1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanali Gaddafi ashikilia yuko Libya na haondoki

8 Septemba 2011

Nchini Libya, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha siku chache zilizopita, Kanali Muammar Gaddafi amezikanusha vikali taarifa zinazosema kuwa amekimbilia nchi jirani ya Niger.

https://p.dw.com/p/12UrG
Bango la Kanali Muammar GaddafiPicha: dapd

Wakati huo huo, waasi wa Libya wanaendelea na mapambano na wanazitolea wito serikali za nchi jirani kuifunga mipaka yao ili kuwazuwia wafuasi wa Kanali Gaddafi wanaotoroka.

Michezo ya Kiakili na uvumi

Akizungumza kwa simu alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Arrai Oruba kilichoko mjini Damascus, Kanali Muammar Gaddafi alisema kuwa taarifa hizo ni uvumi mtupu na michezo ya kiakili. Kiongozi huyo alisisitiza kuwa lengo na dhamira ya maadui wake ni kuwavunja moyo wananchi wa Libya na hakuna haja ya kuzitilia maanani kauli zao. Kanali Gaddafi aliendelea kufafanua kuwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO inayoendelea na operesheni ya mapambano nchini humo haitafanikiwa kwani nyenzo zake itaikwamisha.

Ifahamike kuwa Kanali Muammar Gaddafi amekuwa akiwatolea wito waLibya kujikaza kupitia kanda za video zinazopeperushwa na kituo cha televisheni cha Arrai.

Flash-Galerie Gaddafi Familie Flucht Algerien Libyen Exil
Wana wa Kanali Muammar Gaddafi: Hannibal al-Gaddafi (kushoto), mkewe Safiya al-Gaddafi na bintiye Aisha al-GaddafiPicha: picture alliance/dpa

Mbunge wa Iraq

Kituo hicho cha televisheni kinasimamiwa na mbunge wa Iraq wa zamani wa Kisunni, Mishan al- Juburi. Bwana Juburi pekee ndiye anayeweza kuwasiliana na Kanali Gaddafi tangu alipokimbilia mafichoni pindi waasi wa Libya walipofanikiwa kuudhibiti mji wa Tripoli. Kulingana na Mbunge huyo wa zamani, Kanali Gaddafi na mwanawe wa kiume Saif al-Islam bado wako Libya na wana siha njema tayari kufa kwenye mapambano kwa ajili ya nchi yao. Kauli hizo zinaungwa mkono na mmoja ya viongozi wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi wanaoidhibiti ngome ya Bani Walid

Msimamo wa Niger

Kituo hicho cha televisheni kimekuwa kikizipeperusha taarifa nyingi za wana wa Kanali Gaddafi.

Kwa upande mwengine, baraza la mpito la waasi wa Libya linaripotiwa kuwa linahofu Kanali Gaddafi na washirika wake wataponyoka na kuingia kwenye nchi jirani kupitia mipaka ya karibu. Hata hivyo uongozi wa Niger umeyakanusha madai kwamba kiongozi huyo ameingia nchini humo.

Wasiwasi huo ulijitokeza baada ya msafara wa viongozi wa ngazi za juu wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi kuripotiwa kukimbilia Niger siku ya Jumatatu. Ili kuuzuwia uwezekano huo, baraza hilo la waasi limewapeleka wajumbe mjini Niamey kwa minajili ya kuwakamata na kuwazuia endapo wataonekana nchini Niger.

Libyen Rebellen vor Bani Walid September 2011 FLASH-GALERIE
Waasi wa Libya wakiwa Tarhouna: ngome ya Bani Walid bado imezingirwaPicha: dapd

Wafuasi sio wapambe

Hata hivyo, duru zinaeleza kuwa kati ya walioonekana wakiingia Niger mapema wiki hii, hakuna yeyote kati yao aliye kwenye orodha ya watu waliowekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Victoria Nuland, watu hao ni maafisa wa ngazi za juu na kijeshi wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi na kwa sasa wanazuiliwa mjini Niamey.

Msemaji huyo amesema kuwa wanawasiliana na serikali za Mali, Mauritania, Chad na Burkina Faso ili kuwasisitizia umuhimu wa kuyaheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa pamoja na kuuimarisha usalama kwenye mipaka yao.

Kwa upande wao Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso Alain Edouard Traore anasisitiza kuwa," Taarifa tulizonazo zinaashiria kuwa Gaddafi hayupo Burkina Faso. Kokote aliko..iwe ni Niger au kwengineko hatukujui na pia hatuna mawasiliano naye."

Jumamosi siku ya siku

Kauli hizo zinaungwa mkono na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Niger, Mohammed Bazoum, anayehudhuria kikao cha mataifa ya eneo la Sahel kinachofanyika mjini Algiers.

Kwa upande mwengine, waasi wa Libya wanajiandaa kupambana na wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi waliosalia kwenye ngome zilizoko eneo la Bani Walid, eneo la kusini mwa Tripoli, Sabha kwa upande wa kusini na mji wa pwani wa Sirte anakotokea kiongozi wa Libya.

Niger Präsident Mahamadou Issoufou
Rais wa Niger Mahamadou IssoufouPicha: picture alliance / dpa

Wanajeshi hao wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi wamepewa hadi siku ya Jumamosi wiki hii kujisalimisha.

Mwandishi: Mwadzaya, Thelma- RTRE/DPAE

Mhariri:Josephat Charo