1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KABUL: Ripoti zagongána kuhusu mateka wa Kijerumani

21 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBgR

Ripoti zisizothibitishwa zimemnukulu msemaji wa Taliban akisema kuwa wahandisi 2 wa Kijerumani waliotekwa nyara wameuawa.Kwa upande mwingine, wizara ya masuala ya nje ya Afghanistan,mjini Kabul imesema,Mjerumani mmoja amefariki kutokana na ugonjwa wa moyo na wa pili yungali hai.Kwa hivyo matamshi ya wizara hiyo yanagongána na madai ya msemaji wa Wataliban,kuwa mateka wote wawili wameuawa kwa sababu,Ujerumani haikutimiza madai ya Taliban ya kuondosha vikosi vya Ujerumani kutoka Afghanistan.

Wakati huo huo,msemaji wa wizara ya masuala ya nje ya Ujerumani,mjini Berlin amesema,hakuna hakikisho huru kuhusu kuuawa kwa mateka hao wa Kijerumani.

Serikali ya Ujerumani mara kwa mara imesisitiza kuwa haitokubali kushinikizwa.Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel amepinga kuondosha vikosi vya Ujerumani,akisema kazi za kufanya ukarabati wa huduma za kirai,zinapaswa kuendelea.

Ujerumani ina wanajeshi 3,000 kaskazini mwa Afghanistan,vikiwa ni sehemu ya vikosi vya NATO vinavyosimamia usalama nchini humo.