1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jukwaa la Vyombo vya Habari mjini Bonn

Othman, Miraji9 Juni 2008

uUtumiaji mabavu na ukandamizaji katika maeneo ya mizozo duniani, hayo ni mambo yasioshughulikiwa, lakini sio na vyombo vya habari vilivyo huru.

https://p.dw.com/p/EG6P
Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Bwana Erik BettermannPicha: picture-alliance/ dpa

Utumiaji nguvu na ubakaji huko Sudan, vita vya kienyeji katika Zimbabwe, kuendewa kinyume haki za binadamu huko Mnyanmar na Tibet- kwa ujumla, utumiaji mabavu na ukandamizaji katika maeneo ya mizozo duniani, hayo ni mambo yasioshughulikiwa, lakini sio na vyombo vya habari vilivyo huru. Waandishi wa habari wanaoipenda kazi yao na walio majasiri wanayafichua hadharani maovu hayo. Lakini kitu gani hasa ambacho vyombo vya habari vinaweza kufanya? Hatari gani wanakabiliana nazo wanapojaribu kuchochea kuweko amani na kuzuwia kutokea mizozo? Hiyo ndio ilikuwa mada ya mkutano wa kimataifa uliofanyika mjini Bonn, hapa Ujerumani, baina ya Juni 2 na 4, Deutsche Welle ikiwa mwenyeji. Kwanini Deutsche Welle ikauundaa mkusanyiko huu wa watu 800, wengi wao wakiwa waandishi wa habari na pia wawakilishi wa siasa, biashara na utamaduni. Mkurugenzi mkuu wa Deutsche Welle, Erik Bettermann, alikuwa na haya ya kusema katika hotuba ya kuufungua mkutano huo:


+Hasa vyombo vya habari, kutokana na mitihani inayotokana na utandawazi, vinaweza na lazima vituo mchango mkubwa; lakini mchango huo na matakwa yanayofungamana na mchango huo bado hayajafafanuliwa vya kutosha. Masuala hayo yanahusiana na kuzuwia kuchipuka mizozo na kuchochea kuweko amani, uongozi wa serekali na kuheshimiwa haki za binadamu, jumuiya za kiraia na kujenga maadili fulani, elimu na maendeleo. Hapo vyombo vya habari vinaweza na ni lazima vijenge mwamko miongoni mwa watawala na wanaotawaliwa.+


Kwa hakika fikra na mikakati mingi ya kujenga vyombo vya habari vilivyo huru ilianzia wakati wa Vita Baridi. Lakini baada ya kusambaratika ukoministi hali ilikuwa nyingine ukilinganisha na hali ya sasa ambayo nchi zinazotaka kuleta marekebisho zinajikuta nayo.


Mabadiliko yaliotokea katika nchi zilizokuwa za kambi ya Mashariki hayajasababishwa na vita, na wengi wa watu wa nchi hizo walikuwa wanajuwa kusoma. Mambo ni tafauti tangu kutokea yale mashambulio ya New York, Madrid na London na kuchomoza kile kinachoitwa ugaidi wa habari.


Katika mkutano wa Bonn wa wiki iliopita alikuja pia Bibi Schirin Ebadi, mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel, na alikuwa na haya ya kuuambia mkutano:


+Pale utumiaji mabavu unapofichuliwa, mawazo ya ubinadamu yanaamka. Hapo tena mtu anatafuta suluhisho kupambana na hali hiyo. kazi ya unadishi wa habari ni ya hatari, lakini ni kazi tukufu.+


Mkutano wa Bonn wa wiki iliopita uligusia pia mada namna Ulaya inaweza na inavolazimika kufanya ili kuzuwia kutokea mizozo, tukitambua Umoja wa Ulaya umechangia kuhakikisha kufanyika uchaguzi kwa njia ya amani huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo; polisi wa nchi za Ulaya wanalinda mipaka baina ya Misri na Ukanda wa Gaza; huko Bosnia wanajeshi wa Umoja wa Ulaya walisimamia kutekelezwa mapatano ya Dayton; nchini Afghanistan nchi za Ulaya zinasaidia kuundwa jeshi la polisi na katika Georgia unasaidia kuundwa taasisi za sheria. Kwa hakika Umoja wa Ulaya unatakiwa msaada wake duniani kote.


Pia yalijadikiwa masuala ya maendeleo ya kiuchumi na utulivu wa kisiasa, vipi ukweli unaovoweza kunusurika kwani barani Afrika uandishi wa habari unajikuta katikati baina ya medani mbili za mzozo, kila upande unawaona waandishi wa habari kuwa ni mahasimu wao, na pia vipi kuwapatia mafunzo waandishi wa habari walioko katika maeneo ya mizozo. Waandishi wa habari katika maeneo ya mizozo ya Afrika wanalipa gharama kubwa, mara nyingine hata ya maisha yao. Hivyo ndivyo alivoniambia Jenerali Ulimwengu wa kutoka Tanzania aliyehudhuria mkutano wa Bonn:

Mauaji ya kiholela- jana yalikuwa Rwanda na leo tunajionea huko Darfur, Sudan, makundi ya waasi na wababe wa kivita wanapigana dhidi ya serekali na raia. Kabla ilikuwa Sierra Leone na leo Kongo. Wanaharakati wa kupigania haki za binadamu wako katika mbinyo, kwa mfano huko Chad na Angola.


Kwa mfano, vipi vyombo vya habari vilivojikuta katika ghasia za karibuni huko Kenya, Charles Otieno wa gazeti la Standard la nchi hiyo aliniambia hivi:


Pia redio za matangazo ya lugha za kikabila zilizochipuka katika maeneo mengi zinaweza kutumiwa kuendeleza siasa ya chuki katika nchi yenye makabila mbali mbali. Tena Charles Otieno wa kutoka Kenya aliniambia hivi:


Katika nchi ambako watu wengi hawawezi kusoma na kuandika, ambako umeme na Internet hazifanyi kazi kwa kutegemea, redio ndio chimbuko nambari moja kwa watu kujipatia habari na vile vinavosimamiwa na serekali vinafanya kazi kwa kuendesha tu maslahi ya kisiasa ya watawala. Kumbuka habari zinazoaminika na zilizofaniwa utafiti mzuri zinaweza kuokoa maisha, na hasa katika nchi ambako mafunzo ya uandishi wa habari ni ya chini.


Mmoja watu waliohudhuria mkusanyiko wa Bonn, japokuwa sio mwandishi wa habari, lakini ni mtu mwenye ushawishi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Alikuwa mwenyekitiwa Tume Huru ya Uchaguzi, na hivi sasa anasimamia mapatano ya amani katika eneo la Mashariki la nchi yake. Ni Padre Appolinaire Malumalu. Eneo hilo limekumbwa na vita na mizozo kwa miaka sasa. Aliniambia hivi kuhusu Deutsche Welle inayosikika sana katika nchi anakotokea:

Bado thuluthi mbili ya wanadamu duniani wanaishi katika nchi ambako uhuru wa vyombo vya habari bado ni neno la kigeni. Deutsche Welle, baada ya kumalizika utawala wa Wataliban katika Afghanistan, unasaidia kujenga nchini humo vyombo huru vya habari, na kuendeleza ushirikiano bila ya kujali mipaka ya nchi ndio imekuwa shughuli kubwa ya Deutsche Welle.