1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joto la uchaguzi Tanzania: Suluhu aweka mambo wazi

Daniel Gakuba
27 Agosti 2019

Kwa mara ya kwanza, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu, ameingia kwenye orodha na wale wanaobainisha misimamo hiyo, akisema hana nia ya kuwania urais wa Zanzibar kama wengi wanavyodhania.

https://p.dw.com/p/3OY4a
Samia Suluhu, Vizepräsidentin Tansania
Samia Suluhu, Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaPicha: DW/Said Khamis

Licha kwamba imesalia miezi 14 kwa Watanzania kurudi tena kwenye vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mkuu mwingine, tayari minong'ono ya hapa na pale imeanza na joto la uchaguzi huo limeanza kupanda miongoni wanasiasa.

Katika taifa ambalo lina utamaduni wa rais aliyepo madarakani kutawala vipindi viwili mutawaliya, ni wazi kuwa mwenyekiti wa chama tawala cha mapinduzi, Rais John Magufuli, atakiomba tena chama chake kumpa ridhaa ya kutetea urais wa Muungano akipambana na wagombea wa upinzani.

Hata hivyo, kwa miezi kadhaa sasa ndani ya CCM kwenyewe kumekuwa na kile kinachoelezwa kuanza kujitokeza makundi ya kimkakati kuelekea kwenye uchaguzi huo. Na hata kama hakuna mwanasiasa aliyejitokeza hadharani, hata hivyo baadhi ya vigogo wamekuwa wakitajwa mara kwa mara kwamba huenda wakachukua fomu kupambana na Rais Magufuli kusaka ridhaa ya CCM.

Soma zaidi: Bunge la Tanzania lataka malipo ya Tundu Lissu yasimamishwe

Lakini baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema yale yanayaonza kushuhudiwa sasa ndani ya chama hicho ni sehemu ya muendelezo wa mazoea ya mambo yanayojitokeza wakati unapokaribia uchaguzi mkuu.

Tundu Lissu kujitosa?

Nje ya CCM, wameshajitokeza wanasiasa wa upinzani wanaoonekana kuendesha mikakati ya ndani kwa ndani kuelekea uchaguzi. Tayari mwanasiasa machachari, Tundu Lissu, ameeleza shabaha yake kuhusu uchaguzi huo.

Tansania - Tundu Lissu
Tundu Lissu, miongoni mwa wapinzani wanaokikodolea macho kiti cha urais wa TanzaniaPicha: DW

Hali ikiwa hivyo kwenye kiwango cha Jamhuri ya Muungano, upande wa Zanzibar kunatarajiwa kuwa na kinyang'anyiro kikubwa zaidi kwa kuwa kiongozi wa sasa wa visiwa hivyo vyenye mamlaka ya ndani, Rais Ali Mohamed Shein, anamaliza muda wake na hivyo kuhitajika mtu wa kurithi kiti hicho.

Soma zaidi: Rais wa Tanzania akabidhiwa uenyekiti wa SADC

Miongoni mwa waliokuwa wakitajwa kuwa na nia hiyo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na ambaye anatokea Zanzibar, Samia Suluhu, ambaye hata hivyo, hapo jana aliamua kulishusha mapema joto la uchaguzi huo kwa kutangaza kwamba kamwe hana ndoto yoyote ya kuwania urais wa Zanzibar. 

Samia Suluhu asema ameridhika

Akizungumza kwenye mkutano wa jimboni kwake Makunduchi, kusini mwa kisiwa cha Unguja, iliko ngome madhubuti ya CCM, makamu huyo wa rais ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya serikali ya Zanzibar kabla ya kuhamia serikali ya Muungano alikokuwa waziri na baadaye naibu spika katika bunge maalum la katiba, alisema ametosheka na nafasi aliyonayo sasa:

Mama Samia anakuwa kigogo wa kwanza ndani ya CCM kuweka bayana msimamo wake kuhusu mbio za urais katika visiwa vya Zanzibar. Hata hivyo, kumbukumbu zinaonesha kuwa rais anayemaliza muda wake, Dk Shein, aliachia nafasi ya makamu wa rais wakati wa utawala wa awamu ya nne na kisha kwenda kuwania urais wa visiwani Zanzibar.

Uchaguzi wa mwakani utatanguliwa na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24 ambao pia utatumika kama kipimo kuelekea uchaguzi huo mkuu.

 

George Njogopa/DW Dar es Salaam