1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame kugombea muhula wa tatu Rwanda

1 Januari 2016

Rais Paul Kagame wa Rwanda ametangaza nia yake ya kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi wa mwaka wa 2017, akithibitisha uamuzi uliotarajiwa na wengi

https://p.dw.com/p/1HWgx
Ruanda Präsident Paul Kagame
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Senne

Hii ni baada ya kuidhinishwa kwa marekebisho ya katiba yanayomruhusu kusalia madarakani kwa miaka mingi ijayo.

Akizungumza katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja na televisheni ya nchi hiyo, Kagame aliwaambia wananchi kwenye mkesha wa Mwaka Mpya kuwa ameitikia wito wao huo ingawa "Rwanda haihitaji kiongozi wa milele."

Kagame amekuwa madarakani tangu mwaka wa 2000, akiwa anadhibiti takribani kila muhimili wa utawala tangu jeshi lake la waasi lilipoingia mjini Kigali kusitisha mauaji ya halaiki ya mwaka wa 1994.

Awali alikuwa amewekewa ukomo wa mihula miwili, lakini mwaka wa 2015, Rwanda iliidhinisha marekebisho ya katiba ambayo yanamruhusu sasa kusalia madarakni hadi mwaka wa 2034 ikiwa atashinda uchaguzi. Kagame kwa miezi kadhaa alisisitiza kuwa hakuwa amefanya uamuzi kuhusu kama angegombea katika uchaguzi wa 2017 au la.

Ruanda Volksabstimmung über Zukunft von Präsident Kagame
Warwanda waliidhinisha marekebisho ya katibaPicha: picture-alliance/dpa/J. Johannsen

Kura ya maoni kuhusu mabadiliko hayo, ambayo ilipata asilimia 98 ya wale walipiga kura zao, ilizusha shutuma kutoka kwa mataifa yenye nguvu ya magharibi ambayo yana wasiwasi kuhusu orodha inayoendelea kuongezeka ya viongozi wa Afrika ambao wamekuwa wamekuwa wakitafuta mbinu za kuongeza mihula yao madarakani.

Nchi jirani Burundi ilitumbukia katika machafuko mwezi Aprili wakati tangazo la Rais Pierre Nkurunziza kuwa angegombea kwa muhula wa tatu lilizusha miezi kadhaa ya maandamano ya barabarani na vurugu ambazo zilisababisha vifo vya karibu watu 400. Kisha alishinda uchaguzi huo bila kupingwa.

Makundi ya haki za binaadamu yanakiri kuwa Kagame ana uungwaji mkono mkubwa kwa juhudi zake za kulijenga upya taifa hilo lakini wanaiokosoa serikali kwa kuvibana vyombo vya habari na sauti za upinzani, madai ambayo serikali inakanusha.

Marekani, ambayo kwa muda mrefu imemsifu Kagame kwa kuibadilisha nchi hiyo tangu mauaji ya halaiki mwaka wa 1994, inasema rais huyo anaweza kulihudumia vyema taifa lake kwa kujiuzulu katika mwaka wa 2017.

Umoja wa Ulaya ulikosoa kasi ambayo kura ya maoni iliandaliwa, ukisema haikutoa muda wa kutosha kwa wananchi kuzingatia hoja zao. Kura ya maoni ilifanyika karibu mwezi mmoja baada ya bunge la Rwanda kutoa idhini ya mwisho kwa mabadiliko hayo kufanywa.

Kuna chama kimoja tu cha kweli Rwanda. Chama cha Kidemokrasia cha Kijani, ambacho ni kidogo mno na hakina viti bungeni, kiliwasilisha kesi mahakamani ambayo haikufua dafu ya kupinga marekebisho hayo ya katiba.

Mabadiliko ya katiba yanamruhusu Kagame kugombea kwa muhula mwingine wa miaka saba katika mwaka wa 2017, ukifuatwa na mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.

Mwandishi: Bruce Aman/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef