1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kiislamu Dakar

13 Machi 2008

Viongozi wa Jumuiya ya mnchi za kiislamu wakutana nchini Senegal leo na kesho wakijaribu kuutakasa uislamu magharibi.

https://p.dw.com/p/DO0I
Rais Ahmadinejad (kulia)Picha: AP

Viongozi wa nchi 57 zanachama wa Jumuiya ya nchi za kiislamu wamejumuika leo mjini Dakar,Senegal kwa ufunguzi wa mkutano wao wa kilele wa siku mbili.Agenda mbele yao ni kusaka njia ya kuikuza heba ya uislamu katika nchi za magharibi na kustawisha maendeleo ya kiuchumi katika nchi masikini za Jumuiya .

Rais wa Senegal,mwenyekiti mpya wa OIC-Organisation of Islamic countries inayowakilisha waislamu zaidi ya bilioni 1 kuanzia Mashariki ya kati,Afrika hadi Asia, alitangaza leo kwamba usoni kabisa jukumu la jumuiya hii ni kusuluhisha mgogoro kati ya wapalestina na Israel .

►◄

Mkutano huu wa kilele wa Jumuiya ya kiislamu yenye wanachama 57-jumuiya kubwa ya waislamu ulimwenguni ,inazikusanya pia pamoja nchi za kiarabu zinazoamua bei ya mafuta na zile za kiafrika zinazopigana kuwapatia wakaazi wake mahitaji ya lazima na kuboresha barabara na njia .

Mkutano huu unarejea Afrika kwa mara ya kwanza tangu kupita miaka 14.

Kiasi cha viongozi wa dola na serikali 40 wanahudhuria huko Dakar pamoja nao rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran,rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria,rais Oumar al-Bashir wa Sudan na jirani yake Idris Deby wa Chad ambao walikua wakutane jana kutia saini mapatano ya kumaliza ugomvi wao.Halkadhalika amewasili mjini Dakar,Katibu mkuu wa UM Ban Ki-Moon na rais wa Mamlaka ya ndani ya wapalestina-Mahmoud Abbas.

Mwenyekiti mpya wa jumuiya hii ni rais Abdoulaye Wade wa Senegal.Jaribio lake alilofanya kuleta ufumbuzi kati ya rais Oumar al Bashir wa Sudan na rais Idriss Deby wa Chad lilikwama jana aliposhindwa rais wa Sudan kuhudhuria kikao katika Qasri la rais lake mjini Dakar.Alitoa udhuru badae akisema akiumwa na kichwa.

Kwa muujibu wa taarifa ya serikali ya Chad iliotoka leo ,Sudan ilifanya jana hujuma kadhaa za vikosi vyenye silaha dhidi ya Chad.Chad iliwaita wapiganaji hao waliohujumu ni "mamluki"-jina inalotumia kuwaita waasi wa Chad inaowatuhumu kusaidiwa na Sudan.

Mbali na kisa cha Sudan na Chad, jumuiya ya nchi za kiislamu imeingiwa na kiwewe na kuongezeka na bughdha dhidi ya uislamu na waislamu katika nchi za magharibi-jambo ambalo imeueleza ni kitisho kwa usalama wa kimataifa.

Kwa jicho hilo,Jumuiya ya nchi za kiislamu imezitaka nchi za Ulaya na Marekani kuchukua hatua kali kuzuwia bughdha kama hizo kwa waislamu -hii ilikuwamo katika ripoti ilioandaliwa kwa kikao hiki cha leo na kesho.

Viongozi wa kiislamu kitambo sasa wakionya kutia chungu kimoja ugaidi na uislamu na hasa baada ya shambulio la Septemba 11, 2001 pale magaidi wa Al Qaeda waliposhambulia Marekani.Kuutia chungu kimoja uislamu na ugaidi walionya viongozi hao kutapalilia hisia kali za uislamu."Kambi ya nchi za magharibi yafaa kufahamu kwamba vita dhidi ya ugaidi haviwezi kushinda bila ya msaada wa nchi za kiislamu."

Viongozi wa jumuiya ya kiislamu wameelezea upya hofu kutokana na visa kama vile vilivyozuka nchini Denmark vya kuchapishwa vikatuni vikimdhihaki mtume Muhammad pamoja na mpango wa mbunge wa Holland wa siasa za mrengo wa kulia Geert Wilder kuchapisha filamu inayokieleza kitabu kitakatifu cha kuran kuwa ni cha kifashisti.

Jumuiya ya kiislamu imearifu kwamba uislamu umekumbana mara kwa mara na dharuba kali tangu ilipoanza dini hii lakini miaka ya karibuni mambo yamefurtu ada na hivyo imezusha wasi wasi mkubwa miongoni mwa waislamu kote duniani.