1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel ziarani Mashariki ya Kati

P.Martin2 Aprili 2007

Kansela wa Ujerumani,Angela Merkel akiendelea na ziara yake ya Mashariki ya Kati hii leo amewasili Beirut nchini Lebanon.

https://p.dw.com/p/CHH3
Kansela Merkel akikaribishwa na Waziri Mkuu Siniora mjini Beirut
Kansela Merkel akikaribishwa na Waziri Mkuu Siniora mjini BeirutPicha: AP

Mbali na kukutana na viongozi wa nchi hiyo,Merkel atawatembelea pia wanamaji wa Kijerumani wanaoshirikiana na vikosi vya Umoja wa Mataifa kulinda amani nchini Lebanon.

Kansela Angela Merkel,amepokewa na waziri mkuu wa Lebanon Fouad Siniora chini ya ulinzi mkali,alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut.Mbali na majadiliano yake pamoja na Siniora anaeungwa mkono na nchi za magharibi,Merkel vile vile anatazamia kukutana na spika wa bunge la Lebanon,Nabih Berri ambae ni mwanachama mashuhuri wa upinzani wa Hezbollah nchini humo.Mada kuu katika duru ya mwanzo ya majadiliano yatakayofanywa kati ya Kansela Merkel na waziri mkuu Siniora,ni uhusiano wa nchi hizo mbili.Kwa mujibu wa duru ya serikali ya Lebanon,Siniora vile vile atamuarifu Merkel juu ya mgogoro wa kisiasa ndani ya nchi yake.

Kwa upande mwingine,Merkel atazungumza juu ya mchango unaotolewa na Ujerumani katika vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa UNIFIL.Ujerumani inaongoza kikosi cha kama wanamaji 1,700 wa kike na kiume katika pwani ya Lebanon,kuambatana na azimio la Umoja wa Mataifa.Wanamaji hao wanapiga doria katika pwani ya Lebanon,ili kuzuia usafirishaji haramu wa silaha kwa kundi la Hezbollah.Vikosi hivyo,ni sehemu ya wanajeshi 13,000 wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani Lebanon-(UNIFIL) kwenye mpaka wa Israel na Lebanon.

Suala la Mashariki ya Kati limepewa kipaumbele na Kansela Merkel,ambae hivi sasa ameshika wadhifa wa urais unaozunguka kila miezi sita katika Umoja wa Ulaya.Wakati wa ziara yake ya Mashariki ya Kati,Merkel amesema mkutano wa kilele wa nchi za Kiarabu uliofanywa hivi karibuni mjini Riyadh unatoa matumaini ya kupatikana maendeleo katika utaratibu wa amani wa Mashariki ya Kati.Baada ya kukutana na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert mjini Jerusalem na rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah,Merkel alisema ni matumaini yake kuwa kutapatikana suluhisho la kuwepo mataifa mawili ambapo Israel na Palestina zitaweza kuishi pamoja kwa amani katika mipaka inayotambulika na kuwepo ujirani mwema.

Kansela Merkel anakamilisha ziara yake ya Mashariki ya Kati iliyompeleka Jordan,Israel, Maeneo ya Wapalestina na Lebanon kwa kuitembelea manowari ya Kijerumani “Brandenburg” katika bandari ya Beirut.