1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani Mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou11 Juni 2009

George Mitchell ataka mazungumzo yaanze na yamalizike haraka kati ya Israel na Palastina

https://p.dw.com/p/I7OX
Mjumbe maalum wa Marekani George Mitchell azungumza na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud AbbasPicha: picture alliance/dpa

Mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya kati,George Mitchell anaendelea na juhudi zake.Baada ya mazungumzo pamoja na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina huko Ramallah,George Mitchell alikwenda Cairo.Baadae anatazamiwa kuitembelea Libnan na hatimae Syria.

Akizungumza na kiongozi wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas jana mjini Ramallah, mjumbe huyo maalum wa rais Obama,George Mitchell ameshadidia msimamo wa Marekani wa kuundwa dola la Palastina na kusema nchi yake haitayapa kisogo madai ya wapalastina ya kuwa huru.

"Kama rais Obama alivyosema wiki iliyopita,Marekani haitoyapa kisogo madai ya haki ya wapalastina ya kujipatia hadhi,fursa na taifa lao wenyewe."

George Mitchell amesisitiza tunanukuu"rais wa Marekani na waziri wa mambo ya nchi za nje wamesema wazi kabisa"ufumbuzi pekee wa kudumu ni kutekelezwa hamu ya pande hizi mbili ya kuwa na mataifa mawili-la Israel na la Palastina."

"Marekani inataka mazungumzo yaanze haraka na yamalizike haraka" amesema mjumbe huyo maalum wa rais Obama baada ya mazungumzo pamoja na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas,mnamo siku ya pili ya mazungumzo yake pamoja na viongozi wa Israel.

Mjumbe huyo maalum wa rais Barack Obama katika Mashariki ya kati amezitaka pande zote mbili ziheshimu muongozo wa mpango mpya wa amani ulioandaliwa na pande nne, yaani Marekani,Umoja wa Mataifa,Umoja wa ulaya na Urusi.

Mauer zwischen Israel und Palästina
Ukuta uliojengwa na Israel kuitenganisha na PalastinaPicha: AP

Mjumbe wa Palastina katika mazungumzo ya amani Saeb Arakat amesema Mahmud Abbas amemhakikishia bwana George Mitchell nia yake ya kuendelea kuheshimu muongozo wa mpango mpya wa amani,ikiwa ni pamoja na "kuzuwia visa vinavyochochea matumizi ya nguvu , kutia njiani dola linaloheshimu sheria na kumaliza vurugu."

"Kila pendekezo lazma likubaliwe,hakuna tena kupoteza wakati,hakuna tena mbinu za kuvuta wakati,kila kitu ni bayana.Nnadhani wakati umewadia wa kupitisha maamuzi na sio kuendeleza majadiliano,sio kuwachezea watu na wala si kwa kubabaisha baisha."

Baada ya mazungumzo yake mjini Ramallah George Mitchell alielekea Cairo jana usiku ambako alizungumza pia na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Ahmed Abu Gheith na mkuu wa idara ya upelelezi ya Misri Omar Suleiman.Bwana Suleiman ni mpatanishi kati ya Israel na Hamas katika juhudi za kuweka chini silaha huko Gaza.

Kituo cha mwisho cha ziara ya mjumbe maalum wa Marekani George Mitchell ni Libnan na baadae Syria.

Kwa mujikbu wa vyombo vya habari,rais Barack Obama anatazamiwa kutangaza mpango timamu wa amani kati ya Israel na Palastina ,wiki zijazo.


Mwandishi:Oummilkheir Hamidou

Mhariri:M.Abdul-Rahman