1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jules Alingete akosolewa kwa kusema hakuna vita DRC

Amina Mjahid
27 Aprili 2022

Mashirika ya kiraia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanapinga matamshi ya mkaguzi mkuu wa fedha (IGF) aliyesema hakuna vita nchini Kongo. Aliyasema hayo mjini Houston, Marekani kwenye kongamano la wawekezaji.

https://p.dw.com/p/4AV4f
Demokratische Republik Konog | Unruhen in Goma
Picha: Guerchom NdeboAFP/Getty Images

 

Matamshi ya mkaguzi mkuu wa fedha, Jules Alingete aliyoyatoa wakati akijaribu kuwashawishi wawekezaji kwenda kuwekeza nchni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, yamepokelewa vibaya sana hapa nyumbani, na haswa katika maeneo ambayo vita vinaendelea.

Huko Ituri ambako wanamgambo wa ndani ya nchi wa Codeco, na wale wa kigeni wa ADF wanaendelea kuwashambulia wakazi, mashirika ya kiraia yamechukulia matamshi hayo kuwa ni usaliti. "Watu wameuwawa mashariki, vitu vinaharibika siku kwa siku mashariki, manyumba na magari vimechomwa. Bwana Jules Alingete yeye kama Kiongozi anayeangalia mambo ya feza, kama hawezi kujua maana yake yeye ni mmoja wa maadui wa Kongo. Anastahili kuachishwa kazi na kupelekwa mahakamani," alisema Dieudonné Lossa Dekhana, mratibu wa mashirika ya kiraia mkoani Ituri.

Msimamo huo wa mashirika ya kiraia ya jimbo la Ituri ndio unaungwa mkono pia na shirika la kiraia Kivu kaskazini, ambako raia wanaendelea kuwa wahanga wa mashambulizi ya makundi yenye kumiliki silaha.

Huko Beni, ambako raia wamekuwa wahanga wa mauaji kwa miaka kadhaa, makundi ya waliokasirishwa wanachukulia matamshi ya Alingete kuwa ukanushaji ambao unawakejeli maelfu ya Wakongomani wanaoendelea kuuwawa katika vita mashariki mwa Kongo.

Hayo yamejitokeza wakati Rais Félix Tshisekedi akijaribu kila  liwezekanalo ili kutatua mambo kwa njia ya mazungumzo, katikamaeneo yanayoendelea kukumbwa na mizozo huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kama vile mazungumzo yanayofanyika huko Nairobi nchini Kenya.

Mwandishi: Jean Noël Ba-Mweze, DW, Kinshasa.