1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi mpya za kidiplomasia zaendelea Misri

6 Agosti 2013

Juhudi mpya za kidiplomasia za kutafuta njia ya kumaliza mzozo nchini Misri, zinaendelea, ambapo wajumbe wa Umoja wa Ulaya na Marekani, wanaendelea na mazungumzo na pande zinazohasimiana.

https://p.dw.com/p/19KQd
Waziri wa kigeni wa Marekani, William Burns akiwa na makamu wa rais wa Misri, Mohamed El-Baradei
Waziri wa kigeni wa Marekani, William Burns akiwa na makamu wa rais wa Misri, Mohamed El-BaradeiPicha: picture-alliance/dpa

Mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayehusika na Mashariki ya Kati, Bernardino Leon na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, William Burns, wameongeza muda wao kuwepo mjini Cairo kwa lengo la kuendelea na juhudi za kumaliza mzozo wa Misri, uliochochewa na hatua ya kupinduliwa Mursi, mwezi uliopita.

Leon alikutana na Waziri Mkuu wa Misri, Hazem al-Beblawi wa serikali ya mpito inayoungwa mkono na jeshi jana Jumatatu, ikiwa ni siku moja baada ya kukutana gerezani na msaidizi wa kiongozi aliyeondolewa madarakani Mohamed Mursi wa chama cha Udugu wa Kiislamu, Khairat al-Shater.

Makamu raisi wa Udugu wa Kiislamu, Khairat al-Shater
Makamu rais wa Udugu wa Kiislamu, Khairat al-ShaterPicha: AFP/Getty Images

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Marie Harf, amesema kuwa Burns na Leon walimtembelea Al-Shater gerezani Jumapili iliyopita, wakiongozana na mawaziri wa mambo ya nje wa Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambao ni washirika wakubwa wa Marekani.

Ziara yenye lengo la kumaliza ghasia

Harf amesema kuwa ziara hiyo ilikuwa na lengo la kuzuia ghasia zaidi, kutuliza mvutano uliopo na kuwezesha mazungumzo kati ya Wamisri wenyewe, ambayo yanaweza kusaidia kuwepo na kipindi cha mpito kitakachowezesha kuchaguliwa kwa serikali ya kiraia kwa kuzingatia demokrasia. Imeelezwa kuwa Burns hata hivyo, hana mpango wa kukutana na Mursi.

Kwa mujibu wa msemaji wa Udugu wa Kiislamu, Gehad al-Haddad, hata hivyo, Al-Shater hakutowa ushirikiano mzuri kwa wajumbe hao waliokwenda kumtembelea gerezani.

Amesema msaidizi huyo wa Mursi alikataa kuzungumzia hali ya Misri na wajumbe hao, akisema kuwa msimamo wa Udugu wa Kiislamu katika kuunga mkono uhalali wa Mursi, bado haujabadilika.

Catherine Ashton, akiwa na rais wa mpito wa Misri, Adli Mansour
Catherine Ashton, akiwa na rais wa mpito wa Misri, Adli MansourPicha: Reuters/Amr Abdallah Dalsh

Katika hatua ya kutafuta suluhu ya mzozo wa Misri, wabunge wa Marekani, John McCain na Lindsay Graham leo Jumanne (06.08.2013) wanatarajiwa kuanza awamu mpya ya juhudi za kidiplomasia mjini Cairo.

Juhudi za kidiplomasia za awali

Hivi karibuni, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, wanadiplomasia wa mataifa ya Kiarabu, ujumbe wa Afrika na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, walikwenda mjini Cairo katika jitihada za kuutatua mzozo wa Misri.

Mbunge wa Marekani, Senata John McCain
Mbunge wa Marekani, Senata John McCainPicha: imago/UPI Photo

Misri imejikuta katika mzozo wa kisiasa uliosababisha watu kuuawa, baada ya jeshi kumuondoa madarakani Mohamed Mursi, kiongozi wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia mnamo Julai 3, mwaka huu.

Wafuasi wa Mursi wameyachukulia mapinduzi hayo kama kukiuka demokrasia na wamesisitiza wanataka kiongozi huo arejeshwe madarakani.

Hata hivyo, viongozi wa serikali ya mpito wamesema hakuna kurudi nyuma, baada ya kuandaliwa mpango wa kufanyika kwa uchaguzi mpya mwaka ujao wa 2014.

Zaidi ya watu 250 wameuawa tangu Mursi alipoondolewa madarakani. Mursi amekuwa akishikiliwa mahabusu kwa tuhuma za kufanya makosa kadhaa wakati alipotoroka gerezani wakati wa vuguvugu la mwaka 2011, lililomuondoa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman