1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karzai asema madai ya hila yameongezwa chumvi

Thelma Mwadzaya17 Septemba 2009

Tume ya uchaguzi nchini Afghanistan imeyatangaza matokeo mapya baada baadhi ya kura kuhesabiwa upya.Hatua hiyo ilichukuliwa kwasababu ya malalamiko kwamba matokeo hayo yalikuwa na hila.

https://p.dw.com/p/Jigb
Rais Hamid Karzai wa AfghanistanPicha: AP

Kwa upande wake Rais Hamid Karzai wa Afghanistan anaamini kuwa madai hayo yameongezwa chumvi na shughuli nzima ya uchaguzi inaaminika.Wakati huohuo waangalizi wa Umoja wa Ulaya walioshiriki katika zoezi hilo wamethibitisha kuwa kura milioni 1.5 zilikuwa na hila kwahiyo matokeo hayo ni ya muda mpaka pale uchunguzi utakapofanyika.

Matokeo ya muda yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Afghanistan yanaonyesha kuwa Rais Hamid Karzai anaongoza kwa zaidi ya asilimia 54 ya kura zote.Mpinzani wake mkuu Abdulla Abdullah ameripotiwa kuwa amepata kiasi cha asilimia 29 ya kura zote baada ya baadhi ya kura hizo kuhesabiwa upya.

Hivi ndivyo mambo yalivyokuwa katika chumba cha kuhesabia kura.

Hila ya milioni moja u nusu

Afghanistan Wahlfälschung EU Vertreter in Kabul
Waangalizi wa Umoja wa UlayaPicha: DW

Hata hivyo waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya wameonya kuwa kiasi cha kura milioni moja u nusu zina hila kama anavyoeleza Dimitra Iannou ,naibu mwenyekiti wa ujumbe huo''Tumezihesabu jumla ya kura milioni 1.5 zilizokuwa na hila.Kura milioni 1.1 kati ya hizo ni za Hamid Karzai,laki tatu za Abdullah na alfu 92 ni za Basildon.''

Matokeo kamili yatatangazwa pale kamisheni inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa itakapokamilisha uchunguzi wake kamili wa madai hayo ya hila na udanganyifu.Hilo limetiliwa mkazo pia na Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alipouzuru mji wa Munich.Ujerumani ina jumla ya vikosi 3700 nchini humo vinavyoziunga mkono juhudi za ukarabati.

Tutendeeni haki

Rais Karzai kwa upande wake bado hajajitangaza mshindi na amesisitoza kuwa uchunguzi huo sharti ukamilike kwanza.Kiongozi huyo pia aliyapuuza madai kwamba hila na udanganyifu uliotokea ulikuwa mkubwa sana jambo ambalo huenda likasababisha uchaguzi huo kufutiliwa mbali na awamu ya pili kufanyika.

Rais Karzai aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ikiwa ni mara ya kwanza tangu uchaguzi huo wa Agosti 20 kufanyika. Rais Karzai alitoa wito wa nchi yake kutendewa haki wakati wa uchunguzi wa malalamiko hayo''Raia wa Afghanistan walikuwa na kipindi kigumu ili kufanikisha uchaguzi huu.Hicho ndicho ninachokitaka ..kuuheshimu ushujaa wa raia waliojitolea.Ikiwa hila ilitokea sharti ichunguzwe ila kwa kudumisha haki na bila uonevu''.

Mkwamo wa kisiasa

Endapo matokeo hayo yatazua utata hilo huenda likaiwia Marekani vigumu inayojiandaa kuongeza idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan kwa minajili ya kuziimarisha serikali za Afghanistan na Pakistan katika mapambano dhidi ya ugaidi.Kulingana na Shirika la utafiti wa masuala ya Usalama na Maendeleo,ICOS lililoko London,Uingereza njia pekee ya kuiokoa Afghanistan ni kuunda serikali ya muda.

Ripoti ya Shirika hilo inaonya kuwa ikiwa hatua hiyo itasusua mkwamo wa kisiasa huenda ukatoea wakati ambapo wanamgambo wa Taleban wanaimarisha mashambulizi yao.

Tume ya Uchaguzi ya Afghanistan inaendelea na shughuli ya kuzihesabu tena kura ila bado haijatoa muda kamili itakapoikamilisha shughuli hiyo.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya -AFPE/DPAE

Mhariri:M.Abdul-Rahman