1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi zote zisizokuwa halali zitabomolewa!asema Sarkozy

17 Septemba 2010

Ufaransa imeshikilia kuwa itaendelea kuzibomoa kambi za Waroma zisizokuwa halali na ikajitetea kuwa ni kwasababu za kiusalama.

https://p.dw.com/p/PEO1
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy,kwenye kikao cha EUPicha: AP

Wakati huo huo, matamshi ya Kamishna wa Umoja wa Ulaya wa Sheria, Vivian Reding, bado yanaendelea kuikera Ufaransa. Rais Sarkozy amezielezea kauli hizo kuwa ni za kushtua na hazikuwa na nia njema. Yote hayo yametokea wakati wa kikao cha kilele cha Umoja wa Ulaya kilicholazimika kuiacha ajenda yake ya kuyajadili masuala ya kuimarisha biashara,uchumi na sera za kigeni.Hata hivyo kilifanikiwa kuyatimiza baadhi ya walioyaorodhesha.

Ajenda yasambaratika

Matamshi hayo ya Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa yaliisambaratisha ajenda ya kikao hicho cha kilele cha viongozi wa Umoja wa Ulaya. Akizungumza kwa ghadhabu, Rais Sarkozy alisema kuwa,''Kamwe hatua ya kuwafurusha Waroma haifafani na kilichotokea wakati wa vita vya dunia na kwamba kauli hizo zinatia uchungu.''Kiongozi huyo wa Ufaransa alishikilia kuwa serikali itaendelea kuzibomoa kambi zote zisiso halali ziwe za yeyote yule. Alijitetea zaidi na akasema kuwa ,''Matamshi ya Kamishna wa Masuala ya Sheria wa Umoja wa Ulaya hayakuwa na nia njema.'' Kufuatia yote hayo Kansela Merkel wa Ujerumani alikubaliana na maelezo hayo na akasema kuwa ,''Inasikitisha kwamba tukio hilo limefananishwa na maovu yaliyotokea wakati wa vita vya dunia,'' ila anaafiki kwamba kauli hizo hazikuwa za kufurahisha kwa kweli na maneno aliyoyatumia pia hayakupendeza.''Tunawajibika kuheshimiana…kwenye taasisi zetu na pia kati yetu. Hilo ni la msingi,'' alisisitiza.

NO FLASH Merkel Sarkozy Roma Abschiebung
Rais Nicolas Sarkozy na Kansela Angela Merkel wakinong'onezana kikaoniPicha: AP

Kuupoza moto

Mtazamo wa Kansela Merkel uliungwa mkono na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron. Ili kujaribu kuyapoza moto malumbano hayo, Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy aliwatolea wito viongozi hao kuelewana pasina kuacha kuheshimiana.

Kwa mujibu wa kiongozi wa Jumuiya hiyo, Umoja wa Ulaya una kauli ya pamoja inayoupinga ubaguzi ulio na misingi ya kiraia au kikabila ijapokuwa nchi wanachama zina wajibu wa kuhakikisha kuwa heshima inakuwapo wakati wote kadhalika kuzifuata taratibu zilizopo. Itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa wiki hii Kamishna wa masuala ya sheria wa Umoja wa Ulaya Viviane Reding aliikosoa serikali ya Rais Nicolas Sarkozy na hata akatishia kuwa ataliwasilisha suala hilo kwenye Mahakama ya Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo mwanasiasa huyo wa Umoja wa Ulaya tayari ameshaiomba radhi Ufaransa ila bado mvutano wa kidiplomasia bado unatokota. Ili kuinusuru hali hiyo, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, alisisitiza ,''Ubaguzi wa aina yoyote ile wa walio wachache hapa barani Ulaya kamwe haukubaliki.Kuheshimiana kati yetu ni jambo muhimu kwa Umoja wa Ulaya.''

Demonstrationen Frankreich Sarkozy Roma Politik
Maandamano Paris ilipoanza bomoabomoa ya kambi zisizo halali za WaromaPicha: AP

Mlo wa mchana na kupapuana

Duru zinaeleza kuwa Bwana Barroso na Rais Sarkozy walipapuana wakati wa mlo wa mchana jambo ambalo kiongozi huyo wa Ufaransa analikanusha naye mwenzake alikuwa hana la kusema kuhusu suala hilo.

Itakumbukwa kuwa Kamishna Reding ni raia wa Luxembourg iliyo jirani ya Ufaransa. Waziri Mkuu wa Luxembourg, Jean Claude-Juncker, alilazimika kuitetea nchi yake na akafafanua kuwa haifai kulilaumu taifa lake kwa sababu matamshi hayo makali yalitolewa na mwanasiasa anayetokea kwao. Kulingana na Waziri Mkuu Juncker, pindi makamishna wanapoteuliwa kushika nyadhifa kwenye Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ndipo wanapoacha kuziwakilisha nchi wanazotokea.

Viviane Reding Vizepräsidentin EU-Kommission
Kamishna Viviane Reding wa EUPicha: DW

Baada ya purukushani zote hizo, kikao hicho kilifanikiwa kutia saini makubaliano ya kufanya biashara huru na Korea Kusini, kikaisihi Israel kuuongeza muda wa kusimamisha ujenzi upya kwenye Ukingo wa Magharibi na pia wakaafikiana kimsingi kuisaidia Pakistan iliyoathiriwa na mafuriko.    

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-AFPE/RTRE

Mhariri:Josephat Charo