1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa yaijadili Yemen

27 Januari 2010

Viongozi wa mataifa makuu ulimwenguni wanakutana jijini London kuijadili Yemen, kabla ya mkutano wa kimataifa juu ya Afghanistan, utakaoanza Alhamisi.

https://p.dw.com/p/LhgU
Waziri wa Nje wa Yemen Abu Bakr al-Qirbi, kushoto na Waziri wa Nje wa Marekani Hillary Rodham ClintonPicha: AP

Kikao hicho kimeitishwa ili kuzijadili mbinu za kuisaida, kifedha, serikali ya Yemen ambayo inatatizwa na ugaidi na vita nchini humo. Jamii ya kimataifa ilitikiswa na jaribio la shambulio la kuiripua ndege iliyokuwa ikielekea Detroit, Michigan, Krismasi iliyopita. Shambulio hilo linaaminika kuwa liliwahusisha magaidi wa Al Qaeda tawi la Yemen.

Ripoti ya hivi karibuni ya maseneta wa Marekani imebaini kuwa Yemen inakabiliwa na hatari kubwa ya ugaidi ambao unawahusisha wapiganaji wa kundi la Al Qaeda. Kikao hicho cha London, kimsingi, kitajaribu kulitafutia ufumbuzi suala hilo viongozi hao watakapokutana leo baadaye.

Ajenda kuu ya mkutano huo ni suala la Afghanistan litakalojadiliwa hapo kesho Alhamisi. Mchana wa leo mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na mataifa mengine 20 watajadiliana kwa pamoja na wawakilishi wa uongozi wa Yemen kwa kipindi cha muda wa saa mbili.

Kama anavyoeleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen, Abu Bakr al-Qibri,mkutano huo kwa kweli una azma ya kutaka kuisaidia nchi yake.

´´Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita tumekuwa tukitoa wito wa kusaidiwa, mafunzo ya ziada na vifaa ili tuweze kupambana na ugaidi hapa Yemen. Kwa bahati mbaya hatujafanikiwa kuvipata hivyo. Kila wakati tumekuwa tukisisitiza kuwa vita dhidi ya ugaidi sharti viambatane na maendeleo nchini´´

Kiasi cha nusu ya raia wote milioni 23 wa Yemen wanaaminika kuwa masikini. Kwa mtazamo wa mataifa ya magharibi, rushwa na mivutano ya ndani serikalini vyote vimeyaathiri maendeleo ya aina yoyote ile.

Hali ni mbaya kwani pato la mafuta limepungua kwa kiasi kikubwa, kwa sababu utoaji wa mafuta umepungua. Kadhalika, ghasia katika maeneo ya kusini na kaskazini navyo pia vimechangia.

Mchambuzi na mhadhiri wa masuala ya mashariki ya kati katika chuo cha Uchumi cha London, LSE, Profesa Fawaz Gerges, anasisitiza kuwa serikali haina nguvu.

´´Maeneo mengi ya Yemen hayana udhibiti.Serikali ya Yemen imeshindwa kuyadhibiti maeneo yaliyo nje ya mji wa Sa'naa´´.


Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen, al-Qirbi, ana matumaini makubwa na amekumbusha kuwa katika kikao cha wafadhili cha mwaka 2006 nchi yake iliahidiwa kiasi cha zaidi ya dola bilioni 3 zilizopangwa kutumiwa katika miradi ya maendeleo.

Marekani nayo inataka kuiambatanisha misaada itakayoipa Yemen na juhudi za kuimarisha uongozi. Kwa upande wake, Yemen imeyakanusha madai yote kuwa inazikiuka haki za binadamu, kuwakandamiza wafuasi wa upinzani pamoja na rushwa iliyokithiri.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, alikiri kuwa sharti washirikiane pamoja katika vita hivyo dhidi ya ugaidi.


Gordon Brown Rede auf Jahreskonferenz in Brighton
Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon BrownPicha: AP

´´Ni dhahiri kuwa watayatafuta maeneo mengine ulimwenguni watakakoweza kuendeleza harakati zao. Tulisema kuwa kabla ya jaribio la shambulio la Disemba kutokea tulikuwa tayari tumeanza kuyatazama kwa karibu maeneo ya Somalia na Yemen, kwani harakati hizo ziliripotiwa kuwa zimeongezeka´´.


Kulingana na mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati, Fawaz Gerges, kuna haja ya kutoa msaada zaidi ya kuwapa mafunzo wanajeshi wa Yemen na kuwasalimisha ili kufanikiwa katika vita dhidi ya magaidi wa Al Qaeda. Hata hivyo, kikao cha London hakitoweza kuyapitisha maamuzi hayo.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya-ZPR-B, Wesel

Mhariri: Miraji Othman

Audio in DaletWeb:

Ende