1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni ya kupinga nyuklia yashinda Tuzo ya Amani ya Nobeli

6 Oktoba 2017

Kamati ya Tuzo ya Nobeli iliyoko Oslo, Norway, imemtangaza mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobeli wa mwaka huu. Ni kampeni ijulikanayo kama ICAN inayopambana na matumizi na utengenezwaji wa silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/2lKoG
Tuzo ya Amani ya Nobeli
Picha: Getty Images/AFP/J. Nackstrand

Mwenyekiti wa kamati ya kimataifa ya Nobeli  Berit Reiss Andersen ametangaza washindi hao hivi punde mjini Oslo, akisema: "Tunaishi katika ulimwengu ambao hatari ya kutumiwa silaha za nyuklia imezidi kuongezeka kuliko wakati wowote mwengine. Baadhi ya nchi zinazigeuza silaha zao za nyukilia ziwe za kisasa na kitisho ni kikubwa kwamba nchi zaidi zinajiandaa kumiliki silaha za nyuklia, mfano wa Korea ya Kaskazini," amesema Bibi  Reiss-Andersen. Ameyatolea wito madola yenye kumiliki silaha za nyuklia yaanze kujadiliana kwa dhati namna ya kujiepusha na silaha hizo.

Nembo ya kampeni ya ICAN ya kutokomeza silaha za nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Sweden Margot Walsstrom alisema kuipa kampeni hiyo ya ICAN tuzo ya amani ya Nobeli ni jambo lililostahiki. Alisema chama hicho kimekuwa kifanya kazi kubwa  tokea  2007 na kila mmoja anajua jinsi suala hilo lilivyo kubwa duniani kote.

Miongoni mwa watu na makundi 300 waliokuwa wamependekezwa kwa tuzo ya mwaka huu ni Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis na kundi linalojiita "White Helmets" linalookoa watu kutoka kwenye vifusi nchini Syria. Mshindi wa tuzo ya Nobeli hupewa medali pamoja na  fedha, kisiasi ya Dola za Kimarekani milioni 1.1.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kulisifia kundi hilo linaloendeleza kampeni ya kimataifa ya kutaka silaha za nyuklia kupigwa marufuku-ICAN kwa ushindi wake. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Guterres aliandika, "Kwa sasa tunahitaji zaidi ya wakati wowote ule dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia."

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, lessandwa Vellucci amesema Geneva kuwa tuzo hiyo bahati njema kwa utekelezwaji wa mkataba unaopiga marufuku silaha za nyuklia ambao ulitiwa saini na nchi 122 mnamo mwezi Julai.

Akizungumzia juhudi ambazo zimelipa shirika laake tuzo hiyo, mkurugenzi mtendaji wa ICAN Beatrice Fihn amesema wanafanya bidii sana kuhakikisha silaha za nyuklia ni haramu. Ameonmgeza kuwa: "Watu wamekuwa wakikubali silaha za nyuklia kama silaha halali za kujilinda, wajua kwa miaka 70 na sasa tunajaribu kubadili mtazamo huo, hakika haikubaliki kuhatarisha mji mzima  ili kujiweka mwenyewe kwenye hali ya usalama."

Mkurugenzi wa ICAN, Beatrice Fihn
Mkurugenzi wa ICAN, Beatrice FihnPicha: Reuters/D. Balibouse

Nayo Jumuiya ya kujihami ya NATO imefurahia tuzo hiyo kukabidhiwa kundi la ICAN ikisema juhudi za kumaliza mabomu ya atomiki lazima zitilie maanani vitisho halisi vya usalama wa ulimwengu. Jens Stoltenberg ambaye ni katibu mkuu wa jumuiya ya NATO ameipongeza  ICAN kwa kupokea tuzo hiyo na kusema NATO imejitolea kujenga mazingira yasiyokuwa na zana za nyuklia

Hata hivyo NATO ambayo wanachama wake watatu wana uwezo mkubwa wa silaha za nyuklia imeukosoa mkataba unaopiga marufuku zana za nyuklia wa Umoja wa Mataifa ikisema hali ya wanachama hao inaweza kuhujumu juhudi za kimataifa kuhusu mipango ya zana za Korea Kaskazini.

Tuzo hiyo imejiri wakati ambapo Korea Kaskazini imeisukuma dunia katika ukingo kufuatia misururu ya majaribio yake ya nyuklia na makombora, hali ambayo imezidisha hofu ulimwenguni. Katika hotuba yake wakati wa mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa mwaka huu, Rais Donald Trump alitishia kuiangamiza kabisa Korea Kaskazini. Aidha Trump ametishia kuiondoa Marekani kwenye mkataba wa kimataifa  pamoja na Iran kuhusu kudhibiti mpango wa nyuklia wa taifa hilo.

Ujerumani pia imeupongeza uamuzi wa kamati ya tuzo ya Nobel ya Amani kupatia ICAN tuzo hiyo. Kwenye mkutano wake wa mara kwa mara na waandishi wa habari mjini Berlin, msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema "serikali inaunga mkono lengo la kuwa na dunia isiyokuwa na silaha za nyuklia.

Kauli kama hiyo pia imetolewa na Umoja wa Ulaya uliosema kuwa utaendelea kutaka utekelezwaji wa mkataba wa kimataifa wa nyuklia na Iran na washirika wengine. Maneno hayo ya mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akizungumzia ushindi wa ICAN wa Tuzo ya Amani imejiri kufuatia ripoti kuwa Rais Trump huenda akatangaza wiki ijayo mpango wa kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia na Iran.