1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa yawashinikiza viongozi wa Kenya

Josephat Charo30 Januari 2008

Umoja wa Ulaya walaani vikali mauaji ya mbunge wa upinzani

https://p.dw.com/p/CzYY
Rais Mwai KibakiPicha: AP Photo

Jumuiya ya kimataifa inamshinikiza rais Mwai Kibaki wa Kenya na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wagawane madaraka ili kuumaliza mzozo wa kisiasa uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi.

Jana Kofi Annan alianzisha rasmi mazungumzo ya kuutanzua mzozo wa kisiasa kati ya rais Mwai Kibaki na Raila Odinga mjini Nairobi. Rais Kibaki amesema mchakato wa mdahalo wa kitaifa umeanza ili kuishughulikia hali ya kisiasa nchini Kenya.

Akizungumza mjini Nairobi Kofi Annan amesema ana matumaini maswala ya kisiasa yanayohitaji kutatuliwa yatapatiwa ufumbuzi katika majuma manne yajayo na kuipa Kenya mwaka mmoja kukabiliana na uharibifu uliosababishwa na machafuko ambapo watu takriban 1,000 wameuwawa.

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umelaani vikali mauaji ya mbunge wa upinzani, Mugabe Were, aliyeuwawa mapema jana wakati alipokuwa akirejea nyumbani kwake mjini Nairobi.

Umoja huo pia umeitaka serikali na upinzani ushirikiane na Kofi Annan kuumaliza mgogoro wa kisiasa uliopo.

Viongozi watano wa Ulaya wametoa mwito machafuko yanayoendelea nchini Kenya yakomeshwe wakisema ipo haja ya viongozi wa nchi hiyo kuzungumza kwa masilahi ya taifa na eneo zima kwa jumla.

Katika taarifa yao ya pamoja viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na halmashauri ya Umoja wa Ulaya, wamewataka wanasiasa wa Kenya wachukue hatua za dharura kumaliza ghasia na kurejesha usalama kwa wakenya wote.

Taarifa hiyo iliyotolewa baada ya mkutano ulioandaliwa na waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown mjini London, ambao ulijadili matatizo ya kiuchumi duniani, pia imesema viongozi hao wanaziunga mkono juhudi za katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Graca Machel, mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Sambamba na hayo waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amesema machafuko yanayoendelea nchini Kenya yanatia wasiwasi.

Kwa mara nyingine kiongozi huyo amewataka viongozi wa Kenya watafute suluhisho la kisiasa kwa mzozo uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi wa tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana.

Condoleezza Rice amewaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba kuna haja ya kila mkenya kuwa na utulivu na kuziunga mkono juhudi za Kofi Annan kutafuta makubaliano kati ya rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Condoleeza Rice ambaye alikuwa akikutana na waziri wa mashauri ya kigeni wa Albania, Lulzim Basha, kujadili maswala mengine, amesema atawasiliana na Kofi Annan hii leo kutathmini vipi Marekani na nchi nyingine zinavyoweza kusaidia kuumaliza mzozo huo wa kisiasa nchini Kenya.