1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KABUL : Afghanistan na Pakistan wakamilisha mazungumzo

13 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBZp

Viongozi wa kikabila wa Afghanistan na Pakistan wamekamilisha kikao chao cha pamoja cha amani cha baraza la jirga mjini Kabul kwa wito kwa serikali za nchi hizo kushinikiza vita nyumbani dhidi ya ugaidi na kuahidi kutoruhusu kuwepo kwa hifadhi za magaidi na kambi za mafunzo katika ardhi za nchi zao.

Lakini katika kile kinachonekana kama ni uungaji mkono wa wenyeji kwa kundi la Taliban na Al Qaeda katika jamii nyingi zinazoishi kwenye maeneo ya mbali ya mpakani ambazo zimewakilishwa kwenye baraza hilo wajumbe 650 pia wameamuwa kuunda baraza dogo la wajumbe 50 mashuhuri kuanzisha mazungumzo ya amani na usuluhishi na upinzani.

Rais Pervez Musharraf wa Pakistan ameamuwa kushiriki kikao hicho dakika za mwisho kuungana na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan kufunga kikao hicho kilichofanyika kwenye hema kubwa kabisa katika mji mkuu wa Kabul na kutowa wito kwa nchi hizo mbili kuacha mfarakano na kuungana dhidi ya waasi pamoja na kupiga vita biashara ya kasumba yenye kugharamia wanamgambo.