1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kadhia ya Kurnaz yapaliliwa na afisa wa zamani wa Marekani

Oummilkheir2 Machi 2007

Kizungumkuti kikubwa chamfika waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier

https://p.dw.com/p/CHIy
Murat Kurnaz ,mturuki anaeishi Ujerumani aliyeshikiliwa kwa makosa Guantanamo
Murat Kurnaz ,mturuki anaeishi Ujerumani aliyeshikiliwa kwa makosa GuantanamoPicha: AP

Murat Kurnaz,mturuki anaeishi Ujerumani,alishikiliwa kama gaidi mtuhumiwa kwa zaidi ya miaka mine katika kambi ya wafungwa ya Guantanamo.Tuhuma hizo zilidhihirika kua hazina msingi,hata hivyo palipita miaka mine hadi alipoachiwa huru.Sababu mojawapo ni kwamba serikali ya wakati ule ya Ujerumani ilizuwia asirejeshwe humu nchini.Mshika bendera wa yote hayo anasemekana kua waziri wa mambo ya nchi za nje Frank Walter-Steinmeier ambae wakati ule alikua mkuu wa ofisi ya kansela akisimamia pia shughuli za idara za upelelezi.Kamati ya uchunguzi imeundwa na bunge la shirikisho Bundestag kuishughulikia kadhia.Kamati hiyo inakumbwa na mtafaruku baada ya tuhuma zaidi kutolewa na afisa mmoja wa serikali ya Marekani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anajikuta akikumbwa na kizungumkuti kikubwa cha kadhia hii ya Murat Murnaz.Kadhia hiyo imezidi makali kutokana na hoja zilizotolewa jana usiku na mjumbe maalum wa serikali ya Marekani aliyekua akishughulikia suala zima la Guantanamo,Pierre Prosper.Alihojiwa katika kipindi cha “Monitor” cha kituo cha televisheni cha ARD bwana Pierre Prosper amezisuta hoja za waziri wa mambo ya nchi za nje Frank Walter Steinmeier aliyesema serikali kuu ya wakati ule kila kwa mara ilikua ikizungumza na serikali ya Marekani juu ya uwezekano wa kuachiwa huru Murat Kurnaz na kwamba waliendeleza juhudi za kutaka kijana huyo mwenye uraia wa Uturuki aachiliwe huru.Afisa huyo wa zamani wa serikali ya Marekani amesema “hakujakua na dalili yoyote kutoka Ujerumani.”

Msemaji wa waziri wa mambo ya nchi za nje,Steinmeier,Martin Jäger amesema kilichosemwa na Prosper hakiingii akilini,kwasababu serikali kuu ya Ujerumani ,tangu mwaka 2002 ilikua kila kwa mara ikiijishughulisha na kisa cha Kurnaz.

Suala kwa jinsi gani serikali kuu ya Ujerumani imejishughulisha hasa na kuachiliwa huru Murat Kurnaz,kuanzia mwaka 2002,lilikua lipatiwe jibu kwa kudurusiwa na wajumbe wa kamati ya uchunguzi ya bunge,madaftari ya idara ya upelelezi ya jimbo la Bremen.Idara hiyo ilimtaja kijana huyo anaeishi Bremen,Murat Kurnaz kua ni hatari.Na makadirio hayo ndiyo sababu ya kupitishwa uamuzi na mkuu wa idara kuu ya upelelezi BND na kwa hivyo pia serikali kuu ya wakati ule,Murat Kurnaz aliyekua akishikiliwa katika kambi ya Marekani ya Guantanamo asiachiwe kurejea Ujerumani pindi akiachiliwa huru.Waziri wa mambo ya nchi za nje Frank Walter Steinemeier ambae wakati ule alikua mkuu wa ofisi ya kansela,alikuwepo uamuzi huo ulipopitishwa.

Madaftari hayo yalikuwa yawasilishwe mbele ya kamati ya uchunguzi tangu wiki iliyopita.Lakini mpaka hii leo bado hayajafika.Kuna wanaosema madaftari hayo yanakutikana katika ofisi za wakala wa jimbo la Bremen mjini Berlin.Ndio maana mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi Siegfried Kauder ameamua hapo jana,kuakhirisha kusikilizwa hoja za mwenyekiti wa idara kuu ya upelelezi BND ERNST UHRLAU na mashahidi wengineo.

“Kwa kua mpaka leo hayajafika si katika ofisi ya kamati ya uchunguzi na wala si ofisini kwangu,sina njia nyengine isipokua kuakhirisha kwa wiki moja mpango wa kuwahoji mashahidi.Bila ya madaftari hayo hakuna cha maana kamati ya uchunguzi inachoweza kukifanya.”

Mkuu wa wawakilishi wa walinzi wa mazingira katika kamati hiyo Hans Christian Ströbele anahisi madaftari hayo hayakaweii bure,pengine anasema yamepelekwa akwanza wizara ya mambo ya ndani.

Kamati ya uchunguzi wa kadhia ya Murat Kurnaz inapanga kuwasikiliza mashahidi march nane ijayo.Waziri wa mambo ya nchi za nje Frank Walter Steinemeier atahojiwa March 22 ijayo na kamati hiyo.