1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel ziarani barani Afrika

Oummilkheir3 Oktoba 2007

Kansela angela Merkel atahutubia Umoja wa afrika mjini Addis Ababa na kuhimiza utawala bora,,haki za binaadam na demokrasia

https://p.dw.com/p/CH7D
Picha: AP

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameanza ziara yake ya kwanza barani Afrika,kwa kuitembelea Ethiopia.Atafika pia Afrika kusini na Liberia.Lengo ni kushadidia ushirikiano wa kisiasa chini ya misingi ya haki za binaadam na utawala bora.

Ushirikiano pamoja na Afrika kwa kuheshimu misingi ya haki za binaadam na utawala bora ndio kiini cha mkutano wa viongozi wa mataifa tajiri kiviwanda waliokuta Heiligendamm,kaskazini mashariki ya ujerumani mwezi June uliopita na huo ndio ujumbe anaokwenda nao barani Afrika.

Kansela Angela Merkel atasisitiza pia juu ya “mkakati wa pamoja wa umoja wa ulaya na Afrika.

Duru za serikali kuu ya Ujerumani zinasema viongozi kadhaa wa bara la Afrika wamekua wakitilia mkazo haja ya kuiona Ujerumani ikiwajibika zaidi barani humo katika wakati ambapo ushawishi wa kiuchumi unaozidi kukua wa China,unazidi kuwatia wasi wasi viongozi wa ulaya.

Katika kituo chake cha kwanza mjini Addis Ababa kansela Angela Merkel atahutubia mbele ya Umoja wa Afrika hii leo na kuzungumza na mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja huo,Alpha Omar Konare wa Mali na mwenyekiti wa umoja wa Afrika John Agykum Kufour wa kutoka Ghana.

Mbele ya umoja wa Afrika sawa na ilivyokua hapo awali wakati wa mazungumzo yake pamoja na viongozi wa Ethiopia,ambapo hakuchelea kulizusha suala la haki za binaadam, kansela Angela Merkel anatazamiwa hii leo kulizusha suala la mzozo wa Darfour na Somalia ambako wanajeshi wa Ethiopia wanashirikiana na vikosi vya serikali ya mpito.

Atakapokua ziarani nchini Afrika kusini,ijumaa na jumamosi ijayo,ujumbe mdogo wa wafanyabiashara wanaofuatana na kansela Angela Merkel utaongezeka kutoka watu kumi na kufikia watu 21.

Nchi hizi mbili zimekua na biashara ya pamoja yenye thamani ya yuro bilioni 11 mwaka jana na zaidi ya makampuni 500 ya Ujerumani yameshaanza kuwekeza katika sekta za kibinafsi nchini Afrika kusini.

Haki za binaadam hazitaachwa kando pia nchini Afrika kusini,ambako kansela Angela Merkel anapanga pia kwenda Cape Town kuonana na Helen Zille,mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Afrika kusini.

Wakati wa mazungumzo yake pamoja na rais Thabo Mbeki kansela Angela Merkel amedhamiria kuzungumzia kinaga ubaga kuhusu Zimbabwe na kumuomba awe mkakamavu zaidi mbele ya Robert Mugabe.

Hata hivyo kansela Angela Merkel hatotishia kuususia mkutano wa kilele wa umoja wa Ulaya na Afrika,December ijayo,ikiwa rais Mugabe atahudhuria kama alivyofanya waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown.

“Kansela anataka kwa kila hali kuhudhuria mkutano huo nchini Ureno” duru za serikali ya ujerumani zimesema na kushadidia tunanukuu:”uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika ni muhimu kupita kiasi na hauwezi kuachiwa kugeuka mateka wa suala la kushiriki au la rais Robert Mugabe wa Zimbabwe” Mwisho wa kunukuu duru za serikali ya Ujerumani.Kuhusu mkutano huo kansela angela merkel anasema:

Nchini Afrika kusini Kansela Angela Merkel atafungua mradi uliolengwa kuwapatia mafunzo ya kazi vijana 45 elfu kwaajili ya michuano ya fainali ya kombe la dunia mwaka 2010-mfano way ale yaliyoshuhudiwa wakati wa michuano ya kombe la dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani.

Jumapili,katika ziara fupi nchini Liberia,kansela Angela Merkel atakutana na rais Ellen Johnson Sirleaf na kusifu juhudi zake katika kupiga vita rushwa na kuimarisha utawala bora.