1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani Sudan Kusini zasambaratika tena

Iddi Ssessanga
22 Juni 2018

Juhudi za hivi karibuni za kumaliza vita vya miaka mitano nchini Sudan Kusini zimeshindikana baada ya rais Salva Kiir kukataa kufanya kazi na hasimu wake Riek Machar kufuatia mkutano wao nchini Ethiopia wiki hii.

https://p.dw.com/p/304h8
Äthiopien Friedensgespräche in Addis Abbea | Salva Kiir & Riek Machar
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Ayene

"Hii ni kwa sababu tumemchoka," msemaji wa serikali na waziri wa mawasiliano Michael Makuei alisema siku ya Ijumaa. Mahasimu hao walikutana wiki hii katika taifa jirani la Ethiopia kwa mwaliko wa waziri mkuu Abiy Ahmed, wakishikana mikono na kukumbatiana walipofanya mazungumzo ya ana kwa ana.

Walishikana mikono tena wakati viongozi wakuu wa mataifa na serikali za kanda walipokutana kujadili vita vya wenye kwa wenyewe katika taifa hilo changa kabisaa duniani.

Lakini ilidhihirika wazi kwamba wakati serikali ya Sudan Kusini iko tayari kutoa nafasi ya makamu wa rais kwa mwanasiasa wa upinzani, haigekubali kurejea kwa Machar katika nafasi hiyo. Machar aliikimbia nchi hiyo baada ya kuzuka mapigano mapya katika mji mkuu Juba Julai 2016, na kuhitimisha jaribio la muda mfupi la kurejesha amani ambamo alikuwa amerejea katika nafasi yake kama naibu wa Kiir.

Msemaji wa upinzani, Lam Paul Gabriel, aliliambia shirika la habari la Associated Press "hakukuwa na kilichokubaliwa katika mazungumzo", lakini mkutano wa ana kwa ana na rais wa Sudan Kusini ulikuwa wa manufaa "kwa sababu tuliweza kuona vurugu machoni mwa Salva."

Südsudan Michael Makuei Lueth Informationsminister
Waziri wa habari na msemaji mkuu wa serikali ya Sudan Kusini Michael Makuei.Picha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Gabriel pia aliishutumu jumuiya ya kikanda kwa kuipendelea serikali ya Sudan Kusini na kutanguliza maslahi yake yenyewe mbele ya "amani ya kweli," na kuongeza: "Hii inavunja moyo kabisaa."  Kanda hiyo - ambayo ni jumuiya ya ushirikiano wa maendeleo baina ya serikali - IGAD - imeongoza duru kadhaa za mazungumzo ya amani yalioshindikana.

Kiir, Machar kukutana tena Sudan na Kenya

Maafisa wamesema viongozi hao hasimu watakutana tena nchini Sudan na Kenya. Waziri wa mawasiliano Michael Makuei amasema rais Kiir atahudhuria mkutano na Kiir nchini Sudan wiki ijayo.

"Huu ni uamuzi wa wakuu wa mataifa ya jumuiya ya IGAD na tutauheshimu," alisema katika mkutano na waandishi habari mjini Addis Ababa alipoulizwa iwapo Kiir atahudhuria mazungumzo hayo yanayodhaminiwa na serikali ya Sudan. Lakini alisisitiza kuwa Kiir hayuko tayari kufanya kazi na Machar.

"Rais Salva Kiir..hayuko tayari kwa namna yoyote ile kufanya kazi tena na Riek Machar," alisema Makuei, akimlaumu Machar kwa kusababisha vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano ambavyo vimegharimu maisha ya maelfu ya raia na kusababisha wengine wapatao milioni 4 kuyahama makaazi yao.

Vita hivyo vilivyozuka miaka miwili tu baada ya Sudan Kusini kujipatia uhuru wake kutoka Sudan, vimeendelea licha ya juhudi kadhaa za kufikia amani. Mgogoro wa wakimbizi uliosababishwa na vita hivyo unaelezwa kuwa mkubwa zaidi tangu mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.

Mamilioni wengine wanaoendelea kuwapo nchini humo wakabiliwa na hatari ya kukumbwa na njaa, wakati pande hasimu zinalaumiwa kwa kuzuwia au kutatiza kasi ya uwasilishwaji wa msaada unaohitajika vibaya.

Maafisa wananufaika na mgogoro

Juhudi za karibuni zaidi za mapatano ya kusitisha mapigano mwezi Desemba zilikiukwa katika muda wa masaa tu baada ya kufikiwa. Pande zote zimetuhumiwa kwa ukiukaji ulioenea wa hakiza binadamu kama vile ubakaji wa kimakundi dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na kwa misingi ya kikabila.

maafisa kadhaa wa serikali ya Sudan Kusini wametuhumiwa pia na mashirika ya haki za binadamu kwa kujinufaisha kutokana na mgogoro huo na kuzuwia njia ya kupatikana amani, na Marekani -- ambayo ndiyo mfadhili mkubwa zaidi ya msaada wa kiutu -- imetishia kuondoa msaada wake.

Südsudan UN denken über Verstärkung von Unmiss nach
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vimesababishavifo vya maelfu na kuwalaazimu karibu milioni nne kuyahama makaazi yao.Picha: Reuters/A. Ohanesian

Mapema mwezi huu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha azimio lililoandaliwa na Marekani likitishia kuiwekea Sudan Kusini zuwio la kuuziwa silaha na vikwazo dhidi ya watu sita, akiwemo waziri wa ulinzi wa taifa hilo, ikiwa mapigano hayatasitishwa na makubaliano ya kisiasa kufikiwa. Azimio hilo linamtaka katibu mkuu Antonio Guterres kuripoti kwa baraza hilo kuhusu suala hilo ifikapo Juni 30.

Jumuiya ya IGAD imetishia kuwasilisha hatua za adhabu dhidi ya wakiukaji wa makubaliano ya karibuni ya mpango wa kusitisha mapigano, inagwa vikwazo vitahitaji kuidhinishwa na viongozi wa mataifa na serikali. Katika taarifa kuhusu mkutano wa wiki hii serikali ya Sudan Kusini ilipinga vikwazo, ikisema vilikuwa vinaupa kiburi upinzani.

Machar wakati huo huo, amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani nchini Afrika Kusini. Haikubainika wazi wapi angekwenda sasa. Kulingana na taarifa ya serikali ya Sudan Kusini, jumuiya hiyo ya kikanda inataka Machar ahamishiwe nje ya kanda na siyo katika taifa lolote lililokatibu na Sudan Kusini."

Makuei, msemaji wa serikali, alisema Machar anakaribishwa kutembelea Sudan Kusini na kusubiri uchaguzi, lakini "hatutaki kuwa na mapigano mengine."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,dpae.

Mhariri: Mohammed Khelef