1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za Uchaguzi zashika kasi Marekani

P.Martin31 Oktoba 2008

Siku ya uchaguzi wa Marekani ikikaribia,kampeni za kuwavutia wapiga kura zinazidi kushika kasi huku wagombea urais,John McCain wa Republikan na Mdemokrat Barack Obama wakituhumiana kuhusu hali ya uchumi nchini humo.

https://p.dw.com/p/Fl4q
Republican presidential candidate Sen. John McCain, R-Ariz. laughs as he his photographed prior to participating in a National Security Roundtable, Wednesday, Oct. 29, 2008, at The University of Tampa in Tampa, Fla. (AP Photo/Carolyn Kaster)
Mgombea urais wa chama cha Republikan,John McCain.Picha: AP

Kampeni hizo za uchaguzi zinakaribia siku zake za mwisho huku Mdemokrat Barack Obama akiongoza katika baadhi ya majimbo ambako Mrepublikan George W.Bush alishinda katika mwaka 2004.Lakini John McCain wa Republikan yupo nyuma katika kila jimbo alikoshinda Mdemokrat John Kerry 2004.Kama ilivyokuwa wakati wa chaguzi mbili zilizopita nchini Marekani,majimbo ya Ohio na Florida huenda yakaamua nani atakaejinyakulia ushindi wa uchaguzi wa Novemba 4.

Utafiti wa maoni Marekani ukionyesha kuwa Barack Obama yupo mbele ya McCain hata katika majimbo hayo mawili muhimu,Mrepublikan McCain alianzisha kampeni ya siku mbili katika jimbo la Ohio.Akipigania kuwavutia wapiga kura katika jimbo lililopoteza nafasi 100,000 za kazi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita tu,McCain alimtuhumu Obama kuwa Mdemokrat huyo hatochukua hatua za kupunguza faida za makampuni ya mafuta. McCain akakumbusha kuwa mwaka 2005 ni Obama alieunga mkono mswada wa nishati uliopendekeza kupunguza kodi inayolipwa na makampuni ya mafuta lakini yeye alipinga.Amesema,iwapo atachaguliwa rais,serikali yake haitoruhusu kulipa dola bilioni 700 kila mwaka kwa mafuta yanayotoka nchi zilizokuwa na chuki na Marekani.Badala yake amesema,serikali mpya moja kwa moja itachimba visima nje ya pwani yake.

Kwa upande mwingine,Mdemokrat Obama pia akiendelea na kampeni zake alihotubia mkutano wa hadhra katika mji wa Sarasota katika jimbo muhimu la Florida.Yeye aligusia ripoti iliyotolewa siku ya Alkhamisi kuwa uchumi wa Marekani umeporomoka vibaya sana katika kipindi cha miaka saba iliyopita.Kupunguka vibaya mno kwa pato la jumla la ndani amesema, huonyesha kuwa sera za uchumi za McCain na Rais George W.Bush wa Repiblikan hazijafanikiwa.McCain wakati huo alikuwa ubavuni mwa Bush akingojea kumpokea.Akaumbia umati uliokusanyika kuwa katika uchaguzi huu,suala lililo muhimu ni hatua gani zitakazochukuliwa na rais ajae kubadilisha mkondo huo?Licha ya utafiti wa maoni kuonyesha kuwa Obama anaongoza kidogo katika majimbo muhimu mawili ya Ohio na Florida, Mdemokrat huyo aliwakumbusha wafuasi wake kuwa bado hawajashinda uchaguzi.