliza uchaguzi wao tangu mwezi Novemba basi umekosea. Leo Jumatatu jopo maalum la wapiga kura katika majimbo yote ya nchi hiyo watapiga kura ya kuamua juu ya kumuidhinisha rasmi Donald Trump kama rais wa Marekani, huu ukiwa ni mchakato unaotegemewa na wanaompinga Trump kujaribu kwa mara ya mwisho kumpokonya nafasi ya kuingia Ikulu ya White House. 

Maandamano yamepangwa kufanyika katika miji mikuu ya majimbo mbali mbali ya nchi hiyo ingawa maandamano yenyewe hayategemewi kutoa  ushawishi wowote kwa wapiga kura hao kumbwaga Trump.Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Associated Press kuhusu wapiga kura hao umeonesha kwamba hamasa ni ndogo mno ya kuweza kuwafanya kuamua kuwapigia kura wagombea mbadala.

Jopo maalum la wapiga kura wa chama cha Republican wanasema wamekuwa wakipokea simu chungunzima,barua pepe na hata barua za kawaida zikiwataka wasimuunge mkono Donald Trump.Mpiga kura mmoja wa jimbo la Mississippi  wa chama cha Republican Yerger Jr anasema amepokea maelfu ya barua pepe  zinazomshauri asimpigie kura Trump lakini amesema barua zote hizo amezitupilia mbali.

USA Donald Trump 'Thank You Tour'
Picha: picture-alliance/dpa/D. Anderson

Kimsingi utaratibu huu wa jopo maalum kupiga kura ya maamuzi nchini Marekani ulipitishwa katika mkutano mkuu  kuhusu katiba ya nchi hiyo mwaka 1787.Ni mchakato uliopitishwa ili kumaliza tafauti iliyokuwepo kati ya wale waliounga mkono rais achaguliwe na kura za wananchi waliowengi na upande ule wa watu waliopinga wananchi washirikishwe katika uchaguzi wa rais.

Jopo hilo la wapiga kura maalum au kile kinachoitwa (Electrol College) lina wajumbe 538 idadi ambayo inagawanywa katika kila jimbo kwa kuzingatia jimbo lina wawakilishi wangapi bungeni na maseneta.Ingawa pia jimbo la Columbia  linapewa wajumbe watatu licha ya kwamba eneo hilo halina mbunge hata mmoja.Ili mtu akabidhiwe urais nchini Marekani analazimika kushinda alau kura 270 za wajumbe hao.Majimbo mengi kwa kawaida yanampa kura zote za wajumbe maalum mgombea yoyote anayeshinda kura za wananchi.

Baadhi ya wanasiasa wa chama cha Demokrat wamelalamika kwamba mfumo huu sio wakidemokrasia kwasababu unatoa nguvu nyingi kwa majimbo ambayo yana idadi ndogo ya wananchi.Na hiyo pia ndiyo sababu iliyomfanya Hillary Clinton mgombea wa chama hicho cha Demokratic aliyepata kura milioni 2.6 zaidi za wananchi dhidi ya Trump nchi nzima ashindwe katika uchaguzi wa rais na mpinzani wake huyo wa chama cha Republican.

Baada ya mchakato wa leo wa kupiga kura kikao maalum cha pamoja cha bunge la Marekani kitafanyika Januari 6 kuidhinisha matokeo ya mchakato wa uchaguzi wa leo ambapo makamu wa rais Joe Biden ataongoza kikao hicho kama spika wa baraza la Seneti.Na pindi matokeo hayo yatathibitishwa basi mshindi ambaye mara hii huenda ni Trump ataapishwa kuwa rais wa Marekani Januari 20.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga