1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karadzic alalamika kukamatwa kwake.

Abdulrahman, Mohamed1 Agosti 2008

Afichua kulikuwa na makubalino ya siri.

https://p.dw.com/p/EoVw
Radovan Karadzic akiingia mahakamani mjini The Hague. kawa mara ya kwanza Alhamisi iliopita akishtakiwa kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita na dhidi ya binaadamu.Picha: AP

Wakati kiongozi wa zamani wa waserbia wa Bosnia Radavan Karadzic akisubiri kufikishwa tena mbele ya mahakama ya umoja wa mataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague tarehe 29 mwezi huu, wachambuzi wanahisi huenda akatumia mbinu sawa na iliotumiwa na kiongozi wa zamani wa Serbia Slobodan Milosevic alipofikishwa mahakamani. Mbinu yenyewe ni kujaribu kuiabisha Marekani kuwa iliandaa makubaliano ya siri, vilipomalizika vita vya Bosnia.

Karadzic aliyefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza jana baada ya kukamatwa wiki iliopita, kufuatia msako wa miaka 13 alipokua mafichoni, alidai alifikia makubaliano na mpatanishi kwa niaba ya Marekani richard Holbrooke wakati wa kumalizika vita vya Bosnia vilivyoripuka 1992-1995, Chini ya makubaliano hayo Karadzic alitakiwa kujiondoa katika shughuli aza umma.

Mshitakiwa huyo alimwambia jaji Alphons Orie kwamba makubaliano hayo yameyaweka hatarini maisha yake akiongeza ," Nikikabiliwa na hatari ya kuangamizwa kwa sababu nilitoa ahadi.

Bw Holbrooke ambaye ni muasisi wa makubaliano ya amani ya Dayton yaliomaliza vita vya Bosnia na kusainiwa na pande kuu husika ambapo watu 100.000 waliuwawa, amekanusha kwamba kulikua na makubaliano ya aina yoyote.

Lakini familia ya Karadzic inasemekana imekua ikidai wakati wote kwamba ina ushahidi juu ya makubaliano hayo ya siri. Florence Hartmann, msemaji na mshauri wa mwendesha mashitaka wa zamani wa uhalifu wa kivita Bibi Carla del Ponte, alisema Bw Holbrooke aliahidi kwamba Karadzic hatofikishwa katika mahakama ya The Hague ikiwa atajiondoa katika shughuli za umma.

Bibi hartmann anadai kwamba hata majeshi ya shirika la kujihami la magharibi NATO hayakumtia nguvuni Karadzic wakati alikua akipita mbele ya macho yao ama kwenda ofisini au nyumbani kwake.

Hoja nyengine inayotajwa ni kwamba Marekani, Ufaransa na Uingereza ambazo zote zilihusika katika juhudi za kuleta amani nchini Bosnia, zilikua na wasi wasi kwamba kumkamata Karadzic kungezusha ukosefu zaidi wa usalama na hivyo walitaka kuepusha mauaji zaidi miongoni mwa wanajeshi wao.

Wanasema hivi sasa Karadzic ambaye ameiambia mahakama anataka kujitetea mwenyewe huenda akaomba watu kama Holbrooke pamoja na viongozi wa zamani wa Marekani, Ufaransa na Uingereza waitwe mahakamani kutoa ushahidi.

Marekani imekana mara kadhaa kuwa haikumuahidi kitu Karadzic ili badala yake awe huru na kuingia mafichoni .Ufaransa ambayo marubani wake wawili waliokamatwa na wanajeshi wa Kiserbia wa Bosnia muda mfupi kabla ya kusainiwa makubaliano ya amani ya Dayton pia imekanusha madai hayo.

Baada ya kufikishwa mahakamani jana, jaji alimua Karadzic afikishwe tena mahakamani tarehe29 ya mwezi huu wa Agosti kujibu kama anakiri mashitaka yanayomkabili au la,huku wataalamu wakiashiria kwamba huenda ikachukua miezi kadhaa kabla ya kesi yenye kuanza.