1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Karzai azivunja kampuni binafsi za usalama, amezipa miezi minne.

Abdu Said Mtullya17 Agosti 2010

Makampuni binafsi yanayolinda usalama nchini Afghanistan yatavunjwa.

https://p.dw.com/p/Opgo
Rais Karzai atoa amri ya kuyavunja makampuni binafsi ya ulinzi nchini:Picha: AP

Rais Hamid Karzai leo ametoa amri ya kuyafunga makampuni yote binafsi yanayolinda usalama nchini Afghanistan.Rais Karzai ametoa muda wa miezi minne kwa makampuni hayo kuvunjwa.

Rais Karzai amefikia uamuzi huo ili kuepusha matumizi mabaya ya silaha ambayo tayari yameshasabaisha maafa.Amri iliyotolewa na huyo inasema hatua ya kuyavunja makampuni binafsi ya usalama yanayoajiri watu hadi alfu 40 imechukuliwa ili kuzuia kilichoitwa hitilafu na matumizi mabaya ya silaha na vifaa vya kijeshi.

Mashirika yote binafsi ya usalama ya ndani na ya kutoka nje yatakumbwa na amri ya rais Karzai.Hata hivyo makampuni ya ulinzi yanayolinda usalama ndani ya maeneo yanayotumiwa na balozi hayataguswa na sheria hiyo ,licha ya ofisi ya rais kusema wiki iliyopita kwamba makampuni yote yatahusika na amri hiyo.

Hatua ya kuyafunga mashirika hayo binafsi ya ulinzi inaambatanishwa na ratiba muhimu ya rais Karzai juu ya majeshi ya wazalendo wa Afghanistan kuchukua jukumu lote la usalama kutoka kwa majeshi ya nje ,kuanzia mwaka wa 2014 .

Askari 150,000 kutoka nje wanalinda usalama wa Afghanistan.

Mashirika binafsi ya usalama yasiyokuwa chini ya udhibiti wa serikali ya Afghanistan, kwa muda mrefu yamekuwa karaha kubwa kwa waafghani, Marekani na kwa majeshi ya Nato hasa baada ya kutokea kashfa nyingi.

Jeshi la Marekani linayaajiri baadhi ya mawakala binafsi wa ulinzi na wizara ya ulinzi ya Marekani iliarifu wiki iliyopita kwamba ilikuwa inafanya mazungumzo na serikali ya rais Karzai juu ya suala la ulinzi.

Makampuni hayo yanatoa ulinzi kwa majeshi ya kimataifa,kwa watumishi wa wizara ya ulinzi ya Marekani , Umoja wa Mataifa na kwa mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali.Ofisi za kibalozi na mashirika ya habari ya nchi za magharibi pia yanalindwa na mawakala hao binafsi .

Lakini watu wa Afghanistan wanayashutumu makampuni hao binafsi. Wanasema makampuni hayo yanajikweza na yanafanya ujeuri hasa barabarani.

Rais Karzai pia amelalamika kwa kusema kwamba makampuni binafsi ya ulinzi yanalundikiza kazi ya majeshi ya usalama ya Afghanistan na kwamba yanachukua nyenzo ambazo vinginevyo zinahitajika kwa ajili ya mafunzo ya jeshi na polisi.

Hadi itakapofika januari mosi mwaka ujao,makampuni binafsi ya ulinzi yanatakiwa yavunjwe nchini Afghanistan .

Mwandishi Mtullya Abdu/AFPE/

Mhariri/.....Josephat Charo.