1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KABUL: Watu sita kuhojiwa na polisi kuhusiana na mauaji ya wajerumani wawili

9 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD4a

Maofisa wa usalama nchini Afghanistan wanataka kuwahoji watu sita wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya waandishi wawili wa habari raia wa Ujerumani.

Karen Fischer na Christian Struwe, waliokuwa wakifanya kazi na shirika la habari la Deutsche Welle, walipigwa risasi juzi Jumamosi asubuhi katika hema lao mkoani Beghlan, yapata kilomita 120 kaskazini mwa mji mkuu Kabul.

Walikuwa safarini kutoka Baghlan kuelekea mkoa wa kati wa Bamiyan wakati walipopiga kambi kulala waweze kuendelea na safari yao asubuhi.

Msemaji wa Taliban amesema kundi hilo halikuhusika na mauaji hayo. Waandishi hao walikuwa wakifanya utafiti wao na walikuwa wamekutana na wanajeshi wa Ujerumani katika jeshi la NATO kaskazini mwa Afghanistan.

Ujerumani ina wanajeshi 2,800 chini ya uongozi wa NATO nchini humo.

Wakati huo huo, maofisa watatu wa serikali waliokuwa wakienda kuchunguza kisa cha shule kuchomwa moto mashariki mwa Afghanistan, wameuwawa mapema leo baada ya bomu lililokuwa limetengwa kando ya barabara kuliripua gari lao.