1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagwe: Hakuna fedha ya COVID-19 iliyotafunwa Kenya

Shisia Wasilwa,3 Septemba 2020

Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe amedai kuwa hakuna fedha zilizofujwa za kukabiliana na virusi vya Corona. Akijijitea mbele ya Kamati ya Bunge Kagwe amesema fedha iliyopotea ni hasara iliyopotikana ya kununua vifaa

https://p.dw.com/p/3hwGx
Kenia Gesundheitsminister Mutahi Kagwe
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

"Mimi sijawahi kufika katika Shirika la Ugavi wa Vifaa vya Matibabu”(KEMSA)...ndivyo alivyojitetea waziri wa Afya Mutahi Kagwe, alipoulizwa iwapo aliwahi kushawishi bodi ya shirika hilo, kuwapa zabuni marafiki zake kupitia jumbe za simu. Hata hivyo amekiri kuwa Wizara yake hutoa mwongozo kwenye sera za shirika hilo la Ugavi wa Vifaa vya Matibabu.

Kagwe alikuwa anajibu madai ya Afisa Mkuu Mtendaji wa KEMSA aliyetimuliwa kazini kwa muda, John Manjari, kuwa yeye pamoja na Katibu Mkuu katika Wizara hiyo Susan Mochache walikuwa wanamshinikiza kuwapa zabuni watu ambao hawajatajwa hadi sasa. Kagwe anakanusha wizi fedha:

"Hakuna hasara ambayo imepatikana ikizingatiwa vitu vilivyonunuliwa. Hasara pekee ambayo iliyopo ni ya ununuzi wa vifaa kwa bei ya juu wakati huo. Hasara hiyo ni ya kiuendeshaji", alisema Kagwe.

Aidha Kagwe amekanusha kuuzwa kwa barakoa za msaada zilizotolewa na bilionea wa China Jack Ma katika taifa jirani la Tanzania. Wizara ya Afya ilinunua barakoa zenye thamani ya shilingi milioni 300, lakini hazijatolewa kwa watu. Katibu Mkuu katika Wizara hiyo Susan Mochache aliiambia kamati hiyo ya Bunge kuwa Wizara yake ilitengewa shilingi bilioni 23 za kukabiliana na janga la COVID-19.

Kenia Corona-Pandemie
Afisa wa hospitali ya Kenyatta akizungumza na mgonjwa katika wadiPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Inganga

Hata hivyo wajumbe wa Kamati ya Bunge walisema kuwa wakenya wengi hawajanufaika na barakoa pamoja na fedha hizo. Wakurugenzi watatu Wakuu wa Shirika la KEMSA wametimuliwa kazini kuhusiana na wizi wa mabilioni ya fedha zilizokusudiwa kupambana na janga la Corona. Naibu Rais William Ruto amejitokeza kuwa mkosoaji mkubwa kwenye sakata hiyo akisema; "Kwa kulewa mamlaka, mnatumia nafasi hiyo kuwaibia wakenya, kuendeleza ufisadi, mpaka leo KEMSA inasemekana kuwa kuna mabilionea wa corona, hamna aibu na utu, kwamba watu wana matatizo mengi?

Kenya yathibitisha kisa cha kwanza cha Corona

Rais Uhuru Kenyatta ameliagiza Shirika hilo la Ugavi wa Vifaa vya Matibabu kuchapisha majina ya watu na kampuni zilizoshinda zabuni ya vifaa vya matibabu katika kipindi cha siku 30. Kamati ya Bunge kuhusu Afya, imefahamishwa kuwa vifaa vya matibabu vyenye thamani ya shilingi bilioni 6.2 vingali katika ghala la Shirika la Ugavi wa Vifaa vya Matibabu nchini.

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi