1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel kukutana na Rais Erdogan wa Uturuki

23 Mei 2016

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akihudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya misaada nchini Uturuki anatarajiwa kumshinikiza Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kuhusu makubaliano ya wahamiaji ya Umoja wa Ulaya..

https://p.dw.com/p/1Isuw
Picha: Reuters/K. Ozer/Presidential Palace

Ingawa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ni mmojawapo ya viongozi wa ngazi ya juu kabisa kuhudhuria mkutano huo wa kilele masuala kadhaa muhimu kati ya Uturuki na Ujerumani yumkini yakapewa kipau mbele wakati atakapokutana na Rais Erdogan wa Uturuki baadae Jumatatu.

Merkel amekuwa akishutumiwa kwa kumridhia mno Erdogan wakati akitaka uungaji mkono wa serikali yake kwa makubaliano ya wahamiaji na Umoja wa Ulaya. Wakati fulani alidhihakiwa kuwa yuko upande wa Erdogan baada ya rais huyo kumfungulia mashtaka msanii wa vichekesho wa Ujerumani kwa shairi lake la tashtiti dhidi ya kiongozi huyo wa Uturuki.

Hapo jana gazeti la Ujerumani la Frankfurter Allgemaine Zeitung limemnukuu Merkel akishutumu mipango ya bunge la Uturuki kuwavuwa kinga ya kutoshtakiwa takriban theluthi moja ya wabunge hatua ambayo itawaathiri zaidi wabunge wa Kikurdi.Pia ameshutumu kukwama kwa mchakato wa usuluhishi na Wakurdi ambao ulivunjika hapo mwaka 2015 wakati matumizi ya nguvu yalipozuka tena kati ya chama cha Wafanyakazi cha Kurdistan cha (PKK) na serikali.

Masuala muhimu kujadiliwa

Merkel amesema anapanga kuyazusha masuala yote muhimu wakati wa mazungumzo yake na Erdogan ikiwa ni pamoja na mvutano wa kisiasa unaoendelea,utawala wa sheria na ushirikiano katika suala la sera ya wakimbizi.Chini ya makubaliano kuhusu wahamiaji ya Umoja wa Ulaya,Uturuki imekubali kuwarudisha nchini Ugiriki wakimbizi pamoja na kuwazuwiya wasiondoke nchini mwake kuelekea kwenye nchi za Umoja wa Ulaya.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Merkel ameliambia gazeti hilo kwamba anaangalia kwa makini kwa kiasi gani Uturuki inatimiza hasa ahadi zake ambapo hadi sasa imekuwa ikizitekeleza kwa uaminifu na bila ya shaka atazungumza na rais wa nchi hiyo juu ya hali ilivyo.

Akizungumzia mipango ya Umoja wa Ulaya kuruhusu wananchi wa Uturuki wasafiri katika nchi wanachama wa umoja huo bila ya kuhitaji visa Merkel amesema masharti waliyokubaliana yanapaswa kutimizwa kwanza : "Yanahusu kanuni ziliopo nchini Uturuki ambapo zinatakiwa zifanyiwe mabadiliko."

Erdogan agoma kubadilii sheria ya ugaidi

Erdogan amekataa kubadili sheria za nchi hiyo za kupiga vita ugaidi licha ya shinikizo kutoka Umoja wa Ulaya.

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: Reuters/O. Orsal

Gazeti la Bild la Ujerumani Jumatatu limetaja duru kutoka serikalini zikisema kwamba serikali haitaraji Waturuki wataruhusiwa kusafiri Umoja wa Ulaya bila ya kuhitaji visa kabla ya mwaka 2017 kwa sababu ya serikali ya nchi hiyo kushindwa kutimiza masharti iliyowekewa kabla ya kumalizika kwa mwaka huu.

Serikali ya Uturuki imekuwa ikidai kwamba tayari imetimiza kigezo cha Umoja wa Ulaya ili wananchi wa nchi hiyo waruhusiwe kusafiri katika nchi zinazounda Umoja wa Ulaya bila ya kuhitaji viza.

Uturuki na Umoja wa Ulaya zimekuwa zikijadili kuregezwa kwa masharti hayo ya visa tokea mwaka 2013 na zimekubaliana hapo mwezi wa Machi kuendelea na mpango huo kama sehemu ya makubaliano kwa Uturuki kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu wanaokimbilia Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP/dpa

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman