1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamata kamata ya wanajeshi na majaji yaendelea Uturuki

Caro Robi17 Julai 2016

Maelfu ya raia wa Uturuki walijitokeza jana (16.07.2016) kumuunga mkono Rais Recep Tayyip Erdogan baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali lililofanywa na jeshi Ijumaa usiku kutibuka.

https://p.dw.com/p/1JQGw
Picha: Reuters

Jaribio hilo la kuipindua serikali ya Uturuki limesababisha vifo vya takriban watu 265 na maelfu ya wengine kujeruhiwa. Serikali ya Erdogan inamshutumu hasimu mkuu wa Rais Erdogan, Sheikh Fethullah Gulen, aliye uhamishoni Marekani kwa kuhusika na njama hiyo ya mapinduzi, madai ambayo Gulen ameyakanusha vikali na kulaani jaribio hilo la mapinduzi ya serikali.

Maafisa nchini Uturuki wamewakamata takriban watu 3,000 wanaoshukiwa kuhusika katika njama ya kuipindua serikali na kuagiza maelfu ya majaji nchini humo kukamatwa.

Kiasi ya majaji na waendesha mashitaka 3,000 wameondolewa kutoka nyadhifa zao na agizo la kukamatwa kwao limetolewa kwa kudaiwa kushirikiana na Gulen kutaka kuipindua serikali.

Gulen alaumiwa kwa kuchochea uasi

Erdogan anamlaumu Gulen kwa kujaribu kuchochea uasi katika jeshi, vyombo vya habari na idara ya mahakama nchini Uturuki. Uturuki imeitaka Marekani kumrejesha Gulen nchini humo. Marekani imesema iko tayari kuisadia Uturuki kubaini ni kina nani walihusika na njama hiyo lakini imeweka wazi itachukua hatua iwapo kutakuwa na ushahidi Gulen alihusika.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/M. Sezer

Akizungumza hapo jana mjini Istanbul, Erdogan amesema waliohusika katika jaribio hilo lililofeli wataadhibiwa vikali na kuongeza uasi huo wa baadhi ya wanajeshi ni zawadi kutoka kwa Mungu kwasababu itakuwa ni sababu ya kile alichokitaja 'kulitakasa jeshi'.

Miongoni mwa waliokamatwa ni makamanda wakuu wa jeshi akiwemo mkuu wa kikosi cha jeshi kinacholinda mipaka ya taifa hilo na Syria, Iraq na Iran.

Mamia ya wanajeshi wanazuiwa mjini Ankara kwa kudaiwa kuhusika katika mapinduzi hayo, na kusababisha vituo vya polisi kuwa na msongamano mkubwa wa waliokamatwa.

Erdogan ameitawala Uturuki, taifa lenye idadi ya watu milioni 80 tangu mwaka 2003. Rais wa Marekani Barack Obama ameeleza kuiunga mkono serikali ya Uturuki na kuzitaka pande zote nchini humo kuepuka kuliyumbisha taifa hilo na kuzingatia sheria.

Marekani yahusishwa na mapinduzi

Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amemuonya mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu dhidi ya kuihusisha Marekani na njama hiyo ya kuipundua serikali na kuongeza madai hayo ni uwongo mtupu na huenda ikaathiri uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Wafuasi wa Erdogan wakisherehekea baada ya jaribio la mapinduzi kufeli
Wafuasi wa Erdogan wakisherehekea baada ya jaribio la mapinduzi kufeliPicha: Reuters/Y. Karahan

Matukio hayo ya hivi karibuni yanatarajiwa kuiathiri sekta ya utalii ya Uturuki ambayo tayari imeathirika kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi nchini humo.

Kufikia jana mchana, shirika la habari la CNN la Uturuki liliripoti maafisa wa usalama wamekamilisha operesheni dhidi ya waliopanga mapinduzi.

Katika nchi jirani ya Ugiriki, maafisa nchini humo waliwakamata watu wanane waliokuwa katika ndege ya kijeshi ya Uturuki iliyotua katika mji wa kaskazini mwa nchi hiyo wa Alexandroupolis.

Wakati huo huo, serikali ya Uturuki imetangaza kambi ya jeshi la anga ya Incirlik imefungwa kufuatia jaribio hilo la mapinduzi.

Kambi ya Incirilk yafungwa

Kambi hiyo inatumika na muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani pamoja na jeshi la Ujerumani na ni kituo maalumu cha operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la wanamgambo wenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu IS.

Ndege za kivita za Ujerumani katika kambi ya kijeshi ya Incirlik
Ndege za kivita za Ujerumani katika kambi ya kijeshi ya IncirlikPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Inashukiwa kuwa kambi hiyo ilitumika na wanajeshi walioshiriki katika jaribio la kutaka kuipindua serikali ya Uturuki hapo juzi usiku.

Mapema mwezi huu, wabunge kadhaa wa Ujerumani walizuiwa kuitembelea kambi hiyo, huku kukiwa na mvutano uliotokana na Ujerumani kuyatambua mauaji yaliyofanywa na utawala wa Ottoman dhidi ya Waarmenia mwaka 1915 kuwa ni mauaji ya halaiki.

Huku hayo yakijiri, Marekani imewaonya raia wake dhidi ya kusafiri kuelekea Uturuki. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeonya kuwepo ongezeko la kitisho kutoka kwa makundi ya kigaidi kote Uturuki na kuwaonya raia wake dhidhi ya kusafiri kuelekea hasa kusini mashariki mwa Uturuki.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Yusra Buwayhid