1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni yatolewa kuhusu kashfa ya Kombe la Dunia 2006

27 Oktoba 2015

Mjadala umepamba moto Ujerumani wakati umma ukitaka kujua kama kweli uamuzi uliopelekea Ujerumani kuandaa dimba la kombe la dunia mwaka 2006 ulikuwa wa halali au la. Kuna madai uamuzi huo ulitokana na kununuliwa kura

https://p.dw.com/p/1Gueu
FIFA Theo Zwanziger
Picha: picture-alliance/dpa/E. Leanza

Kuna wanaozungumzia kuhusu akaunti za siri - kasheshe hiyo inatishia kuichafua hadhi ya soka la Ujerumani. Kutokana na kasheshe hiyo, kocha mashuhuri wa zamani wa vilabu vya Dortmund na Bayern Munich, Ottmar Hitzfeld ametoa wito wa kuitishwa meza ya duara hasa kutokana na malumbano kati ya mwenyekiti wa zamani wa shirikisho la kabumbu la Ujerumani DFB Theo Zwanziger na mrithi wa kiti chake Wolfgang Niersbach pamoja na kufichuliwa siri eti kumekuwepo na makasha ya siri kwa ajili ya maombi ya Ujerumani kuandaa fainali za kombe la dunia mwaka 2006. "Nnasikitika sana na yanayotokea katika shirikisho la DFB. Wote wanaogombana hivi sasa wameandika historia ya kusisimua na kufanikiwa pakubwa katika dimba la Ujerumani" amesema Ottmar Hitzfeld kupitia kituo cha matangazo cha Sky 90. "Yote yamevurugika, kilichosalia sasa ni kuketi katika meza ya majadiliano.

Kila la kufanya lazima lifanywe,ili kuiwezesha kamati ya maandalizi ya kombe la dunia kukutana upya, pawepo atakaesimamia majadiliano na atakaejibu masuali moto moto yatakayojitokeza. Ni suala la kurejesha uaminifu ambao unaonyesha kutoweka" amesisitiza Ottmar Hitzfeld anaeiongoza hivi sasa timu ya taifa ya Uswisi.

Itafaa kusema hapa kwamba ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa mjini Frankfurt inachunguza,kutokana na tuhuma zilizozagaa kuhusu kisa hicho,kama kuna dhana za awali zinazoweza kupelekea kuanzishwa uchunguzi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/SID
Mhariri: Gakuba Daniel