1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel akutana na rais wa Urusi mjini Berlin

Oumilkher Hamidou31 Machi 2009

Kansela Merkel asisitiza umuhimu wa ushirikiano wa dhati pamoja na Urusi

https://p.dw.com/p/HNeW
Kansela Angela Merkel (wapili kushoto) na rais wa Urusi Dmitri Medwedew (kati)Picha: AP

Kansela Angela Merkel anakutana hii leo na rais wa Urusi Dmitri Medwedew mjini Berlin.Mada kuu mkutanoni ni pamoja na mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kiviwanda na yale yanayoinukia-G-20 mjini London.

Katika mkutano huo pamoja na kansela Angela Merkel,rais Dmitri Medwedew hatozungumzia pekee mkutano huo wa kilele unaoanza alkhamisi ijayo mjini London,japo kama hiyo ndio sababu hasa ya ziara yake rasmi mjini Berlin.Moscow inahisi imeachwa kando katika mazungumzo ya kutengenezwa upya mabomba ya gesi ya Ukraine,baada ya Bruxelles na Kiew kukubaliana kushirikiana.


Duru za kutoka ikulu ya rais mjini Moscow-Kremlin zinasema rais Dmitri Medwedew anapendelea mada hiyo ijadiliwe,sio kwasababu ya kupata msaada wa Berlin,hasha,bali kwasababu Ujerumani ndio inayotumia sehemu kubwa ya gesi ya Urusi na ndio maana ni muhimu suala hilo kujadiliwa.


Rais huyo wa Urusi anataka pia kuelezea madhara ya aina gani yanaweza kusababishwa na mzozo wa jamhuri ya Tcheki katika mdahalo kati ya Bruxelles na Moscow.Jamhuri ya Tcheki ndio mwenyekiti wa zamu wa umoja wa Ulaya kwa nusu hii ya kwanza ya mwaka 2009.


Mada nyengine ambayo bila ya shaka itajadiliwa inahusu jumuia ya kujihami ya NATO.Katika mkutano wa kilele wa jumuia hiyo utakaofanyika ijumaa na ijumamosi ijayo mijini Kehl na Strassbourg,baraza la ushirikiano la NATO na Urusi linatazamiwa kuanza rasmi shughuli zake.Shughuli hizo zilisitishwa kufuatia vita katika eneo la Caucasus.


Tangu siku kadhaa zilizopita kansela Angela Merkel amekua akizungumzia umuhimu wa kushirikiana kwa dhati na Urusi katika masuala ya usalama.Kansela Angela Merkel anasema:

"NATO inataka kuwa na ushirikiano mzuri na Urusi.Uhasama wetu umemalizika tangu miaka 20 iliyopita.Enzi za vita baridi zimeshapita na kamwe hazitarejea."


Rais Dmitri Medwedew anapanga kukutana pia na wawakilishi wa sekta ya kiuchumi ya Ujerumani mjini Berlin.Makampuni ya Ujerumani yanapanga kuwekeza yuro bilioni tisa mwaka huu katika miradi mbali mbali nchini Urusi.

Muandishi;Hamidou Oummilkheir

Mhariri;Abdul rahman