1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jukwaa la maji ulimwenguni

17 Machi 2009

Jukwaa la kuzungumzia shida za maji safi na ya kutosha limefunguliwa Istanbul,Uturuki.

https://p.dw.com/p/HEHo

Mkutano wa siku 7 wa ulimwengu juu ya maji-World Water Forum- ulifunguliwa rasmi jana mjini Istanbul, Uturuki. Jukwaa hilo linalenga kukabiliana na msukosuko unaozidi wa kuania chemchem za maji safi. Hili ni jukwaa linalofanyika kila miaka 3 likizungumzia ukosefu wa maji, hatari za kwenda vitani kunyanganyia chemchem za maji, huku nchi mbali mbali zikitaka kudhibiti mito na maziwa pamoja na jinsi ya kuwapatia mamilioni ya wanadamu katika sayari hii maji safi na zana za usafi majumbani mwao.

Kiasi cha wajumbe 20,000 kutoka nchi 130 wamewasili mjini Istanbul,Uturuki tangu jana kwa jukwaa hilo.Hili ni jukuwaa linalowaleta pamoja watu tangu wale wanaohusika moja kwa moja na sekta ya maji na wale wa nje yake ili kusaka ufumbuzi wa changamoto zinazosababisha ukosefu wa maji safi na ya kutosha kukidhgi mahitaji ya wanadamu.

"Kikao hiki kinatoa kwa idara za maji na wanaopitisha maamuzi juu ya matumizi ya maji kote ulimwenguni fursa maalumu kukusanyika pamoja, kuwasiliana,kujadiliana na kujaribu kusaka suluhisho la kujipatia bila shida maji-safi." hii ni kwa muujibu wa Baraza la maji linaloandaa jukwaa hili.

Banki Kuu ya Dunia imearifu huko Istanbul kuwa msukosuko wa sasa wa uchumi ulimwenguni unaweza ukapunguza fedha za kugharimia ujenzi wa miundo-mbinu,sekta muhimu katika kujipatia maji safi na sekta ambayo mabingwa tayari wanadai fedha ziliopo hazitoshi.

Bw.Jamal Saghir,afisa wa banki kuu ya dunia, amesema pia raslimali katika kujipatia maji safi na ya usalama katika fedha za serikali mbali mbali za kuustawisha uchumi ili kujikomboa katika balaa la hivi sasa haziotoshi.

Maji safi yanakosekana hivi sasa katika nchi nyingi zinazoendelea na zana za usafi zisizoridhisha ni chanzo kikubwa cha maradhi yanayo sababisha vifo.

Bw.Saghir aliuambia mkutano wa Istanbul juu ya maji hii leo kuwa msukosuko wa fedha duniani wakati huu unaweza kudhuru uimara wa chemchem za maji. Akatoa mwito kuchukuliwe juhudi kubwa za kuongoza barabara mipango ya maji licha ya hali ya sasa ya ukosefu wa fedha.

Isitoshe, iwapo ni kutokana na ukame, mafuriko, kuyayuka kwa theluji au kupanda kwa vipimo vya maji baharini, maji ni mhanga wa kwanza wa mabadiliko ya hali ya hewa -amesema Dr.Mark Smith anaeongoza mradi wa maji katika shirika kubwa la kimazingira ulimwenguni-International Union for Conservation of nature.

Bw.Mark anaongeza kusema kuwa, athari kubwa zinazotokana na badiliko la hali ya hewa na linalozungumzwa na wanadamu wakati huu, ni ukame, mafuriko,vimbunga na dharuba,kuyayuka barafu na kupanda kwa vipimo vya maji fukweni mwa bahari. Katika juhudi na vita vya jinsi tunavyokabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, anashauri mtaalamu huyu ,maji lazima yawe mada ya usoni kabisa.

Muandishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Othman.Miraji