1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jordan yawashambulia wanamgambo wa IS

Mjahida6 Februari 2015

Waziri wa mambo ya kigeni wa Jordan Nasser Judeh amesema mashambulizi ya angani yanayofanywa na nchi yake dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu ni mwanzo tu wa majibu kwa kundi hilo, kufuatia mauaji ya rubani wake

https://p.dw.com/p/1EWSA
Ndege za Jordan
Ndege za JordanPicha: Reuters/M. Hamed

Jeshi la Jordan limesema limeanzisha mashambulizi mapya ya angani kupitia ndege zake za kivita dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu nchini Syria. Jeshi hilo limesema linalenga maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo pamoja na kambi zao za mafunzo.

Hatua hii imetokea baada ya rubani wa Jordan Moaz al Kassasbeh aliyekuwa na miaka 26, kuuwawa kwa kuchomwa moto akiwa hai baada ya kuchukuliwa mateka na wanamgambo hao kufuatia ndege yake ya kivita kuanguka karibu na eneo wanalolidhibiti.

Kifo chake kimesababisha hasira kubwa miongoni mwa raia nchini Jordan, wanaotaka serikali kulishambulia kundi la wanambambo wa IS. Kwa upande mwengine maafisa wa Marekani wamesema ndege zao aina ya F-16 na F-22 zilitoa ulinzi kwa ndege za Jordan wakati wa mashambulizi dhidi ya IS.

Babaka rubani aliyeuwawa akizungumza wakati wa maombolezo
Babaka rubani aliyeuwawa akizungumza wakati wa maombolezoPicha: Reuters/M. Hamed

Marekani pia imepeleka ndege zake nyengine pamoja na wanajeshi Kaskazini mwa Iraq ili kuwaokoa marubani ambao ndege zao zitadunguliwa kutoka angani wakati wa mashambulio dhidi ya IS karibu na mpaka wa Syria.

Zaidi ya watu laki mbili wameuwawa nchini Syria tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mwaka wa 2011 kati ya vikosi vya serikali na makundi ya waasi hatua iliyotoa muanya kwa wanamgambo wa kiislamu kuingia huko na kuanza kudhibiti maeneo kadhaa nchini humo na katika taifa jirani la Iraq.

Huku hayo yakiarifiwa Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan aliitembelea familia ya rubani Kassasbeh kutoa rambi rambi zake. Familia ya rubani huyo imeihimiza serikali kulipiza kisasi kwa kulisambaratisha kundi hilo la wapiganaji wa jihadi.

Maandamano ya mshikamano na familia ya Moaz yafanyika Jordan

Kwengineko maandamano yanaendelea mjini Amman na maeneo mengine nchini Jordan ya kuonesha mshikamano na familia ya rubani huyo. Siku ya Jumatano Jordan iliwanyonga wanawake wawili raia wa Iraq waliokuwa katika kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya ugaidi. Sajida al-Rishawi na Ziad al-Karboli, walinyongwa muda mfupi baada ya kutolewa mkanda wa video ulioonyesha mauaji ya rubani wa Jordan.

Wanamgambo wa dola la kiislamu awali walidai kuachiwa kwa wafungwa hao ili Rubani Kassasbeh aachiwe huru, lakini walitekeleza mauaji hayo hata kabla ya majadiliano juu ya hilo kumalizika.

Rubani wa Jordan aliyeuwawa Moaz al Kassasbeh
Rubani wa Jordan aliyeuwawa Moaz al KassasbehPicha: picture-alliance/dpa/Jordan News Agency

Aidha rais wa Marekani Barrack Obama aliyekuwa mwenyeji wa mfalme Abdullah katika ziara yake nchini Marekani kabla ya kurejea nyumbani nchini Jordan amelaani vikali mauaji ya Moaz al Kassasbeh.

Wanamgambo wa IS tayari wameshatekeleza mauaji ya waandishi habari wawili wa Marekani, mfanyakazi wa misaada ya kiutu wa Marekani, na wengine wawili wa Uingereza na baadaye kutuma mikanda ya Video ilioonyesha mauaji yao waliyoyafanya kwa kuwakata vichwa. Kundi hilo pia limemuua mateka wa pili raia wa Japani.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo