1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani ya Mashariki ya kati zashika kasi

Oumilkher Hamidou16 Septemba 2009

Mjumbe maalum wa rais Obama George Mitchell apanga kuzungumza tena ijumaa na waziri mkuu wa Israel na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina

https://p.dw.com/p/JiFU
Waziri mkuu wa Israel na mjumbe maalum wa rais Obama,George MitchellPicha: AP

Waziri mkuu wa Israel na mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya kati, George Mitchell, wamemaliza mazungumzo yao bila ya kufikia makubaliano.Watakutana tena, lakini ijumaa ijayo.

Msemaji wa waziri mkuu wa Israel, Mark Regev, amesema mazungumzo kati ya Benjamin Netanyahu na George Mitchell "yamepita vizuri na wameamua kukutana tena ijumaa ijayo."

Mjumbe huyo maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya kati, aliyeanza ziara yake hii mpya jumapili iliyopita, alikwishazungumza na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa muda wa saa tatu jana, kabla ya kwenda Ramallah kwa mazungumzo pamoja na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina, Mahmoud Abbas. Na huko pia Bwana George Mitchell anapanga kurejea tena ijumaa asubuhi.

Mwishoni mwa mazungumzo hayo, George Mitchell alizisihi pande zote mbili zionyeshe "moyo wa kuwajibika" ili kurahisisha juhudi za kuyafufua mazungumzo ya amani yaliyokwama tangu mwishoni mwa mwaka 2008.

Kwa upande mmoja, mjumbe huyo maalum wa Marekani anajaribu kuishawishi Israel isitishe ujenzi wa makaazi mepya ya wahamiaji wa kiyahudi. Na kwa upande wa pili anajaribu kumtanabahisha Mahmoud Abbas akubali kukutana na waziri mkuu wa Israel pembezoni mwa mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa wiki ijayo mjini New-York, mkutano utakaosimamiwa na rais Barack Obama wa Marekani.

Benjamin Netanyahu na serikali yake hawataki kuitika shinikizo la kimataifa la kusitisha moja kwa moja ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika ukingo wa magharibi na katika eneo la mashariki la Jerusalem.

Waziri wa maendeleo ya kimkoa katika serikali ya Benjamin Netanyahu, Silvan Shalom anasema:

"Ikiwa watu wataunga mkono tangu mwanzo kusitishwa ujenzi wa makaazi ya wayahudi na kuunga mkono tangu mwanzo liundwe dola la Palastina, hapo yatabakia msuala kuhusu wakimbizi na hatima ya Jerusalem tuu. Hakuna serikali yoyote ya Israel itakayoweza kutekeleza masharti ya Wapalastina.Ndio maana ninasema mie, kwa heshma zote, hiyo ni fidia kubwa mno ya kulipa, ili kuweza kukutana na Mahmoud Abbas."

Mahmoud Abbas George Mitchell
Mjumbe maalum wa Marekani akizungumza na Mahmoud AbbasPicha: AP

Kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina, Mahmoud Abbas, anashurutisha kusitishwa ujenzi wa makaazi mepya ya Wayahudi katika maeneo ya Wapalastina, kama ilivyotajwa katika mpango mpya wa amani wa mwaka 2003, na kukutana na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Waziri mkuu Netanyahu amenukuliwa na gazeti la Maariv akimtolea mwito kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina "aonyeshe moyo wa kijasiri." Benjamin Netanyahu amesema tunanukuu: "Anabidi aueleze umma wake kwamba makubaliano yakitiwa saini, ugomvi utakua umekwisha na hakutokua tena na madai ziada. Si jambo linaloingia akilini kwamba tunakubali taifa la Palastina na wanaendelea baadae kushinikiza," amesema waziri mkuu huyo katika mahojiano yatakayochapishwa ijumaa ijayo kuadhimisha mwaka mpya wa kiyahudi.

Mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Mashariki ya kati, George Mitchell, anapanga kuelekea Libnan hii leo kwa mazungumzo pamoja na rais Michel Suleiman.

Mwandishi: Ummil Kheir Hamidou/AFP

Mhariri: Miraji Othman