1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni ya uchaguzi ya CDU/CSU

24 Juni 2013

Kampeni ya uchaguzi ya vyama ndugu vya CDU/CSU ,visa vya upelelezi na uwezekano wa kuhukumiwa waziri mkuu wa zamani wa Italia Sylvio Berlusconi ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/18uyp
Mwenyekiti wa chama cha CSU,Seehofer (kushoto) na mwenyekiti wa chama cha CDU kansela Angela Merkel wakihudhuria mkutano ulifafanua sera za kampeni yao ya uchaguziPicha: Getty Images

Tuanzie lakini Berlin ambako wakuu wa vyama ndugu vya kihafidhina,Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union-CSU walikutana kudurusu mpango wa kampeni yao ya uchaguzi.Maoni ya wahariri yanatofautiana kuhusu kilichomo ndani ya mpango huo.Gazeti la "Thüringer Allgemeine" linaandika:

Si jambo la hikma kujichagulia mada hivi hivi tu ili kuwaumbia wote wengine.Kwa kufanya hivyo vyama ndugu vya CDU/CSU vinajivurugia muongozo wake wenyewe.Na zaidi ya hayo vinawakoroga wapiga kura.Bila ya shaka malipo ya juu ya fedha za uzeeni kwa akinamama,kuzidishwa kiwango cha fedha wanazolipwa watoto na marupurupu mengineyo ya watoto ni sawa na ni mambo yanayovutia.Hata hivyo na licha ya ahadi zote zinazotolewa katika kampeni za uchaguzi,ukweli ya mambo haustahiki kupuuzwa.Na ukweli huo unamaanisha yote hayo yatagharimiwa vipi?Si muda mrefu hivyo ,kansela Angela Merkel mwenyewe alikuwa akihimiza bajeti iimarishwe.Sasa,muda mfupi kabla ya uchaguzi,wanaipigia upatu ndoto ya kutoa zawadi badala ya kufunga mkaja.Ingekuwa jambo la busara wangefikiria mipango madhubuti na unayoingia akilini ya kugharimia miradi ya familia,na kuimarisha mashirika ya wastani ya kiuchumi.Hayo lakini wanahisi pengine hayavutii.

Upelelezi na madhara yake

Großbritannien Government Communications Headquarters Netzwerk
Makao makuu ya mawasiliano yanayotajikana kuwa kituo kikuu cha shughuli za upelelezi za UingerezaPicha: picture-alliance/dpa

Walimwengu wameduwaa tangu walipoanza kupata habari kwa jinsi gani taarifa zao fupi zinavyosomwa na kunaswa na idara za upelelezi za Marekani na Uingereza.Gazeti la "Landeszeitung" linajiuliza:"Kwani kuna anaestaajabu anaposikia kwa kiwango gani data zimekuwa zikikusanywa na idara za upelelezi? Hakuna.Tangu bei za computor zilipoporomoka,kila mmoja wetu ananasa zaidi picha na muziki ya digitali kuliko tunavyoweza kuziangalia picha hizo au kusikiliza muziki hiyo.Wenyewe wapelelezi  wanafanya kazi yao tu na kusikiliza kila wanachokipata.Ndo kusema tunabidi kuingiwa na wasi wasi?Bila ya shaka kwasababu hakuna ajuaye data hizo zinafanywa nini.CD zenye maelezo ya benki na kodi za mapato tayari watu wameingia mbioni kuzinunua,hapatapita muda pengine hata CD zinazohusu maisha ya watu binafsi zitauzwa.

Hatima ya Berlusconi

Silvio Berlusconi
Waziri mkuu wa zamani wa Italia Silvio BerlusconiPicha: Reuters

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu hukumu inayotaraajiwa kutolewa dhidi ya waziri mkuu wa zamani wa Italia Sylvio Berlusconi.Gazeti la Mittelbayerische Zeitung linaandika:"Katika mazingira ya kawaida,basi mtu anaweza kusema Berlusconi akihukumiwa na hatima yake ya kisiasa ingebidi pia iishie hapo.Lakini tangu alipopanda katika jukwaa la kisiasa miaka 20 iliyopita,hakuna tena mazingira ya kawaida nchini Italia. Mbinu za muda  mrefu za Berlusconi za kujiimarisha katika uwanja wa vyombo vya habari na kupanua mikakati yake,akifika hadi ya kuitaja mahakama kuwa ni chombo cha wafuasi wa mrengo wa shoto,zimeleta tija.Karibu wataliana milioni kumi wamempigia kura uchaguzi wa bunge ulipoitishwa mwishoni mwa mwezi wa februari mwaka huu.Kutokana na kudhoofika demokrasia ya Italia na ile hali ya kutoaminika taasisi nyingi za serikali,Berlusconi anategemea kuutumia umashuhuri wake kama turufu katika mapambano ya kujikomboa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mharir:Yusuf Saumu