1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya Kimataifa yaichangia Syria

Saleh Mwanamilongo
30 Machi 2021

Umoja wa Mataifa unafanya mkutano kwa ajili ya kuwasaidia raia wa Syria.Umoja wa Mataifa utaziomba nchi wafadhili kuchangia kiasi cha hadi dola bilioni 10. 

https://p.dw.com/p/3rN3y
Syrien Krieg Demonstration
Picha: Muhammed Said/AA/picture alliance

Umoja wa Mataifa leo unafanya mkutano wa tano wa kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia raia wa Syria, wanaokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda wa miaka kumi nchini mwao, na sasa wakiwa wanakabiliwa na janga baya duniani la COVID-19. Katika mkutano wa leo ulioandaliwa na Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa utaziomba nchi wafadhili kuchangia kiasi cha hadi dola bilioni 10. 

Dola bilioni 4.2 zinawekewa malengo ya kuwasaidia raia walio ndani ya Syria na zingine bilioni 5.8 ni kwa ajili ya wakimbizi na nchi zinazowahifadhi katika Mashariki ya Kati. Mkuu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock, amesema miaka kumi iliyopita imekuwa ya kukata tamaa na maafa kwa Wasyria, akiongeza kwamba maisha yamekuwa magumu, uchumi kuporomoka na COVID-19 imesababisha njaa zaidi, utapiamlo na magonjwa.

'' Uwezo wetu wa kupeleka misaada na kuepusha hali mbaya zaidi kwa mamilioni ya raia utategemea maamuzi mazuri ya kisiasa na ukarimu wa kuchangia fedha kutoka kwa jumii ya kimataifa.'',alisema Lowcock.

Bado mashambulizi ya anga yaendelea

 Watu wapatao milioni 24 wanahitaji msaada wa kiutu, ikiwa ni sawa na milioni 4 wa ziada ukilinganisha na mwaka uliopita. Idadi hiyo ni ya juu kabisa toka kuzuka machafuko ya Syria yaliosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011.

Mkuu wa shirika la misaada ya Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock.
Mkuu wa shirika la misaada ya Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock.Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Lowcock amesema vita vimepungua lakini matumaini ya amani bado ni madogo. Mapigano baina ya jeshi la Syria na waasi yamepungua toka kutiwa saini makubaliano ya amani mwaka mmoja uliopita kufuatia mashambulizi ya anga ya Urusi yaliosababisha watu milioni moja kuyahama makaazi yao. Hata hivyo ndege za kivita za Urusi, Iran na Syria zinaendelea kuyashambulia maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anatarajiwa kuhutubia mkutano huo wa leo. Machi 10, siku ya maadhimisho ya miaka 10 ya vita vya Syria,Guterres alisema kwamba nchi hiyo inapitia madhila ambayo nusu ya watoto wa Syria hawaja ishi siku moja bila vita na ambako asilimia sitini ya watu wako kwenye hatari ya kukosa chakula.

Ujenzi wa Syria utahitaji ma bilioni ya dola zaidi

Mji wa Idblib baada ya kushambuliwa wiki iliopita na ndege za kivita za Urusi.
Mji wa Idblib baada ya kushambuliwa wiki iliopita na ndege za kivita za Urusi.Picha: Muhammed Said/AA/picture alliance

Kwenye taarifa ya pamoja mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu yalitoa mwito kwa wafadhili wa kimataifa kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Syria, hasa zaidi huduma za afya, maji na umeme.

Khalil Hboubati wa shirika la Hilali Nyekundu nchini Syria amesema kuwa miundo mbinu za nchi hiyo zimechakaa.

 Umoja wa Ulaya unaoandaa mkutano huo umesema ,ujenzi wa miji ya Syria utahitaji mabilioni ya dola zaidi .

Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, Peter Maurer alihimiza nchi zenye nguvu kufikia makubaliano ya amani badala ya kuendelea na mikutano ya kila mwaka ya wafadhili kuhusu Syria. Amesema wahudumu wa misaada ya kiutu wako kwa ajili ya kusaidia,lakini dhamana kuu ni kwa pande husika katika mzozo huo.