1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampuni ya General Motors yasaidiwa isifilisike

Charo Josephat2 Juni 2009

Jaji wa Marekani aidhinisha msaada wa fedha kwa kampuni ya General Motors

https://p.dw.com/p/I1sj
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya General Motors Fritz HendersonPicha: AP

Jaji mmoja wa Marekani ameidhinisha dola bilioni 33.3 kama msaada wa kifedha kutoka kwa serikali kwa kampuni ya kutengeneza magari ya Marekani, General Motors, baada ya kampuni hiyo kuwasilisha ombi kutaka kulindwa isifilisike kwa mujibu wa ibara ya 11 ya sheria kuhusu muflis nchini Marekani.

Jaji anayehusika na maswala ya kufilisika kwa makampuni nchini Marekani amepitisha kwamba kampuni ya General Motors inaweza mara moja kupata dola bilioni 15 kama msaada wa fedha kutoka kwa serikali. Jaji huyo pia ameweka tarehe ya kusikilizwa kwa pendekezo la kuuzwa kwa sehemu kubwa ya mali za kampuni hiyo katika siku 30 zijazo.

Akizingatia kwamba kulikuwa na dharura ya kufanya hivyo, jaji Robert Gerber, hapo jana aliidhinisha kampuni ya General Motors ipate jumla ya dola bilioni 33.3, huku dola bilioni 15 zikitarajiwa kutolewa kwa ajili ya matumizi ya kampuni hiyo katika kipindi cha majuma matatu yajayo. Jaji Gerber ataamua kuhusu kuidhinisha rasmi kiwango jumla cha fedha kwa kampuni ya General Motors ifikapo Juni 25.

Akizungumza kuhusu hatima ya kampuni ya General Motors rais wa Marekani Barack Obama amesema,

"Nina matumaini hatua ninazozitangaza zitaashiria mwisho wa kampuni ya General Motors iliyozeeka na kuanzisha enzi mpya. Ningependa kuona kampuni mpya ya General Motors itakayoweza kutengeneza magari ya kisasa ya hali ya juu, yaliyo salama kwa mazingira na itakayokuwa tena ishara ya ufanisi wa Marekani."

Barack Obama vor AIPAC
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Rais Obama amesema kuiruhusu kampuni ya General Motors kuomba kusaidiwa kwa mujibu wa ibara ya 11 ya sheria za muflis ndio njia pekee ya kuisadia kampuni hiyo kufaulu na kuweza kushindana na kampuni nyingine za kutengeneza magari ulimwenguni. Hata hivyo amesema hana nia ya kusimamia shughuli za kila siku za kampuni hiyo.

" Kitu ambacho hatukifanyi na ambacho binafsi sina nia ya kukifanya, ni kuendesha shughuli za kampuni ya General Motors."

Hatua ya kampuni ya General Motors kuwasilisha ombi la kutaka isaidiwe isifilisike kwa mujibu wa ibara ya 11 ya sheria za muflis nchini Marekani, kunaifanya kuwa kampuni ya kwanza kubwa ya magari kufanya hivyo katika historia ya Marekani. Kampuni hiyo imesema ina deni la kiasi cha dola bilioni 172.8 na mali ya thamani ya dola bilioni 82.29.

Kampuni ya General Motors ina matumaini ya kufuata mkondo wa kampuni ya Chrysler kwa kubadili mali yake nyingi kuwa kampuni mpya katika siku 30 na kujikwamua kutokana na hali ya sasa ya kulindwa isifilisike. Serikali ya Marekani mjini Washington imesema inatarajia kampuni hiyo kuweza kufanya hivyo kati ya miezi miwili hadi mitatu.

Kampuni ya General Motors leo inatarajiwa kutangaza mpango wa kuuza aina ya gari lake la Huumer, lakini haitataja mnunuzi wala bei hadi baadaye. Tangazo hilo litatatolewa siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa kesi kuhusu muflis ya kampuni hiyo mahakamani, siku moja baada ya kuomba kulindwa isifilisike. Kampuni ya General Motors imetangaza haitatengeneza tena magari yake aina ya Pontiac na inatafuta wanunuzi wa magari aina ya Saturn na Saab. Magari aina ya Hummer huenda yasitengenezwe tena iwapo hakutapatikana mnunuzi mwezi huu wa Juni.

Tawi la Geneal Motors nchini Australia, Holden Ltd limesema halitaathiriwa na hatua ya kampuni mama kuomba isaidiwe isifilisike na kwamba itaendelea kuomba fedha kutoka kwa kampuni hiyo ili kuweza kuendesha shughuli zake. Meneja mkuu wa kampuni ya Holden, Mark Reuss, amesema leo kwamba tawi hilo la General Motors nchini Australia halijatangaza kupunguza nafasi za ajira licha ya hali ngumu ya kiuchumi.

Shughuli za kampuni ya General Motors barani Asia pia hazitaathiriwa, amesema kiongozi wa kampuni hiyo katika kanda ya Asia, Steven Carlisle.