1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uchumi

Kampuni ya Nakumatt yatangaza kufilisika

3 Novemba 2017

Kampuni yenye maduka makubwa aina ya "supermarket" ya nchini Kenya, Nakumatt, imetaka kusajiliwa kama kampuni iliyofilisika baada ya kuandamwa na utitiri wa madeni.

https://p.dw.com/p/2mxL3
Nakumatt
Picha: picture-alliance/dpa/epa/D. Kurokawa

Kampuni hiyo, iliyoanza kufanya kazi miaka 25 iliyopita ikiwa kama duka dogo la magodoro, huko maeneo ya  Bonde la Ufa nchini Kenya, ni miongoni mwa maduka makubwa yenye matawi mengi Afrika Mashariki. Chanzo kimoja cha habari kilicho karibu na kampuni hiyo kimesema Nakumatt inadaiwa na wasambazaji wake pamoja na wamiliki wa majengo wanayoyatumia,  karibu dola milioni 193  sawa na Shilingi bilioni 20 za Kenya.

Januari 2017, Mkurugenzi wa maduka hayo, Atul Shah aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa, madeni hayo yamefikia dola milioni 150. Chanzo hicho kimeeleza kuwa kwa makadirio, kampuni hiyo binafsi, ambayo imeajiri watu takribani  4,000 ina mtaji wa  Shilingi bilioni 2. Washindani  wakuu wa Nakumatt kwa sasa ni kampuni  ya ndani ambayo hisa zake hazijaorodheshwa katika soko la hisa, Carrefour,  inayofanya biashara za rejareja Ufaransa  na ambayo imeingia katika soko la Kenya, mwaka jana.

 Mara kadhaa wanaoidai Nakumatt wamekwenda mahakamani wakitaka kufungwa kwa biashara hizo kutokana na kushindwa kulipwa madeni yao. Gazeti la Bussiness Daily la nchini Kenya limewahi kuripoti kuwa wamiliki 19  wa majengo  yanayotumiwa na Nakumatt, wamewahi kuishitaki kampuni hiyo kwa deni la Shilingi 600 milioni.

Nakumatt
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

''Wakurugenzi wa Nakumatt,  wana uhakika kuwa mahakama itatoa amri  ya kuipa fursa Nakumat kuendelea na usimamizi wa kampuni hiyo, amri itakayoiwezesha kupata suluhisho sahihi kwa wadai wake,'' imesema  taarifa ya kampuni hiyo. Taarifa hiyo iliongeza kuwa, kama amri hiyo itatekelezwa, itaiwezesha Nakumatt  kujiimarisha   wakati ikiwa chini ya msimamizi aliyeidhinishwa na mahakama.

Maduka mengi yafungwa

Taarifa zimeeleza kuwa Nakumait inahitaji karibu mwaka mzima, ili kuweza kulipa madeni inayodaiwa na itakapoanza upya itakuwa kampuni ndogo  inayoweza kumiliki maduka kati ya 10 hadi 20. Wakati wa kilele cha mafanikio yake, Nakumatt ilikuwa na maduka zaidi ya 60 nchini Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda.  Nembo zake za sanamu ya tembo iliyotengenezwa kwa shaba huwekwa nje ya maduka hayo. 

Lakini katika miaka michache iliyopita, imekumbwa na dhoruba  ya kiuchumi na kusababisha  rafu katika maduka yake kubaki tupu, na maduka mengine kufungwa.

Washindani wao,  Tuskys walipeleka ombi la kuunganisha kampuni hizo mbili ili kutatua changamoto za Nakumat na wakaahidi kushirikiana nayo  ikiwa chini ya umiliki wa kampuni iliyoteuliwa na mahakama.

Mahakama Kuu, itasikiliza ombi la Nakumatt  kuhusu kufilisika kwake, Novemba 8.

Kwa ujumla, changamoto za Nakumatt, zimeleta msukosuko wa kiuchumi nchini Kenya mwaka huu, kutokana na  mshtuko wa uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti na ule wa marudio wa wiki mwezi Oktoba.

Mwandishi: Florence Majani

Mhariri: Daniel Gakuba