1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaalikwa safari hii mazungumzoni

28 Oktoba 2015

Iran huenda ikajiunga na mazungumzo kuhusu mustakbal wa Syria kwa mara ya kwanza baadae wiki hii kama watasaidia kumaliza vita vya miaka minne vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1GvJe
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi,Sergey LavrovPicha: Reuters/C. Allegri

Washington ilikuwa inasubiri kusikia kama Teheran itashiriki katika duru ijayo ya mazungumzo yanayotarajiwa kuanza kesho alkhamisi na kuendelea hadi ijumaa mjini Vienna.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry,mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov na wanasiasa kadhaa wa ulaya na ulimwengu wa kiarabu watahudhuria mazungumzo hayo ambayo hadi wakati huu hayajawahi hata mara moja kuwahusisha wawakilishi wa Iran.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amepangiwa kuondoka leo hii kuelekea Vienna mji mkuu wa Austria.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani John Kirby amewaambia maripota kwamba maandalizi kuhusu mkutano wa Vienna yanakamilishwa na kuongeza na hapa tunanukuu:"lakini tunataraji Iran itaalikwa kuhudhuria mkutano huu unaokuja."Mwisho wa kumnukuu afisa huyo wa serikali ya Marekani.Maafisa wa serikali ya Marekani wameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba Urusi ina irai Iran;Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi,Lavrov amezungumza mara kadhaa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammad Javad Zarif mnamo siku za hivi karibuni.

Katika wakati ambapo Marekani haikubaliani na "harakati za uharibifu "za Iran nchini Syria,John Kirby amesema maafisa wa Marekani daima wamekuwa wakitambua,kwa njia moja au nyengine,wakitaka kusonga mbele kuelekea kipindi cha mpito wa kisiasa,wanabidi kuwa na mazungumzo na kujadiliana na Iran."

"Ni jukumu la Iran kuamua kama watashiriki au la watakapoulizwa" amesema.

Mazungumzo ya kichini chini pamoja na Saud Arabia

Marekani inajibwaga katika mchezo wa bahati nasibu.Iran imekuwa ikiiunga mkono serikali ya rais Bashar al Assad mnamo wakati wote huu wa mzozo wa Syria,wanajeshi wa Iran wanapigana upande wa jeshi la Syria na Iran inaangaliwa na waasi wanaoungwa mkono na nchi za magharibi na washirika wao Marekani kuwa chanzo kikubwa cha umwagaji damu.Upande wa upinzani nchini Syria unaweza kupinga kujumuishwa Iran katika mazungumzo yoyote yatakayohusu mustakbal wa Syria baada ya enzi za Bashar al Assad.

Ayatollah Seyed Ali Khamenei
Kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Seyed Ali KhameneiPicha: Leader.ir

Kwa upande mwengine,juhudi zote za awali za kimataifa hazijasaidia kukomesha mapigano na John Kerry anajaribu kuziunganisha pande zote zenye ushawishi katika nchi hiyo ya kiarabu kwa msingi wa kuundwa Syria itakayokuwa na amani,ya mchanganyiko wa pande zote husika, isiyoelemea upande wowote wa kidini na itakayopata ridhaa ya wananchi wake.

Washington ilikuwa ikipinga moja kwa moja hapo awali kujumuishwa Iran katika duru mbili za mazungumzo ya muda mrefu yaliyopita,lakini tangu hivi karibuni imekuwa ikizungumzia uwezekano wa Iran kujiunga na mazungumzo yatakayofuata.Na sasa Washington inaikaribisha Teheran baada ya madajiliano ya siku kadhaa ya kichini chini,na hasa pamoja na hasimu wa Iran katika eneo hilo-Saud Arabia-hayo lakini ni kwa mujibu wa afisa mmoja wa Marekani ambae hakutaka jina lake litajwe.

Katika mazungumzo ya simu jana,rais Barack Obama na mfalme Salman wa Saud Arabia wamezungumzia kuhusu ushirikiano wa dhati katika mapambano dhidi ya wafuasi wa dola la kiislam na kusaka njia za kupatikana kipindi cha mpito cha kisiasa nchini Syria."Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya Marekani.Viongozi hao wawili wameahidi kuimarisha juhudi za kidiplomasia.Taarifa hiyo haikutaja lakini chochote kuhusu Iran.

Mvutano kati ya madola makuu kuhusu mustakbal wa Assad

Hakuna uhakika kama Iran itashiriki.Kiongozi wa kidini Ayatollah Ali Khamenei ameondowa uwezekano wa kuzungumza tena na Marekani baada ya kufikiwa makubaliano kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran mwezi Julai mwaka huu.

Syrien Treffen Bashar al-Assad mit Youssef bin Alawi
Rais wa Syria Bashar al Assad akizungumza october 26 iliyopita na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Oman Youssef bin AlawiPicha: picture-alliance/dpa/Syrian Arab News Agnecy

Marekani,Urusi,Saud Arabia na Uturuki walikutana wiki iliyopita mjini Vienna wakileta fikra mpya kuhusu namna ya kufufua matumaini mema ya kisiasa nchini Syria-hata hivyo wamesalia na misimamo tofauti linapohusika suala la mustakbal wa Assad.Marekani na washirika wake wanasema Assad anaweza kushiriki katika kipindi cha mpito,lakini atabidi ang'atuke madarakani kipindi hicho kitakapokamilika.Urusi na Iran zinapinga fikra hiyo.Mada nyengine ya mabishano inahusu muda wenyewe wa kipindi cha mpito na katiba mpya na chaguzi za siku za mbele ziwe za aina gani.

Mbali na Iran,mazungumzo ya wiki hii kuhusu Syria yanatarajiwa kuhudhuriwa pia na wawakilishi wa Uengereza, Ufaransa,Ujerumani,Jordan na falme za nchi za kiarabu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP
Mhariri:Yusuf Saumu