1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kudhibiti Ebola zafanyika

Mjahida6 Agosti 2014

Sierra Leone imewapeleka wanajeshi wake kulinda eneo ambapo waathirika wa Ugonjwa hatari wa ebola wamewekwa, huku kesi ya kwanza ya maambukizi ya ugonjwa huo Saudi Arabia, ikizua wasiwasi wa mripuko wa ebola duniani.

https://p.dw.com/p/1CpW5
Wataalamu wa Afya wakiunyunyizia dawa mwili wa muathirika
Wataalamu wa Afya wakiunyunyizia dawa mwili wa muathirikaPicha: Reuters

Taarifa kutoka ikulu ya rais Sierra Leone imesema, wanajeshi hao watawazuia marafiki na familia ya waathiriwa kuwachukua wagonjwa nyumbani kwa lazima bila idhini ya wataalamu wa afya. Ebola inayoleta homa kali na kutokwa na damu mfululizo hadi sasa imeshasababisha vifo vya watu 900 katika Mataifa manne ya Afrika Magharibi tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2014.

Haijawa wazi ni katika maeneo gani watakapopelekwa wanajeshi hao lakini Kliniki ya Kailahun na Kenema, Mashariki mwa nchi hiyo ndizo zilizo na idadi kubwa ya walioathirika na ugonjwa hatari wa Ebola. Sierra Leone imeshuhudia kesi 646 za ugonjwa huo ikiwa ni dadi ya juu ukilinganisha na mataifa mengine yaliokumbwa na mripuko huo.

Hata hivyo vita dhidi ya ugonjwa huo vinakabiliwa na changamoto kubwa hii ni baada ya jamii ya waathiriwa kuwaondoa wagonjwa wao hospitalini na kuwapeleka vijijini ambapo watu wengi zaidi wanawekwa katika hatari ya kuambukizwa.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Margaret Chan
Mkurugenzi mkuu wa WHO Margaret ChanPicha: picture-alliance/dpa

Hii leo shirika la afya ulimwenguni WHO limeandaa mkutano wa dharura wa siku mbili kujadili janga la ugonjwa wa ebola katika mataifa ya Magharibi.

Kamati ya shirika hilo inakutana kuamua iwapo mripuko wa ugonjwa huo unaweza kuchukuliwa kama janga la kiafya katika kiwango cha kimataifa.

Awali katika mkutano wake na viongozi wa Mataifa manne ya Afrika Magharibi yanayopambana na kasi ya ugonjwa huo, Liberia, Sierra Leone, Guinea na Nigeria, shirika la WHO lilitangaza mpango wa dola milioni 100 wa kukabiliana na Ebola.

Ebola yaonekana kusambaa katika mataifa mengine

Huku hayo yakiarifiwa shirika la ndege la Uingereza limetangaza kufuta safari zake zote katika Mataifa ya Magharibi. Katika taarifa yake shirika hilo limesema limefanya hivyo kutokana na wasiwasi kuhusu hali ya kiafya katika mataifa hayo na kwamba inawajali wafanyakazi wake na wateja wake kwa ujumla.

Kwa upande mwengine wizara ya afya ya Saudi Arabia imesema inafanya uchunguzi kwa raia wake anayeonesha dalili za kuambukizwa Ebola kufuatia ziara yake ya hivi karibuni nchini Sierra leone. Raia huyo wa kiume aliye na umri wa miaka 40 alionesha dalili katika hospitali ya Jiddah na kwa sasa anasemekna kuwa katika hali mahututi.

Wataalamu wanafunzwa namna ya kujikinga wanapowashughulikia wagonjwa wa Ebola
Wataalamu wanafunzwa namna ya kujikinga wanapowashughulikia wagonjwa wa EbolaPicha: picture-alliance/AP

Saudi Arabia ilisema mwaka huu haitotoa visa kwa mahujaji wa Sierra Leone, Liberia na Guinea, kwa sabababu ya wasiwasi wa kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola.

Uhispania nayo imetuma ndege yake ya kijeshi kumchukua raia wake aliyeambukizwa Ebola nchini Liberia ili arejee nyumbani kwa matibabu, hii ni kulingana na wizara ya ulinzi nchini humo.

Nchini Marekani raia wa kike aliyeambukizwa Ebola nchini Liberia amewasili mjini Georgia hii leo kwa matibabu zaidi. Mwanamke huyo aliye na miaka 59 alipelekwa moja kwa moja katika hospitali ambako mwenzake wa kiume pia aliyeambukizwa ugonjwa huo anakopokea matibabu. Wote waliambukizwa walipokuwa wanajaribu kuwatibu wale walioambukizwa ebola nchini Liberia.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP,AP,DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga