1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kukusanya misaada kwaajili ya Syria

17 Mei 2013

Vita vinaendelea Syria na mashirika ya misaada yanapata shida kuendeleza shughuli zao hasa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali .Kuna ukosefu wa chakula ,maji na madawa.

https://p.dw.com/p/18Zma
Mwenyekiti wa shirika la misaada la Welthungerhilfe Bärbel DieckmannPicha: dapd

Katika eneo kati ya Uturuki na Syria,vifurushi vya misaada vinajazwa ndani ya malori ya Syria kutoka malori ya kituruki na kupelekewa watu katika miji ya Aleppo na Idlip.Unga wa ngano, na mahitaji mengineyo kwaajili ya familia ambazo hazimudu kukidhi mahitaji yao.Birgit Zeitler wa shirika la kimataifa la msaada wa chakula anasema familia nyingi zimeishiwa na akiba walizokuwa nazo,wameuza kila walichokuwa nacho kwaajili ya kununua chakula.Kwa miezi sasa mapigano yanaendelea Aleppo kati ya waasi na vikosi vya serikali. Bibi Birgit Zeitler anasema:

"Wamepoteza kazi zao kutokana na vita,shughuli za viwandani zimesita,maduka yamefungwa,hakuna umeme,hakuna maji,takataka zimezidi kurundikana,yote hayo bila ya shaka ni balaa katika mji wenye wakaazi wanaokurubia milioni nne.Na hasa wakati huu ambao msimu wa joto unaopindukia nyuzi joto 40 unakurubia,hali itazidi kuwa mbaya kila kukicha."

Kuna hatari ya kuzuka maradhi ya kuambukiza-anasema Dr. Sadiq Al Moussalie.

Kwa ushirikiano pamoja na shirika la misaada la jamhuri ya Tcheki la PIN-shirika la kimataifa la Msaada wa chakula ulimwenguni linazipatia familia 3000 katika maeneo ya kaskazini magharibi ya Syria- Aleppo na Idlip,misaada ya chakula kila siku zikiwemo tani zisizopungua nne za unga wa ngano wanaotumia kufanya mikate na kugawana na wengine.

Kwa mujibu wa shirika la Misaada la Ujerumani-Aktion Deutschland Hilft,zaidi ya wasyria milioni saba wametawanyika ndani nchini humo kutokana na mapigano yanayoendelea nchini mwao.

Wengi wao lakini misaada hiyo haiwafikii kabisa kutokana na ukosefu wa usalama na hasa katika maeneo ya Syria yanayopakana na Uturuki.

Wito wa kufunguliwa njia za kupitishia misaada ya kiutu

Bildergalerie Vertrieben durch Krieg (syrische Armenier kehren nach Armenien zurück)
Wakimbizi wa Syria wenye asili ya menia wamejazana katika kituo cha shirika moja la misaadaPicha: DW/A. Gazazyan

Sawa na mashirika mengine ya misaada na hili pia la Msaada wa chakula ulimwenguni linasambaza misaada katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi-kwa maneno mengine kaskazini mwa Syria.

Serikali haiyaruhusu mashirika ya misaada kuingia katika maeneo yaliyosalia.Ndio maana bibi Birgit Zeitler anatoa wito ifunguliwe njia haraka kuweza kuwafikishia watu misaada ya chakula na madawa.

Birgit Zeitler anahimiza pia michango itolewe.Hadi wakati huu Euro 12 elfu tu zimekusanywa kwaajili ya kugharimia misaada nchini Syria.

Mwandishi: Conrad Naomi/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Yusuf Saumu