1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel aelezea masikito yake kwa wahanga wa Kunduz

Oumilkher Hamidou8 Septemba 2009

Kansela Angela Merkel aonya dhidi ya kutolewa lawama hata kabla ya matokeo ya uchunguzi kujulikana

https://p.dw.com/p/JXGa
Kansela Angela Merkel ahutubia bungeniPicha: picture alliance/dpa

Kansela Angela Merkel amelihutubia bunge hii leo na kuelezea "huzuni zake za dhati" kwa "wahanga wasiokua na hatia" ,wa shambulio la ijumaa iliyopita la ndege za kijeshi za jumuia ya kujihami ya NATO, kaskazini mwa Afghanistan.

"Kila mtu mmoja aliyeuliwa bure nchini Afghanistan,ni hasara".

Amesema hayo kansela Angela Merkel bungeni hii leo na kusisitiza anahuzunishwa sana na kila aliyejeruhiwa bure au kuuliwa bure hata kama uamuzi umetokana na wajerumani.

Jumuia ya kujihami ya NATO imekiri hii leo kwamba raia wa kawaida pia wameuwawa na kujeruhiwa,katika hujuma za mabomu yaliyovurumishwa na madege ya NATO dhidi ya malori mawili ya mafuta yaliyoibiwa na wataliban huko Kunduz,kaskazini mwa Afghanistan.

Lakini kansela Angela Merkel hakulaani hujuma hizo-akisubiri matokeo ya utafiti rasmi unaofanywa.

Hujuma hizo zimesababisha kutolewa taarifa zinazopingana ,tangu nchini Ujerumani mpaka katika sehemu nyengine ya dunia,kuhusu idadi ya wahanga, kama raia ni miongoni mwa waliouwawa na pia kuhusu lengo la opereshini hiyo.

Kansela Angela Merkel anatilia mkazo umuhimu wa kufanywa uchunguzi wa kina na kusema:

"Uchunguzi wa kina wa tukio la ijumaa na madhara yake,ni jambo la lazima,kwangu mie binafsi na kwa serikali kuu ya Ujerumani kwa jumla.Jeshi la shirikisho litachangia kwa kila hali kurahisisha uchunguzi huo."Matokeo ya uchunguzi huo hatuwezi kuyaashiria hii leo.Lakini nnahakikisha kwamba hatutoficha chochote.Lakini nnasema pia hatutokubali lawama za pupa..."

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje na ulinzi wa Ujerumani wamelalamika jana kutokana na ukosefu wa mshikamano miongoni mwa baadhi ya mawaziri wenzao wa ulaya kuhusiana na kadhia hii.

Bundesaussenminister und Vizekanzler Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter SteinmeierPicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani,Frank Walter Steinmeier,amesema pia bungeni hii leo "hazielewi lawama zinazotolewa hata kabla ya uchunguzi kukamilishwa."

"Nimewapigia simu mawaziri kadhaa wa mambo ya nchi za nje,mwishoni mwa wiki iliyopita,kuwaambia wasubiri ,kama sisi mpaka matokeo ya uchgunzi yatakapotangazwa."Amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani-Frank Walter Steinmeier.

Kansela Angela Merkel amekumbusha pia kwamba kwa makubaliano pamoja na Ufaransa na Uengereza,serikali ya Ujerumani inapanga kuitisha mkutano kabla ya mwaka huu kumalizika ili kujadili namna serikali ya Áfghanistan itakavyoweza kudhamini uongozi mkubwa zaidi wa nchi hiyo.

Wiki chini ya tatu kabla ya uchaguzi mkuu kuitishwa nchini Ujerumani,katika wakati ambapo thuluthi mbili ya wajerumani wanataka wanajeshi wao 4200 warejeshwe nyumbani,bibi Angela Merkel anasema "kutumwa wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan ni kwaajili ya "masilahi ya usalama wa Ujerumani".

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri.Abdul-Rahman